Logo
Sunday, 29 November 2015 00:00    PDF 

HOTUBA YA MHESHIMIWA WAZIRI MKUU ATAKAYOSOMA KWA NIABA YA MHESHIMIWA RAIS KATIKA KUFUNGA MAADHIMISHO YA MIAKA 20 YA DAYOSISI YA PWANI YA KANISA LA AFRICAN INLAND CHURCH TANZANIA YATAKAYOFANYIKA KWENYE UKUMBI WA PTA - VIWANJA VYA MWL. NYERERE, DAR ES SALAAM,TAREHE 29 NOVEMBA 2015

 


Mheshimiwa Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la AIC Tanzania - Askofu Silas Kezakubi;

Mheshimiwa Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la AIC Kenya - Askofu Dr. Silas Yego;

Mheshimiwa Baba Askofu wa Dayosisi ya Pwani - Askofu Charles Salalah;

Waheshimiwa Ma-Baba Askofu kutoka Dayosisi mbalimbali za Kanisa la AIC-Tanzania;

Waheshimiwa Maaskofu Wakuu Wastaafu, Baba Askofu Methusela Nyagwaswa na Askofu Daniel Nungwana;

Mheshimiwa Said Meck Sadick, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam;

Mheshimiwa Katibu Mkuu Kiongozi wa AIC Tanzania, Mchungaji Zakayo Bugota;

Mheshimiwa Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Pwani, Bwana Lucas Singili;

Waheshimiwa Ma-Katibu Wakuu wa Dayosisi za Kanisa la AIC Tanzania;

Mheshimiwa Mchungaji Tony Sargent - Mshirika mwenza wa shughuli za Kanisa Kutoka Uingereza;

Wachungaji; Wamisionari na Viongozi mbalimbali wa Kanisa;

Viongozi wa Serikali;

Waumini;

Mabibi na Mabwana.

Uhuru wa Yesu! Bwana Yesu asifiwe!

Napenda nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha wote kukusanyika kwa pamoja hapa siku ya leo. Niko hapa nikimwakilisha Mheshimiwa John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye awali alikubali kuja kufunga maadhimisho haya. Hata hivyo, kutokana na kukabiliwa na majukumu mengine ya kitaifa imempendeza kunituma mimi nimwakilishe. Anaomba radhi kwa kushindwa kuwa nanyi na anawaombea mema katika kuhitimisha maadhimisho yenu na katika majukumu yenu ya kila siku.

Ninapenda pia kuwashukuru wote walioandaa maadhimisho haya na wote waliohakikisha yanafanikiwa kwa kiwango hiki. Nawapongeza sana.

Ndugu Viongozi na Waumini,

Leo nahudhuria kwenye maadhimisho haya ikiwa ni katika matukio yangu ya mwanzo kuhudhuria nikiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama mnavyojua Uchaguzi Mkuu ulifanyika tarehe 25 Oktoba 2015. Wengi tunakubaliana kuwa ulikuwa uchaguzi uliofanyika kwa amani na utulivu. Kwa niaba ya Serikali nawashukuru wote waliojitokeza kupiga kura na wote walioilinda amani ya nchi yetu katika kipindi hicho cha uchaguzi. Aidha, nawashukuru kwa kumchagua Mheshimiwa John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hata hivyo, tusingeweza kufanikisha uchaguzi huo wenyewe bila Baraka za Mungu. Nawashukuru wote kwa kuliombea Taifa letu liweze kupita katika kipindi hicho likiwa Taifa moja lenye amani na utulivu. Asanteni sana.

Niwashukuru pia wote wanaoendelea kuliombea Taifa letu amani. Amani ndio msingi wa maendeleo yoyote ya binadamu. Tumetoka kusikia wimbo mzuri wa Kikundi cha AIC Makongoro Vijana (Wanakekundu) ukitoa ujumbe mzito kuhusu amani. Nawapongeza sana wanakekundu kwa ujumbe wenu, tumeusikia na sina shaka kila mmoja wetu atauzingatia. Asanteni sana.

Mafanikio ya Kanisa la AICT

Ndugu Waumini, Mabibi na Mabwana,

Nimekuwa nikisikia habari za Kanisa la African Inland Church Tanzania kwa muda mrefu. Nimekuwa nikifuatilia kwa makini shughuli zenu hapa Nchini. Ninafahamu kanisa lilianza katika mazingira magumu sana. Lakini kwa baraka za Mungu AIC Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuhudumia jamii kiroho na kimwili. Nina taarifa kuwa Kanisa lilianzia stesheni ya Nassa mwaka 1909 wakati huo likiwa linaitwa African Inland Mission - AIM. Jina la Kanisa lilibadilika mwaka 1958 na kuwa African Inland Church Tanzania. Hivyo, jina AICT lilianza kutumika mwaka 1958 na leo tutatoa vyeti kwa Waumini wa kwanza kujiunga na AICT mwaka huo wa 1958.

Historia ya Kanisa inaonesha kuwa lilikuwa chini ya Askofu mmoja hadi mwaka 1993 ambapo zilianzishwa Dayosisi tano na sasa naambiwa mnazo Dayosisi sita. Dayosisi yetu ya Pwani ilianzishwa mwaka 1994 ndio maana leo tuko kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwake.

Nimeeleza haya si kwa kuwa hamyajui bali nataka kuonyesha kuwa wote tunayo haki na sababu ya kusherehekea siku ya leo. Safari iliyotufikisha leo ilikuwa ni ndefu yenye changamoto nyingi ambazo kwa juhudi na uvumilivu wa Viongozi wa Kanisa na Waumini na baraka za Mwenyezi Mungu zimeweza kutatuliwa. Ni wazi kuwa kazi kubwa imefanyika. Nawapongeza wote waliochangia kutufikisha hapa na kujenga msingi imara ambao utatumiwa na Kanisa la AICT la siku zijazo.

Huduma za Kijamii

Ndugu Viongozi na Waumini,

Katika kipindi hiki cha miaka 20 pamoja na kuwajenga na kuwasaidia Watanzania kiroho, mmekuwa pia mkiwasaidia kimwili kwa kuwawezesha kupata elimu na huduma za afya. Nina taarifa kuwa mnayo shule ya sekondari iitwayo AICT Tanner Girls’ Secondary School iliyoko Pahi, Kondoa, Shule ya Sekondari ya Askofu Kisula iliyoko Mkoani Arusha na shule ya Awali na Msingi ya Amani iliyoko Pande, Mkoani Tanga. Bila shaka mnawakumbusha na kuwasaidia Wanafunzi wenu kutekeleza maelekezo ya Biblia Takatifu katika Kitabu cha Mithali, Aya ya Nne, Msitari wa 13 usemao “Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako.”

Kwa upande wa afya mnazo zahanati mbili Wilayani Kondoa na mnajishughulisha na utoaji wa elimu kuhusu namna ya kujikinga au kuishi na virusi vya UKIMWI. Kwa niaba ya Serikali nawapongeza kwa juhudi zenu na kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutoa huduma za elimu na afya kwa Watanzania. Tunatambua kuwa pamoja na juhudi zetu zote, kama Serikali hatuwezi kutoa huduma hizo kwa ukamilifu kwa kila Mtanzania bila msaada wenu kama Taasisi za Dini na Sekta Binafsi. Asanteni sana na Hongereni.

Huduma za Kiuchumi

Mheshimiwa Baba Askofu Mkuu,

Ningependa kuwaomba muendelee pia kuisaidia Serikali katika kuboresha hali za kiuchumi za Waumini wenu na Watanzania kwa ujumla. Mnaweza kushiriki katika kuwawezesha waumini kuunda vikundi mbalimbali vya uzalishaji na kuvisaidia kupata mitaji, kuwa na uongozi bora, kupata elimu ya biashara, nk. Wahimizeni kufanya kazi kwa bidii na kwa maarifa wakati wote. Sasa ni wakati wa kazi tu. Wote mnakumbuka kuwa Biblia Takatifu kwenye kitabu cha Wathesalonike, Aya ya Tatu, Msitari wa Kumi inatueleza kuwa ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Ni imani yangu kuwa Waumini mmoja mmoja au katika vikundi wakiwa na nguvu kiuchumi, kanisa litakuwa na nguvu kiuchumi na vivyo hivyo kwa Serikali. Hivyo, nawaomba kadiri Mungu atakavyowajalia muone uwezekano wa kuimarisha eneo hili la uchumi kwa waumini wenu.

Umuhimu wa maadili mema kwa jamii

Ndugu zangu Waumini,

Bila shaka mtakubaliana nami kuwa kadiri Watanzania tunavyoongezeka kwa idadi, na kutokana na utandawazi na matumizi ya TEHAMA, idadi ya watu wasiokuwa na maadili mema inazidi kuongezeka. Tunafahamu kuwa zipo dawa za kulevya, uasherati, wizi, ubadhilifu, rushwa n.k miongoni mwa jamii yetu. Sisi kama Waumini tunawategemea Viongozi wa Dini kukemea haya. Nyie mko mbele yetu na sisi kama Waumini wenu tukitegemea mtuongoze kutenda yaliyo mema. Katika Injili ya Mathayo, Aya ya Tano, Mstari wa 14 hadi wa 16. Mtume Mathayo ameandika maneno ya Yesu akiwaambia Wanafunzi wake kwamba: “Ninyi ni nuru ya Ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya Watu wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye Mbinguni.” Tuungane na Mtume Mathayo kwa tafsiri kuwa ninyi mmetumwa kueneza maadili mema na kujenga afya za watu kiroho ili wawe pia na afya kimwili.

Wito wangu kwenu, nawaomba muisaidie Serikali katika kujenga Maadili mema mbele za jamii. Mnalo kundi kubwa la Waumini wanaowategemea. Tutumie fursa ya kuwa na kundi hili la waumini kuwapelekea habari njema za kiroho ili wawe na utamaduni wa kuwa na matendo mema kwa kutumia imani zao. Tuwakumbushe wajibu wao wa kuishi maisha yenye Maadili Mema ya Kiroho. Tuwajengee imani njema inayoambatana na matendo mema. Tukishirikiana vizuri kati ya Serikali na Viongozi wa Dini tutajenga Taifa lenye Watu Waadilifu na hivyo kupunguza kero nyingi zinazoikabili jamii katika Nchi yetu.

Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano ulielezwa vizuri na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati akilihutubia Bunge tarehe 20 Novemba 2015. Serikali imeanza kukabiliana na upotevu wa mapato ya Serikali na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma. Nia yetu ni kuhakikisha kila kinachopaswa kukusanywa kama mapato ya Nchi kikusanywe na kitumike kwa masuala ya msingi kwa ustawi wa Watanzania wote na si watu wachache.

Tunaomba mtuunge mkono na mtuwezeshe kufanya kazi hiyo. Tunaomba ushirikiano wakati wote na tunaomba muendelee kutuombea katika sala zenu za kila siku ili tuweze kuongoza kwa haki na kuwaletea Watanzania wote maendeleo. Kwa maana imeandikwa kwenye Kitabu wa Mithali, Aya ya 29, Mstari wa Pili kuwa, “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi, Bali mwovu atawalapo, watu huugua.

Hitimisho

Baba Maaskofu, Mabibi na Mabwana,

Baada ya kusema hayo, Niwashukuru tena kwa kumwalika Mheshimiwa Rais na kwa kuniruhusu kuwa nanyi siku ya leo. Nawatakia heri mnaporudi nyumbani, nawaombea afya njema na mafanikio katika maisha yenu.

Mungu awabariki,

Asanteni kwa kunisikiliza.

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved