Logo
Friday, 11 December 2015 00:00    PDF 

HOTUBA YA MHESHIMIWA MAJALIWA KASSIM MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUTOA TUZO YA MWAJIRI BORA WA MWAKA TAREHE 11 DESEMBA, 2015 KATIKA UKUMBI WA MLIMANI CITY, DAR ES SALAAM

Mheshimiwa Almas A. Maige (MB), Mwenyekiti wa

Chama cha Waajiri Tanzania (ATE);

Mheshimiwa Saidi Meck Sadiki, Mkuu wa Mkoa wa Dar-es-Salaam;

Bw. Erick Shitindi, Katibu Mkuu, Wizara ya Kazi na Ajira;

Bi. Zuhura Muro, Makamu Mwenyekiti wa ATE;

Bw. Anthony Rutabanzibwa, Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya ILO

Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda;

Dkt. Aggrey K. Mlimuka, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE;

Bw. Nicholas Mgaya, Katibu Mkuu wa TUCTA;

Waheshimiwa Wajumbe wa Bodi ya ATE;

Washiriki wa Tuzo ya Mwajiri Bora wa Mwaka huu;

Wadhamini wa shindano hili;

Wageni Waalikwa;

Waandishi wa Habari;

Mabibi na Mabwana.

Awali ya yote napenda kutoa shukrani za dhati kwa kunikaribisha kuwa mgeni rasmi wa tukio hili muhimu la kutoa TUZO YA MWAAJIRI BORA WA MWAKA 2015 maarufu kama “Employer of the Year Award (EYA) 2015.” Katika hafla hii waajiri watapata tuzo katika makundi mbalimbali ya ukuzaji biashara.

Kama ambavyo baadhi yenu mnafahamu, mwaliko huu ulikuwa wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye awali alitarajiwa awe Mgeni Rasmi. Hata hivyo kutokana na majukumu mengi imempendeza nimuwakilishe jioni ya leo. Mheshimiwa Rais anawasalimu na kuwatakia kila la kheri katika kufanikisha shughuli yenu.

Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais napenda kuwashukuru kwa mchango wenu mkubwa katika kukuza na kuboresha uchumi wa taifa letu kwa kubuni fursa mbalimbali za ajira. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya kazi pamoja kwa ushirikiano chini ya kauli mbiu ya: “HAPA KAZI TU.” Lengo letu ni kuona kwamba tunafanya kazi kwa bidii ili kufikia maendeleo endelevu kwa ajili ya wananchi wetu.

Ukuaji wa Uchumi

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tanzania tunashirikiana na watu kutoka mataifa mbali mbali kwa njia ya uwekezaji katika sekta kama vile kilimo, viwanda, huduma na sekta ya mafuta na gesi na nyingine nyingi. Kupitia ushirikiano huo, uchumi wetu umendelea kukua kwa kasi ya asilimia saba (7) ambapo tunatakiwa kwenda kwa kasi zaidi ili tuweze kujenga taifa lenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025. Ninaamini kwamba lengo hili linawezekana kama tutafanya kazi kwa bidii na kushirikiana.

Mchango wa Waajiri Kisekta

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Serikali inatambua mchango wa waajiri wetu toka sekta zote hususani sekta ya kilimo ambayo ndio uti wa mgongo wa taifa letu. Sekta hii hutoa ajira kwa asilimia 75 hasa kwa watu wa vijijjini. Aidha, Sekta hii huchangia asilimia 95 ya uzalishaji wa chakula licha ya changamoto nyingi zinazowakabili wakulima. Kupitia kilimo tunapata asilimia 30 ya fedha za kigeni ambazo pia ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wetu.

Hivyo natumia fursa hii ya mwanzo kabisa kuomba waajiri kuwekeza zaidi na kwa wingi katika eneo hili la Kilimo. Tunaweza kuweka kipaumbele kuanzisha na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji, na kuwekeza katika zana za kilimo ili kuongeza mazao ya chakula na biashara.

Ahadi za Serikali

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Ni hivi karibuni tumemaliza uchaguzi Mkuu katika nchi yetu. Niwashukuru wote kwa kufanya uchaguzi kwa amani na utulivu. Moja ya vitu tulivyoahidi wakati wa kampeni zetu ilikuwa ni kujenga Tanzania yenye kutegemea uchumi wa viwanda. Hatukusema hivyo ili tupate au kuvizia kura zenu tu, bali huo ndio msimamo na malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kupitia sekta ya viwanda, kuna mpango wa kuongeza ajira kwa asilimia 40 mpaka kufikia mwaka 2020. Hili ndilo lengo letu kwa kipindi hiki kifupi. Tutakapokuwa na viwanda vyetu, hii si tu itasaidia kuongeza ajira bali pia thamani ya bidhaa zetu hasa za kilimo na madini itaongezeka mara dufu. Tunataka tupunguze kuuza bidhaa ghafi nje. Ni lazima tutambue kuwa kila tunapouza bidhaa ghafi tunahamisha ajira kwa mataifa mengine.

Wajibu wa Mwajiri katika kukuza Ajira

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Kutokana na hali halisi ya kujenga uchumi duniani, mimi ninaamini huu ni wakati muafaka kutumia bidhaa za viwanda vyetu na kuuza ziada nje ya nchi. Hata hivyo, changamoto kubwa ni kuendesha biashara zetu kwa kuzingatia maadili ya uzalishaji ikiwemo kulipa kodi. Aidha, tunatakiwa kujitangaza kupitia majina ya bidhaa zinazozalishwa viwandani mwetu kama vile nguo, viatu, mafuta ya kupikia na nyingine nyingi na hii itaongeza uzalishaji na kuinua ushindani nchini. Matarajio yetu ni kwamba waajiri wengi mlioko hapa mnaendesha biashara zenu kwa uaminifu na ndio maana mkashiriki shindano hili la Mwaajiri Bora wa Mwaka huu.

Aidha, ninaamini kuwa waajiri wote mtaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali za kuongeza ajira kwa vijana wetu wa ndani badala ya kuajiri kutoka nje ya nchi kwa kazi zinazoweza kufanywa na vijana wetu wa Kitanzania.

Naomba niwakumbushe tena wajiri kuendelea kufanya kazi kwa karibu sana na serikali ili kutimiza azma ya kufikia mapinduzi ya viwanda nchini. Hata hivyo katika kutimiza hili, tunatakiwa kufuata sheria na taratibu za nchi ili kudumisha mahusiano mema kibiashara. Tutakapo jenga utamaduni wa kushirikiana ndipo tatakapoweza kuchangia kwa karibu ukuaji wa uchumi wetu kwa manufaa ya taifa letu.

Huduma kwa Wateja

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Wakati huu tunapoendelea kuboresha uchumi wetu, ni muhimu sana kutoa huduma nzuri kwa wateja wetu. Mpango wetu wa kuboresha uchumi unaenda sanjari na kupambana na umasikini ili kupunguza pengo kati ya matajiri na mafukara. Nawaomba waajiri kushirikiana na serikali ili kujenga miundo mbinu kama vile barabara, njia za reli, na huduma ya afya hapa nchini. Msikubali kuruhusu Wazembe na wasio na maadili kuvuruga juhudi zetu katika kukuza uchumi wan chi yetu. Serikali iko makini katika hili. Suala la kutoa huduma mbovu na uzembe hakutavumiliwa hata kidogo.

Vyanzo vya Mapato

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Nchi yetu imendelea kupata neema zaidi katika kupata vyanzo vya mapato zaidi ambavyo tukivitumia vizuri tutakuwa moja ya mataifa yenye uchumi imara duniani. Ugunduzi wa mafuta na gesi katika siku za hivi karibuni unaashiria kupiga hatua kiuchumi endapo kuna usimamizi na ufuatiliaji wa uhakika. Baadhi ya mataifa yalipiga hatua kimaendeleo kupitia uchimbaji wa gesi na mafuta. Kwa maana hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano tutahakikisha tunasimamia vizuri Sheria ya Mafuta na Gesi ya Mwaka 2015 kuhakikisha uzalishaji wa rasilimali hizi unaleta manufaa kwa wananchi wote.

Aidha, mbali na sheria hiyo, bado tunatarajia kurekebisha baadhi ya sheria kama vile Sheria ya Mafuta ya mwaka 1980, Sheria ya Petroli ya mwaka 2008 na Sheria ya Ardhi ya mwaka 1999. Marekebisho hayo yote yanalenga kujenga mazingira bora kibiashara ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Ukusanyaji kodi, usimamizi na udhibiti wa mapato ya ndani ni eneo jingine muhimu sana. Zoezi hili lilitiliwa mkazo kutoka Serikali zilizotangulia na awamu ya nne imefanya kazi kubwa ya udhibiti wa mianya ya ukwepaji ulipaji kodi.

Kutokana na jitihada hizo, Serikali ya Awamu ya Nne iliweza kukusanya kodi kutoka shilingi bilioni 177 kwa mwezi, mwaka 2005 hadi shilingi bilioni 900 kwa mwezi mwaka 2015. Haya ni mafanikio ya kuridhisha ambayo yameweza kupatikana.

Rasilimali Watu

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Natambua kuwa sehemu kubwa ya kazi zenu hutegemea rasilimali watu ambapo kuna uhitaji mkubwa wa ujuzi unaostahili. Kwa kuliona hilo, Serikali imechukua hatua ya kuandaa mkakati kabambe kwa kutoa elimu ya sekondari bure. Nafahamu pia kuwa waajiri wanapendelea kuajiri wafanyakazi wenye ujuzi ambao hata hivyo huandaliwa kupitia mafunzo na usimamizi wa kutosha. Hivyo nawataka waajiri muunge mkono juhudi za Serikali katika kutoa elimu bure kwa kuweka mkakati wa kuboresha ujuzi mahali pa kazi. Waswahili wanasema “hata ng’ombe unapaswa kumpa nyasi, maji na mahitaji mengine ili kupata maziwa ya kutosha”. Naamini Chama cha Waajiri (ATE) kitakuwa mstari wa mbele katika kuwapa mafunzo Wafanyakazi yanayoendana na mahitaji ya soko la ajira ili kuongeza uzalishaji na ushindani nchini.

Kuboresha Mitaala

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Tunao mpango wa kuboresha na kupanua mitaala yetu ya kufundishia ili kuhakikisha unakidhi mahitaji ya soko la ndani na nje. Kwa kuzingatia hilo, tumeona ni vyema kuongeza michepuo mingine kama vile michezo na burudani, ubunifu na uvumbuzi, ujasiriamali na kuendeleza vipaji na mengine mengi. Mabadiliko haya yanalenga kuondoa kasumba iliyojengeka kwa wasomi ya kuzurura na vyeti wakitafuta kazi badala ya kuazisha fursa za ajira kwa kujiajiri wao wenyewe.

Serikali itatoa kipaumbele kwa wale waliojiajiri kwa kuanzisha miradi ya maendeleo kwa lengo la kuwapa nguvu ya kusimama wao na nguvu yao katika biashara. Nitumie fursa hii kuomba mabenki na taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa masharti nafuu hasa kwa wasomi wanaomaliza vyuo ili kupanua wigo wa ajira kwa kuweza kujiajiri na kukuza uchumi wetu.

Mchango wa SMEs

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Nimevutiwa sana kuona kuwa utoaji wa Tuzo hii umekuwa ukitoa kipaumbele kuwatambua na kuwajali wawekezaji wadogo na wa kati (Small and Medium Enterprises - SMEs). Hili ni kundi la msingi sana katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu kwani hutoa ajira kwa watu wengi kupitia sekta isiyo rasmi. Serikali ina mpango kamambe wa kujenga mazingira rafiki kibiashara kwa kujenga miundo mbinu stahiki ili kukuza na kupanua sekta binafsi na uwekezaji nchini kupitia SMEs. Aidha, Serikali imeshaanza kuchukua hatua dhidi ya masuala yanayochangia kuongezeka kwa gharama za kufanya biashara nchini. Hatua hizo zimechukuliwa dhidi ya rushwa na vitendo vya kifisadi.

Nawataka waajiri wenye nia njema na nchi yetu kuepuka kutoa au kupokea rushwa maana huyu ndie adui mkubwa katika taifa letu. Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kusema, naomba kunukuu:

“Rushwa na [Ufisadi] havina budi kushughulikiwa bila huruma kwa sababu naamini rushwa na ufisadi ni adui mkubwa kwa ustawi wa watu kuliko vita.” Mwisho wa kunukuu.

Alichokisema Mwalimu Nyerere kama Baba na mwasisi wa taifa hili alitutaka kupambana na rushwa na ufisadi bila woga wala upendeleo. Aidha, huo ndio msimamo wa serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Naomba Watanzania wenzangu tuachane kabisa na tabia hii chafu ya kutoa au kupokea rushwa. Tujijengee utamaduni wa maadili mema na kwa kufanya hivyo nchi yetu itasonga mbele kimaendeleo na itaheshimika.

Taratibu, Sheria na Kanuni;

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Wakati huu tunapoendelea kukuza na kuimarisha uchumi wetu kwa kuboresha miundo mbinu na teknojia za kisasa, waajiri na wafanyabiashara toka sekta zote wanatakiwa kuheshimu na kufuata taratibu, kanuni na sheria zinazosimamia biashara kitaifa na kimataifa. Aliyewahi kuwa Mwanauchumi Mkuu na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia katika miaka ya 2009 – 2012 Bwana Kaushik Basu, aliwahi kusema na nanukuu:

“Uchumi wa kisasa hauwezi kujengwa bila taratibu na wakati huo huo, uchumi unaweza kuharibika kutokana na sheria mbovu na zenye usumbufu. Changamoto dhidi ya maendeleo ni namna ya kuvuka vikwazo hivi kwa kubaini taratibu nzuri na kuachana na zile zinazokinzana na ukuaji wa biashara ndogo na zile zenye ukubwa wa kati…” Mwisho wa kunukuu.

Ninaomba tutumie muda wetu vizuri kwa kushirikiana na Serikali na kuzingatia Kanuni, Sheria na Taratibu za kufanya kazi na biashara zetu kwa kasi na ufanisi zaidi.

Hitimisho:

Mheshimiwa Mwenyekiti,

Naomba nihitimishe hotuba yangu kwa kutoa tena shukrani za pekee kwa kukubali nijumuike nanyi kwenye tukio hili muhimu la kutafuta Mwajiri Bora wa Mwaka 2015. Nawapongeza kwa ubunifu wenu, maana ni kupitia ushindani kama huu tutaweza kujenga mazingira bora kibiashara na kuongeza ushindani nchini.

Napenda pia kuwashukuru tena baadhi ya wanachama wa ATE kwa kudhamini tukio hili maana bila wao tusingeweza kukutana muda huu. Hivyo nawapongeza sana kwa ukarimu wenu.

Natoa pongezi zangu za dhati kwa uongozi na timu nzima ya ATE waliofanikisha tukio hili, Mungu awabariki na awazidishie afya njema.

Ndugu Mwenyekiti, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,

Mwisho kabisa, pamoja na kutafuta mshindi wa tuzo ya leo nashauri tutumie muda huu kujenga mtandao wa kibiashara na tuhakikishe tunaendelea kufanya kazi pamoja tukizingatia msemo kuwa: “Umoja ni nguvu utengano ni udhaifu.”

Nawatakieni nyote afya njema katika kusherehekea hafla hii ya kutoa Tuzo ya Mwaajiri Bora wa mwaka 2015.

Asanteni sana kwa kunisikiliza!

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday81
mod_vvisit_counterYesterday106
mod_vvisit_counterThis week290
mod_vvisit_counterLast week798
mod_vvisit_counterThis month2447
mod_vvisit_counterLast month3555
mod_vvisit_counterAll days524632
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved