Logo
Thursday, 28 January 2016 00:00    PDF 

MAELEZO YA WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB) WAKATI WA KUHITIMISHA HOJA YA KUJADILI HOTUBA YA MHE. DKT. JOHN POMBE MAGUFULI, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 28 JANUARI 2016

 

UTANGULIZI

 

Mheshimiwa Spika,

· Awali ya yote, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Hotuba nzuri aliyoitoa wakati akizindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 20 Novemba 2016. Sina shaka kuwa majadiliano ya Hotuba hiyo hapa Bungeni yamedhihirisha umakini wa namna Waheshimiwa Wabunge walivyoielewa Hotuba ile na umakini uliotumika katika utayarishaji na uwasilishwaji wake.

· Nichukue nafasi hii kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika na Naibu Spika ambavyo mmesimamia mjadala huu. Aidha, na kwa kipekee kabisa kumpongeza Mwenyekiti Mtemi Andrew Chenge ambaye alipata fursa ya kusimamia mjadala wa Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais.


Mheshimiwa Spika,

· Nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia mjadala wa Hotuba hiyo ya Mheshimiwa Rais. Aidha, niwashukuru kwa kuunga mkono maeneo mbalimbali yaliyobainishwa katika Hotuba hiyo. Kitendo cha kuunga mkono kimeipa Serikali nguvu ya kutekeleza ushauri wa michango mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge.

· Napenda kuwadhihirishia kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge yote kwa ujumla wake itaisaidia Serikali kutekeleza kwa ufanisi zaidi Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015-2020. Aidha, itasaidia kutekeleza Mpango wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 na Dira ya Maendeleo 2025.

 

Mheshimiwa Spika,

· Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 171 wamechangia mjadala huu.

 

Mheshimiwa Spika,

· Katika kuhitimisha Hoja hii si nia yangu ya kujadili tena Hoja moja baada ya nyingine kama ilivyotolewa wakati Waheshimiwa Wabunge wakichangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, bali nitajielekeza katika ujumla wake. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri tayari wameshatoa maelezo ya maeneo muhimu ya kuzingatia.


KUHIMIZA UADILIFU NA UWAJIBIKAJI KWA WATUMISHI WA SERIKALI

Mheshimiwa Spika,

· Serikali ya Awamu ya Tano imeweka msisitizo katika kuhakikisha inarejesha nidhamu katika Utumishi wa Umma kwa kuweka mkazo katika misinngi ya uadilifu, uwajibikaji, kutoa huduma kwa wakati na kuchukua hatua haraka dhidi ya watumishi wote wanaokwenda kinyume na misingi ya utendaji kazi Serikalini.

· Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuzingatia falsafa ya “Hapa Kazi tu” ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli itaendelea kuhakikisha kuwa kila Mtendaji Serikalini anatimiza wajibu wake na pia kuhakikisha inachukua hatua dhidi ya wote wanaokiuka maadili ya kazi na Sheria.

· Napenda kusisitiza kuwa kila Mtumishi mahali popote alipo atimize wajibu wake ipasavyo.

· Tunataka kujenga Utumishi wa Umma wenye kuzingatia uadilifu, unaowajibika na Watumishi wanaofanya kazi kwa bidii na maarifa na kamwe hatutawahurumia Watumishi wazembe na wanaofanya kazi kwa mazoea.

MASUALA YANAYOHITAJI KUTENGEWA BAJETI

Mheshimiwa Spika,

  • Wakati wa mjadala wa Hotuba ya Mheshimiwa Rais zipo hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ambazo utekelezaji wake utahitaji kufanya maandalizi na kutenga Bajeti ya Serikali.
  • Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na ujenzi wa Miundombinu ya Barabara, Mawasiliano, Uchukuzi ikiwemo Bandari pamoja na Miundombinu ya usambazaji wa Maji na Nishati. Vilevile ipo Miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa Nchini katika Sekta za uzalishaji mali ikiwemo Kilimo, Mifugo Maliasili, Madini n.k. na Sekta za Huduma za Jamii kama vile Elimu, Afya, ambayo inahitaji kukamilishwa.
  • Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali itajitahidi kupanga vipaumbele vyake vya mpango na Bajeti kwa kuzingatia ahadi za Mheshimiwa Rais kuanzia mwaka huu wa fedha na kuendelea. Maoni na Hoja za Wabunge zitazingatiwa wakati wa utekelezaji. Kubwa ni kuomba ushirikiano wa Wananchi wote ili utekelezaji uwe wa ufanisi na tija.

KILIMO

· Katika Sekta ya Kilimo, Waheshimiwa Wabunge wameeleza changamoto nyingi zinazowakabili Wakulima ikiwemo Pembejeo kuchelewa kuwafikia Wakulima. Tatizo la ununuzi wa mazao hasa Tumbaku na Pamba, Kahawa na Huduma chini ya Stakabadhi ya Mazao Ghalani. Serikali imepokea ushauri wa Wabunge na utazingatiwa. Napenda kutumia fursa hii kuelezea kuwa kutokana na baadhi ya maeneo katika Nchi yetu kukumbwa na uhaba wa chakula uliotokana na aidha uzalishaji hafifu katika msimu uliopita, ama kutokana na mazao na vyakula kusombwa na mafuriko; Serikali imeendelea kutumia akiba yake ya chakula kuhakikisha waathirika wote wanapata chakula.

· Nachukua fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia kikamilifu ugawaji wa chakula hicho ili kiwafikie walengwa bila upendeleo, na bila kuchepusha na kukipeleka mahali pengine.

· Aidha, chakula hicho kigawanywe hadharani ili kuondoa malalamiko.

· Ili kuhakikisha walengwa wa chakula cha msaada wanafikiwa na kuhudumiwa. Viongozi Wakuu na Watendaji wa Serikali katika ngazi zote watoke maofisini kwenda Vijijini ili kuhakikisha chakula hicho kisitumike kwa matumizi mabaya kama utengenezaji wa pombe.

· Wakulima katika maeneo yaliyopata mafuriko wapatiwe mbegu za mazao yanayokomaa haraka.

· Kuhusu usambazaji wa Pembejeo Halmashauri zote zihakikishe kuwa Pembejeo zinafika mapema katika maeneo yanayotarajia kupata mvua za masika, na zipelekwe kwa walengwa.

· Serikali itaendelea kuangalia mfumo bora wa kusambaza pembejeo za ruzuku ili kuondoa malalamiko ya wakulima.

· Halmashauri na Wizara ya Kilimo wakae kuondoa tozo na ushuru zenye kero kwa mazao.

 

MAJI

 

Mheshimiwa Spika,

  • Suala la maji ni changamoto ya nchi nzima, ili kuboresha Huduma ya Maji, Serikali itajitahidi kutumia mbinu zote zikiwepo kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua ili yatumike wakati wa kiangazi. Aidha, Serikali imepanga kuhakikisha kuwa fedha kwa ajili ya Miradi ya Maji ambayo haijakamilika zinapatikana na kutumwa kwa wakati katika maeneo husika.
  • Vilevile Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa Wakandarasi wanaopewa kazi za kujenga Miradi ya Maji wana uwezo wa kutosha ili iwe na ubora unaotakiwa; na itaendelea kulipa madeni ya Wakandarasi na Wataalam Washauri.

VITA DHIDI YA UJANGILI WA WANYAMAPORI

· Matatizo yanayoikabili Sekta ya Maliasili na Utalii yakiwepo ujangili wa wanyamapori na nyara, migogoro ya mipaka kati ya Vijiji na Hifadhi na upotevu wa mapato yatashughulikiwa kwa wakati ili kuifanya Sekta hii muhimu kuchangia katika uchumi wa Taifa na kuhifadhi rasilimali hii kwa ajili ya kizazi kijacho.

· Ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge utazingatiwa na Wadau wote ili kuhakikisha wanyamapori hususan Tembo na Faru hawaendelei kuuwawa na majangili.

 

SEKTA YA UVUVI

 

Mheshimiwa Spika,

· Masuala ya uvuvi yataimarishwa kwa kuwatafutia wananchi na wadau wa Sekta ya Uvuvi Nchini kwa kuhakikisha wanapatiwa vifaa vya vya kisasa vya uvuvi, kuwatafutia masoko na kuongeza kasi ya uwekezaji katika viwanda vya mazao ya samaki hususan katika Ukanda wa Bahari Kuu.

· Ili kufanya uvuvi katika maeneo ya Bahari, Maziwa na Mito unakuwa endelevu usimamizi na doria utafanyika kwa nguvu kubwa ili kukabiliana na uvuvi haramu.

 

UFUGAJI WA NYUKI

 

Mheshimiwa Spika,

· Serikali itaendelea kuhimiza wananchi kuanzisha ufugaji wa nyuki kwa kutumia mizinga ya kisasa. Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya Nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata mizinga ya kisasa kwa bei nafuu.

 

VIWANDA VYA KUSINDIKA MAZAO YA KILIMO

· Ni lazima tuziangalie Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mtizamo wa kibiashara na viwanda kwa lengo la kuwa na viwanda vya kisasa vya kuongeza thamani ya mazao yake.

· Mkazo utakuwa katika kuanzisha viwanda ambavyo sehemu kubwa ya malighafi yake itatoka ndani hususan kwenye Sekta za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Madini na Maliasili nyingine.

 

MIGOGORO YA ARDHI NCHINI

· Kumekuwepo na malalamiko katika maeneo mengi Nchini yanayohusu matumzi ya ardhi. Maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa ni kati ya wakulima na wafugaji, wananchi kuhodhi maeneo bila ya kuyaendeleza, mipango miji na ujenzi katika maeneo ya wazi. Serikali imepokea michango mbalimbali ya Wabunge ya namna bora ya kuimaliza migogoro hiyo.

· Wizara zinazohusika zitashirikiana na wadau wa Sekta ya ardhi nchini ili kubaini vyanzo vya migogoro hiyo na kuipatia ufumbuzi. Napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuona migogoro hii inakwisha. Wito wangu ni kwa watumiaji wote Nchini kuheshimu na kufuata sheria.

 

HITIMISHO

 

Mheshimiwa Spika,

· Nimeona nielezee haya kwa kifupi kama njia ya kuwaombeni sana Waheshimiwa Wabunge wote na wale wenzangu wa Upinzani ambao kwa hulka yao waliamua kufanya walivyofanya. Lengo letu sote ni kujenga Nchi yetu na kuleta maendeleo ya Nchi yetu.

· Tunalo jukumu la kufanya kama wadau ikiwemo Serikali, sisi kama Wabunge na Wananchi wetu. Jukumu letu ni kuwaongoza Wananchi kutekeleza yote yaliyomo katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais.

· Ninawaomba sana Wabunge wenzangu wa Vyama vyote vya Siasa na Wananchi wote kutambua wajibu wetu na kwa umoja wetu kujenga Nchi yetu. Hakuna sababu na wala si busara kubeza juhudu za kila mmoja wetu ambazo zinasaidia kujenga Nchi yetu. Nawaomba tuungane katika juhudi za kuwaletea Wananchi maendeleo.

· Michango yenu na mawazo yenu ndani na nje ya Bunge ndiyo kielelezo chetu kama Wabunge mbele ya Watanzania waliotupatia dhamana ya kuwaongoza kwamba tunatekeleza wajibu wetu.

· Tunayoyafanya hapa Bungeni kiwe kinalenga maslahi ya Taifa. Hivyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge hasa wenzetu wa Kambi ya Upinzani kwamba, tuna jukumu la kufanya ambalo ni deni la Wapiga Kura wetu waliotuchagua. Tujitahidi kuondoa tofauti zetu kwa maslahi ya Watanzania. Aidha, sisi wote ni Watanzania hivyo hatuna budi kufanya juhudi za dhati za kupendana, kushirikiana na kusaidiana kwa maslahi ya Watanzania wote.

 

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, baada ya kusema haya, ninakushukuru tena Mheshimiwa Spika kwa kunipa nafasi hii, naomba kutoa Hoja.

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday46
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week516
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2634
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days517426
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved