Logo
Sunday, 31 January 2016 00:00    PDF 

HOTUBA YA MHE. KASSIM MAJALIWA MAJALIWA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE SHEREHE ZA KUWEKWA WAKFU NA KUINGIZWA KAZINI MCHUNGAJI DKT. FREDRICK ONAEL SHOO KUWA ASKOFU MKUU WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA (KKKT) MOSHI TAREHE 31 JANUARI 2016

 

 

Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Mkuu Mpya wa KKKT;

Dkt. Alex Malasusa, Askofu Mkuu (Mstaafu) wa KKKT na ambaye pia anamaliza muda wake;

Mheshimiwa Amos Makala Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro;

Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu na wenza wenu;

Waheshimiwa Wabunge wenzangu mlioko hapa;

Maaskofu mlioko hapa;

Bwana Brighton Killewa, Katibu Mkuu wa KKKT;

Viongozi na Wawakilishi wa Madhehebu mbalimbali ya Dini;

Wageni Waalikwa;

Mabibi na Mabwana.

BWANA YESU ASIFIWE!

 

Napenda kuungana nanyi kumshukuru Mwenyezi Mungu kutuwezesha kujumuika sote pamoja mahali hapa asubuhi ya leo katika sherehe za Kuwekwa Wakfu na Kuwekwa Kazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Niwashukuru kwa dhati Viongozi wa Kanisa na Kamati ya Maandalizi kwa kunikubali nishiriki nanyi siku ya leo. Ninatambua kuwa mwaliko huu ulikuwa ni wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kutokana na majukumu mengine ya Kitaifa imempendeza nimuwakilishe kwenye sherehe hizi leo. Mheshimiwa Rais anawapa salaam za kheri katika shughuli hii muhimu.

Kipekee napenda kumpongeza Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo kwa kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania hili. Nimeambiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 19 uliofanyika Chuo Kikuu cha Makumira Agosti, 2015 walikuchagua kwa haki na kura nyingi kuwa Askofu Mkuu wa Tano wa Kanisa hili. Hii ni ishara ya imani kubwa waliyo nayo kwako waumini katika Kanisa hili. Ninakupongeza kwa dhati kwa ushindi huu mkubwa!

Aidha, kwa kutumia nafasi hii pia napenda kukupongeza Dkt. Alex Malasusa, Askofu Mkuu (Mstaafu) kwa kazi nzuri uliyoifanya katika kipindi chako. Tunakushukuru kwa kulifikisha Kanisa hili hapa tulipo. Mafanikio uliyoyaleta tumeyaona. Tunasema asante kwa kazi nzuri iliyotukuka ambayo umeifanya. Umewaongoza Kondoo wa Bwana vizuri. Unastahili kupumzika na kuwasaidia Viongozi wanaokupokea kwa kuwapa ushauri bila kusita kwani uzoefu ulio nao ni HAZINA kubwa kwa Kanisa hili.

JUKUMU LA KUONGOZA KANISA

Baba Askofu na Wageni Waalikwa,

Asubuhi ya leo tunakutana hapa kushuhudia kuwekwa Wakfu kwa Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo kuwa Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilitheri Tanzania (KKKT). Jukumu la kuongoza Kanisa hili ni kubwa linalohusisha huduma za kiroho, kijamii na kiuchumi katika Nchi yetu. Aidha, jukumu kubwa ni kuhakikisha kuwa Waumini (ambao kwa takwimu za mwaka 2014 wamefikia Milioni 6.5) wanakua kiimani na wanapatiwa huduma za kiroho na kimwili. Lazima Kanisa lihakikishe kuwa linatekeleza majukumu haya kwa misingi, kanuni na taratibu iliyojiwekea.

KAZI ZA ASKOFU

Baba Askofu,

Ninakiri kwamba, mimi sio Mtaalam wa Biblia na hasa ninapokuwa mbele ya umati wa Waumini, Walei, Wachungaji na Maaskofu. Lakini ninakumbuka maandiko muhimu katika Biblia kuhusu majukumu na kazi za Askofu ambayo mengi mnajua na yamekwishasemwa hapa.

Kipekee nimeguswa na Majukumu yaliyoorodheshwa katika Waraka wa Kwanza wa Timotheo, Sura ya Tatu, mstari wa kwanza hadi wa Saba (1 Timotheo 3:1-7) ambapo kutokana na muda sitayasoma. Lakini kwa wale walio na Biblia watayasoma kwa wakati wao.

Katika Waraka huu, Mtume Paulo ameeleza mengi kuhusu sifa za Maaskofu. Baba Askofu Dkt. Fredirick Onael Shoo tayari anazo sifa hizo na ndiyo maana amewekwa Wakfu na kuingizwa kazini leo. Tunaamini kuchaguliwa kwake ni kazi njema yenye mkono wa Mungu, ili kumuwezesha kufanya kazi ya Bwana. Napenda nikutie moyo kwamba yote utayaweza. Siku zote kumbuka lile fungu maarufu katika Biblia la Wafilipi Sura ya Nne Mstari wa Kumi na Tatu (Wafilipi 4:13) linalosema: “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”. Nina hakika kwa imani utashinda!

USHIRIKIANO KATI YA SERIKALI NA MADHEHEBU YA DINI

Baba Askofu na Wageni Waalikwa,

Siku zote kumekuwepo na ushirikiano mkubwa kati ya Serikali na Asasi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Madhehebu ya Dini katika kazi za kuwahudumia Wananchi na jamii yetu. Madhehebu ya Dini yamesaidia kuleta maendeleo ya Taifa letu, hususan katika huduma za elimu, afya, maji, utunzaji wa mazingira, pamoja na huduma zingine za jamii.

Serikali inatambua na kuthamini sana mchango na jitihada za KKKT hapa nchini taarifa zinaonyesha kwamba Kanisa hili lenye Dayosisi takriban 24 lina chuo kikuu kimoja cha Tumaini kilichopo Makumira chenye matawi sita (6). Kuna Seminari pale Morogoro na shule za huduma ya wenye ulemavu wa kusikia tatu (3). Lakini Kanisa pia lina Hospitali 23 ikiwemo ya KCMC, vituo vya afya na zahanati zaidi ya 140 nchini. Aidha, Kanisa lina miradi mingi ya maji inayotekelezwa nchini kote.

Kwa hakika huu ni mfano wa kuigwa katika kutekeleza dhana nzima ya Kanisa kuwasaidia Wananchi kijamii na kiuchumi. Naliomba Kanisa chini ya viongozi wako liendeleze kazi hii ya kutoa huduma nchini kwa jamii. Maendeleo ya nchi yetu yanatutegemea sote. Tukishirikiana, hakika tutaweza kuyaendeleza mambo haya yote mazuri.

CHANGAMOTO ZILIZOPO

Baba Askofu,

Unapewa uongozi wakati kuna changamoto kubwa zinazokabili Nchi yetu hasa katika nyanja za elimu, afya, maji, watoto yatima, watoto wenye ulemavu na suala zima la janga la UKIMWI. Changamoto hizi zinatupa vigezo vya kupima juhudi na uwezo wetu kama Viongozi wa Serikali na Viongozi wa Dini katika kuhudumia jamii.

Nirudie kushukuru Madhehebu ya Dini kwa kutoa mchango mkubwa katika kuisaidia jamii. Kwa mfano kwa upande wa elimu, imejitokeza wazi kwamba Shule zinazomilikiwa na Madhahebu ya Dini zinafanya vizuri zaidi kwa kufaulisha Wanafunzi kwa kiwango cha juu kitaaluma.

Huu ni uthibitisho kwamba madhehebu ya dini yako mstari wa mbele katika kuwapatia Watanzania maisha bora. Ubora wa elimu inayotolewa na shule za madhehebu ya dini ni changamoto kubwa sio tu kwa Serikali bali hata na sekta binafsi nyingine zinazoshughulika na elimu. Jukumu letu kama Serikalini ni kujifunza kutoka shule hizi ili tuweze kuboresha utoaji wa elimu katika shule nyingi za Serikali.

Baba Askofu Dk. Shoo ametoa rai kwamba kama Serikali inataka kuondoa ada elekezi haina budi kuziimarisha shule zake ili ziwe kama zilivyokuwa zamani. Napenda nitumie fursa kumhakikishaia kwamba suala la ada elekezi linaendelea kufanyiwa kazi na Serikali na likifika hatua nzuri litahusisha wadau wote ili tuweze kupata maoni yao.

Wito wangu kwa Madhehebu yote ya Dini yanayotoa elimu ni kuangalia uwezekano wa kutoa elimu bora kwa gharama nafuu zitakazowawezesha watoto wengi zaidi kumudu kusoma katika shule hizi. Ninaelewa tatizo la gharama za uendeshaji zilivyo juu, lakini ni vyema kwa imani na upendo kuwawezesha watoto wa ngazi zote wapate elimu bora.

AFYA

Baba Askofu,

Katika suala la afya, bado tunalo tatizo kubwa la ukosefu wa Huduma za Afya kwa Wananchi wetu. Pamoja na juhudi kubwa ambazo Serikali, Dini na Wadau wengine tumeweka katika Sekta hii bado huduma zinapatikana kwa shida. Aidha, katika sehemu nyingine za Nchi lipo tatizo la umbali ambalo sio kila mwananchi anaweza kufikia huduma hizi. Vilevile, gharama za huduma ni kubwa jambo ambalo inakuwa vigumu kwa mwananchi wa kawaida kupata huduma hizo.

Aidha, Serikali kwa upande wake imejiwekea malengo ya kujenga Zahanati katika kila Kijiji na Kituo cha Afya katika kila Kata. Serikali inatambua juhudi za Madhehebu ya Dini katika kuanzisha Zahanati, Vituo vya Afya na hata Hospitali.

Napenda kutumia nafasi hii kuyashukuru Madhehebu yote ya Dini ambayo yamekuwa mstari wa mbele kuisaidia Serikali kufikisha huduma hizi za Afya karibu zaidi na wananchi. Wito wangu kwa hili ni kujitahidi kutoa huduma hizi kwa gharama nafuu ili Wananchi wengi wapate kuzitumia. Napenda kusisitiza kuwa milango yetu Serikalini iko wazi kwa KKKT.

WATOTO YATIMA NA UKIMWI

Baba Askofu,

Changamoto nyingine kubwa ni za watoto yatima na janga la UKIMWI. Ninatambua Kanisa hili linatoa huduma ya ushauri nasaha katika Vituo vilivyoainishwa. Ni dhahiri kwamba maeneo yote haya yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na Madhehebu ya Dini ili kupunguza idadi ya vifo na watoto Yatima.

Aidha, tunalo tatizo vilevile kwa upande wa watoto wenye ulemavu. Niwashukuru kwa kutambua umuhimu wa kuwasaidia Watu wenye Ulemavu. Tayari mnavyo vituo vya wale wenye Ulemavu wa kusikia. Watoto wote hawa wanahitaji kupata huduma zote muhimu zikiwemo, elimu na huduma za afya.

Kama Kanisa hizi ni changamoto ambazo mnahitaji kuzipa kipaumbele katika kuzikabili. Mnapopanga mipango ya Kanisa mfikirie mtawasaidiaje watoto hawa. Mnapotoa matoleo na sadaka mawazo ya Waumini wote yawe katika kufikiria namna ya kutoa huduma kwa jamii hii. Msaada kwao ni ishara ya kwamba sisi tulio wazima na wenye nafasi na afya tunawajali.

Baba Askofu na Wageni Waalikwa,

Takriban miaka 44 iliyopita, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akihutubia Watawa wa Kanisa Katoliki la Maryknoll kule Marekani alisema, nanukuu:

“Katika sehemu nyingi duniani hasa Afrika, Kanisa ……. limejenga shule zake na hospitali zake. Hizo zimekuwa na manufaa makubwa sana. Shule zimetoa elimu na hospitali zimetoa matibabu ambayo yasingepatikana kama zisingekuwepo.... ”. . Mwisho wa kunukuu.

Napenda kusisitiza wito wa Baba wa Taifa wa kushirikiana na washirika wa Kanisa, Serikali na Wananchi wote kwa ujumla kuendelea kushirikiana kuleta maendeleo ya Nchi yetu kwa kujenga shule zaidi na hospitali zaidi.

WAJIBU WA VIONGOZI WA DINI NA MATARAJIO YA WANANCHI

Baba Askofu,

Viongozi wa Dini kazi yao kubwa ni kuunganisha jamii pamoja na wala siyo kuwatenganisha. Kwa maana hiyo, sote tunao wajibu wa kushirikiana kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazotukabili katika Nchi yetu.

Kama Waumini tunao wajibu wa kumsaidia Baba Askofu kukabiliana na changamoto hizo. Tunachotakiwa ni kumuomba Mwenyezi Mungu atuwezeshe kuwaelewa Viongozi wetu na maelekezo yanayotolewa. Tuzingatie mafundisho mbalimbali ambayo yanatolewa ili kutujenga kiroho na kiimani tukijenga imani zetu, upendo utatawala katika jamii nzima na matatizo mengi yanayohusu mmomonyoko wa maadili yatapungua.

Baba Askofu na Wageni Waalikwa,

Nimeongea mambo ambayo sio mageni kwenu. Nimalizie kwa kuwashukuru tena kwa kunijumuisha niwe pamoja nanyi siku ya leo. Nimpongeze tena Mchungaji Dkt. Dkt. Fredrick Onaeli Shoo kwa kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT). Tunajua anayo kazi kubwa ya kulinda na kukuza Waumini kiroho. Tumpe ushirikiano wetu sote.

Aidha, wote kwa pamoja tunalo jukumu la kushirikiana kwa pamoja kujenga Nchi yetu. Tudumishe ushirikiano huu, tuongeze bidii katika kazi kwa ajili ya maendeleo ya Nchi yetu. Kila mmoja wetu awe mhamasishaji mkuu katika kuhakikisha kila mtu anafanya kazi.

Tukifanya hivyo tutakuwa tumeunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais na kaulimbiu yake ya “Hapa Kazi Tu”. Kila mmoja atambue kwamba tukifanya kazi kwa bidii ndiyo tutapa maendeleo.

Aidha, ninawasihi tuendelee kushirikiana kuwekeza katika maeneo ya huduma za jamii zikiwemo shule, vyuo, zahanati, n.k. Serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu yote katika kuwahudumia Watanzania.

Hitimisho:

Nimalizie kwa kurudia niliyoyasema pale mwanzo kwamba Serikali inatambua umuhimu wa Viongozi wa Dini katika kuijenga jamii yenye umoja na yenye utamaduni wa kupendana. Tuepuke kuotesha mbegu mbaya ya Udini, Ubaguzi na Ukabila. Tujenge Umoja na Mshikamano kwa manufaa ya Wananchi wetu na Taifa letu.

Baba Askofu,

Mwisho, napenda kurudia tena kuwashukuru kwa kujumuika sote na kunipatia nafasi hii siku ya leo. Nimtakie tena Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo na Familia yake maisha mema na kazi njema kwa majukumu aliyonayo mbele yake. Tunakuombea Baraka tele za Mwenyezi Mungu na Mungu akuongoze katika jukumu hili jipya.

Nimuombee pia maisha yenye amani na furaha Dkt. Alex Malasusa Askofu Mkuu Mstaafu na familia yake waendelee kushirikiana na uongozi mpya katika kuliongoza Kanisa hili. Tuendelee kuombea viongozi wetu waweze kuiongoza nchi hii kwa amani na hofu ya Mungu. Mwenyezi Mungu atubariki sote tunapohitimisha shughuli ya leo.

Baada ya kusema hayo, nasema asanteni sana kwa kunisikiliza na Mungu awabariki nyote.

 

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday46
mod_vvisit_counterYesterday124
mod_vvisit_counterThis week516
mod_vvisit_counterLast week867
mod_vvisit_counterThis month2634
mod_vvisit_counterLast month3157
mod_vvisit_counterAll days517426
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved