Logo
Friday, 01 July 2016 12:05    PDF 

UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, naomba kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa rehema kwa kutupatia afya njema ya kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge lako Tukufu tuliouanza tarehe 19 Aprili, 2016, takriban siku 73 zilizopita. Mkutano huu ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kujadili na kupitisha Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2016/2017. Kazi hiyo tumeifanya kwa tija na ufanisi wa hali ya juu kabisa.


2. Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba nitumie fursa hii ya awali kabisa kumpongeza Mheshimiwa Spika, Mheshimwa Naibu Spika, Waheshimwa Wenyeviti na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali ya Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Wizara, Mikoa na Taasisi za Serikali. Aidha, nawapongeza pia kwa kuupitisha Mpango wa Pili wa Taifa wa Miaka Miwili wa Maendeleo. Napenda kukiri kwamba mijadala ya mkutano huu ilikuwa yenye msisimko na wakati mwingine iliambatana na hisia kali kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Ninaamini hisia za Waheshimiwa Wabunge waliochangia zilikuwa na hoja ambazo zililenga kujenga na kuiletea maendeleo nchi yetu. Ahsanteni sana!


3. Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Wabunge kwa ushauri mzuri kwa Serikali ambao tutaufanyia kazi. Aidha, michango yenu Waheshimiwa Wabunge ni chachu katika kuongeza kasi ya kuwawezesha wananchi kupata maendeleo ya haraka, hasa wakati huu tunapoanza utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika Serikali ya Awamu ya Tano. Tunawashukuru sana kwa michango yenu!


4. Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha kwa mwaka 2016/2017 ni ya kihistoria kwa sababu kwa mara ya kwanza tangu tupate Uhuru wetu mwaka 1961 tumeweza kutenga asilimia 40 ya Bajeti ya Shilingi Trilioni 29.5 kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Changamoto kubwa na ya jumla tuliyonayo ni jinsi ya kupanua wigo wa kukusanya kodi, kudhibiti matumizi ya fedha za umma ikiwa ni pamoja na kutumia kwa ufanisi fedha zinazokusanywa. Azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Shilingi ya Serikali inayokusanywa kupitia kodi za wananchi, mikopo na michango ya Wahisani inatumika katika shughuli iliyokusudiwa na lazima thamani ya fedha “Value for Money” ionekane bayana katika utekelezaji wa vipaumbele tulivyojiwekea. Vipaumbele vyetu tulivyokubaliana katika mpango wa mwaka huu ni pamoja na kutenga fedha nyingi zaidi katika sekta za elimu, afya, maji, kilimo, viwanda, miundombinu, uchukuzi, bandari, usafiri wa anga na majini, maliasili, nishati na madini.


SHUGHULI ZA BUNGE


5. Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitimisha mkutano huu tukiwa tumepata fursa ya kujadili Miswada, Maazimio na Kauli mbalimbali za Mawaziri. Miswada iliyowasilishwa na Serikali ni saba ambapo miswada minne ilisomwa kwa mara ya kwanza na ifuatayo kupitishwa:

(i) Muswada wa Sheria ya Fedha za Matumizi ya Serikali wa Mwaka 2016 (The Appropriation Bill, 2016).

(ii) Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2016 (The Finance Bill, 2016), na

(iii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2016 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2016].


6. Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 469 ya msingi na mengine 1,365 ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kujibiwa na Serikali. Vilevile, jumla ya Maswali 33 ya Msingi na 19 ya nyongeza ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu ya kila Alhamisi yaliulizwa na kupata majibu. Aidha, Waheshimiwa Wabunge waliridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa za Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni.


7. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa jumla napenda kutoa taarifa katika Bunge lako Tukufu kuwa shughuli zote zilizopangwa katika Bunge la Tatu zimekamilishwa kwa ufanisi mkubwa. Niwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri, Waheshimiwa Wabunge na Wataalam wetu kwa michango yao mizuri iliyofanikisha shughuli za Bunge letu. Nawapongeza sana!


8. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio hayo mazuri, kama kawaida ya Mabunge mengi ya kidemokrasia Duniani, hakuku-kosekana purukushani za hapa na pale. Katika Mkutano huu wa Bunge kumekuwa na taswira potofu waliyojaribu kuijenga lakini bila mafanikio baadhi ya wanasiasa, wakiwemo Wabunge wa Kambi ya Upinzani, kwa wananchi wetu na jumuiya ya kimataifa na kama vile kuna kuminywa kwa demokrasia ndani ya Bunge letu. Kwa bahati nzuri wananchi wetu na wadau wa maendeleo wamebaini kuwa upinzani katika Taifa letu bado haujakomaa kisiasa kwa sababu si jambo la kawaida kwa Mbunge kuzitoa Hoja za Bungeni na kuzipeleka mitaani eti zijadiliwe na wananchi na kisha zitolewe uamuzi. Iwapo hilo linawezekana basi kusingekuwa na umuhimu wa kuwa na Bunge.


9. Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na sintofahamu iliyojitokeza kwa baadhi yetu kuhusu nafasi ya Bunge katika kutunga sheria na kuisimamia Serikali, napenda nitoe ufafanuzi ufuatao kwa muhtasari. Kwanza, Ibara ya 100 na 101 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imetoa haki na kinga kwa Waheshimiwa Wabunge ili waweze kujadili na kuhoji utendaji wa Serikali kwa uhuru bila mashaka yoyote ya kuweza kushitakiwa wanapotimiza wajibu wao huo wakiwa Bungeni. Kinga ya aina hiyo haijatolewa kwa mwananchi yeyote yule nchini, na kwa maneno mengine Mbunge hajafungwa mdomo labda aamue kujifunga mdomo mwenyewe.

Kwa mantiki hiyo, kitendo cha baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kususia vikao vya Bunge hakitoi picha nzuri kwa wananchi waliotuchagua kuwasilisha matatizo yao katika Bunge hili. Hivyo, natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge hao kutafakari upya uamuzi wao na niwasihi kwa busara zao waingie Bungeni ili kwa pamoja na kwa ushirikiano tuweze kutoa ushauri kwa Serikali ambao utaliletea Taifa letu maendeleo. Pili, Bunge letu linaongozwa na Katiba, Sheria na Kanuni za Kudumu za Bunge. Hivyo ni vyema tukazifuata ili kuondoa manung’uniko yasiyo ya lazima. Endapo kuna utata katika jambo lolote ndani ya Bunge letu, zipo taratibu tulizojiwekea na kanuni za kufuata ili kupata ufumbuzi wa jambo hilo. Kususa kuingia Bungeni kunaweza kusiwe na tija kwa tunaowawakilisha na Taifa letu.


MPANGO WA PILI WA MAENDELEO WA TAIFA

10. Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kwamba kabla ya kuanza kwa mjadala wa Bajeti ya mwaka 2016/2017, tulipata fursa ya kujadili na kuidhinisha Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021. Katika Mpango huo yameainishwa maeneo makuu manne ya kipaumbele yafuatayo:-

Eneo la Kwanza ni:          Kukuza na kujenga msingi wa uchumi wa viwanda. Eneo hili litahusisha kuongeza uzalishaji na tija katika sekta zinazoweza kuchochea na kuharakisha maendeleo ya viwanda ambazo ni pamoja na sekta ya kilimo kinayojumuisha kilimo cha mazao, mifugo, uvuvi na misitu, sekta ya madini na utalii.

Eneo la Pili ni: Kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu. Eneo hili litahusisha kupanua fursa za upatikanaji wa elimu bora kwa wote; kuimarisha huduma za afya; upatikanaji wa maji safi na salama, kuboresha mazingira ya kuishi na hifadhi ya jamii.

Eneo la Tatu ni: Kujenga mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara na uwekezaji. Katika eneo hili, Serikali itaimarisha mifumo ya kisheria ili iwe rafiki na iweze kuvutia wawekezaji wa ndani na nje; kuimarisha miundombinu na huduma za msingi wezeshi katika uendelezaji viwanda nchini, hususan upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika na bei ya chini, upatikanaji wa maji, na miundombinu ya uchukuzi, usafirishaji na mawasiliano kama reli, barabara, bandari, usafiri wa anga, usafiri wa majini na TEHAMA.

Eneo la Nne ni: Kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya mpango. Lengo la hatua hii ni kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa Mpango huo.


11. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kushirikiana na Serikali na kila mmoja wetu kuwajibika katika nafasi yake wakati wa kuutekeleza Mpango huo ili tufikie malengo hayo tuliyojiwekea.


UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI 2016/2017

12. Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika utangulizi wa hotuba yangu, Mpango huo umeweka mkazo wa kipekee katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hivyo, katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kutekeleza Mpango na Bajeti ya Serikali ambayo imeainishwa kwa kina na kwa ufasaha mkubwa na Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya sekta zao kwa mwaka 2016/2017. Aidha, Waziri wa Fedha na Mipango, wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali na pia alipohitimisha hoja yake, alitoa maelezo ya ufafanuzi wa kina wa hatua za kibajeti na kisera zitakazotekelezwa na Serikali katika mwaka ujao wa fedha. Naomba mimi pia niungane na Waheshimiwa Mawaziri ambao wamefanya kazi nzuri sana katika Bunge hili la Bajeti kwa kuweka msisitizo katika maeneo yafuatayo: Eneo la kwanza ni kuhusu kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na umuhimu wa kila mwananchi kulipa kodi na Eneo la pili ni kudhibiti matumizi ya fedha za umma. Naomba kuyaelezea kwa muhtasari maeneo haya mawili niliyoyaainisha kama ifuatavyo:


UMUHIMU WA KULIPA KODI


13. Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya mambo ambayo yamechukua uzito mkubwa katika majadiliano ya Bunge hili, ni mahitaji makubwa ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za Serikali, ikilinganishwa na kiasi cha fedha kinachoweza kupatikana kwa njia ya kodi. Kama mlivyoona katika majadiliano Bungeni, wakati wote mahitaji yalizidi kiasi cha fedha kinachoweza kukusanywa kwa njia ya kodi na hivyo kutulazimu kuwa na vipaumbele vichache vinavyoweza kuleta msukumo mkubwa katika kukuza uchumi na kuwaletea maendeleo wananchi walio wengi. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwamba, Serikali itaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi kwa kuchukua hatua zifuatazo:-

Kwanza: Kuboresha mazingira ya uendeshaji wa biashara na uwekezaji ikiwa ni pamoja na kuweka mifumo ya kurahisisha usajili wa makampuni na utoaji wa leseni na urasimishaji wa shughuli zisizo rasmi za wafanyabiashara wadogo ili kupanua wigo wa mapato;

Pili: Kuimarisha usimamizi wa matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki katika maeneo yote ya Mamlaka ya Bandari Tanzania; vituo vyote vya Mamlaka ya Mapato Tanzania; na katika taasisi mbalimbali zinazokusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ikiwemo Serikali za Mitaa na Halmashauri zote;

Tatu: Kuanzisha kikosi maalum cha kufuatilia kwa karibu matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs) za kutoa risiti kila mfanyabiashara anapouza bidhaa au huduma; hivyo basi kila mwananchi unaponunua bidha yoyote dai risiti.

Nne: Kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) wanashirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (eGovernment) kutekeleza mfumo wa kuwa na dirisha moja, yaani Electronic Single Window System na pia kudhibiti mizigo yote inayoingia na kutoka katika Bandari Kavu (ICDs) pamoja na kudhibiti kikamilifu taarifa zinazoandaliwa na Bandari Kavu ili kuzuia ukwepaji kodi;

Tano: Kuziwezesha Halmashauri katika kujenga uwezo wa kusimamia ukusanyaji mapato kwa kuboresha mikataba ya Wakala wanaokusanya mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa;

Sita: Kuwajengea uwezo watumishi wanaohusika na ukusanyaji wa mapato na wale wanaohusika na uchunguzi na ukaguzi wa ndani wa taasisi zinazokusanya mapato. Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi wa uadilifu na maadili ya maofisa wote wanaohusika na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.


14. Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali itaendelea kuzingatia maoni na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge wa kuendelea kubuni vyanzo vipya vya mapato na kupanua wigo wa kodi. Tunaomba ushirikiano wa dhati wa wadau wote wa maendeleo ya nchi yetu, wakiwemo wafanyabiashara wakubwa na wawekezaji, wajasiriamali mbalimbali, wafanyabiashara Wadogo na Wananchi wote kwa jumla.


KUDHIBITI MATUMIZI YA SERIKALI


15. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa udhibiti wa matumizi ya Serikali, sote ni mashahidi kwamba Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeanza kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali na kuepuka matumizi yasisiyo ya lazima. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itachukua hatua zaidi za kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji wa Bajeti ya Serikali pamoja na matumizi ya fedha za umma. Hatua hizo ni kama ifuatavyo :-

Moja: Kutafanya mapitio ya majukumu ya Wizara na Taasisi za Umma ili kuwianisha majukumu vyombo vya Serikali na hivyo kupunguza gharama za uendeshaji;

Mbili: Wizara, Mikoa na Taasisi zote za Serikali kufanya uhakiki wa watumishi wa umma mara kwa mara kwa lengo la kudhibiti ulipaji wa mishahara na malipo mengine kwa watu wasiostahili; na

Tatu: Viongozi na watendaji wote wa Serikalini kuhakikisha wanaimarisha na kudhibiti matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia ukomo wa Bajeti ya Fungu husika lilivyoidhinishwa na Bunge. Aidha, Viongozi wa Bodi na Menejimenti za Mashirika ya Umma na Taasisi za Umma kuhakikisha kwamba zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za kuanzishwa kwake. Msajili wa Hazina na Bodi za Wakurugenzi za Mashirika na taasisi za umma kusimamia kikamilifu matumizi ya Taasisi na Mashirika ya Umma hayo yaendane na majukumu ya msingi ya Taasisi hizo na yenye tija.


16. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia hatua hizo nilizoziainisha, naomba kupitia Bunge lako hili Tukufu kuwaagiza Watendaji Wakuu wa Wizara, Wakala, Idara Zinazojitegemea, Mashirika na Taasisi za Umma, Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa wanasimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na kuwepo kwa udhibiti wa kutosha wa matumizi ya fedha za Serikali. Hatua hii itawezesha kufikia malengo tuliyojiwekea katika sekta mbalimbali.


17. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, ni dhahiri kwamba mamlaka hizi zina wajibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya Serikali pamoja na michango ya wananchi. Hata hivyo, uzoefu unaonesha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zina tatizo la kukaa na fedha kwa muda mrefu kabla ya kuzielekeza kwenye matumizi yaliyokusudiwa. Kuchelewesha kutoa fedha zilizotengwa kwa shughuli zilizopangwa ni kuchelewesha kufikisha huduma muhimu kwa wananchi. Napenda kuhimiza uzingatiaji wa utaratibu wa kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mapato na matumizi ya fedha za Serikali katika ngazi zote ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika sekta ya umma.


UKUSANYAJI MAPATO KATIKA SERIKALI ZA MITAA


18. Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Sura 290, inazipa uwezo Mamlaka za Serikali za Serikali za Mitaa kutoza na kukusanya kodi, ushuru na ada mbalimbali kama vyanzo vya Mapato vya Mamlaka za Serikali za Mitaa. Sheria hiyo pia inazipa Mamlaka hizo kuteua mawakala wa kukusanya Mapato hayo kwa niaba ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu. Hatua ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia Mawakala ni miongoni mwa mikakati ya kuboresha ukusanyaji mapato na pia kutoa muda mwingi zaidi kwa Watumishi wa Mamlaka kushughulika na majukumu ya msingi ya Halmashauri na hasa utoaji wa huduma kwa wananchi na usimamizi wa miradi ya maendeleo. Pamoja na dhamira nzuri ya hatua hizo, Serikali imebaini changamoto za kiufundi katika kufanya tathmini ya vyanzo vya mapato; ugumu katika kupata mawakala wenye weledi katika ukusanyaji mapato na kubuni vyanzo vipya vya mapato, na wakati mwingine watumishi wenyewe kujipa uwakala kinyume na taratibu zinazomzuia mtumishi kufanya biashara na taasisi yake. Tunayo mifano ya baadhi ya Halmashauri kama vile Nzega ambayo baadhi ya wahusika wameshinikiza wakitaka zabuni zote wapewe madiwani. Jambo hili halikubaliki na tena ni kinyume cha maadili ya utumishi.

 

19. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa siyo kila chanzo cha mapato ya Halmashauri kitakusanywa kwa ufanisi kwa kutumia au kwa kutotumia Mawakala, Halmashauri zitaelekezwa kwa waraka ni vyanzo vipi vitahitaji kutumia Mawakala. Kwa baadhi ya vyanzo katika ukusanyaji wa mapato zitapaswa kukusanywa na Halmashauri zenyewe kwa kuzingatia Miongozo iliyotolewa na Serikali. Moja ya Miongozo hiyo ni kwamba kuanzia sasa, aidha kutumia Mawakala au Halmashauri zenyewe ni lazima fedha zinazokusanywa ziwekwe kwenye Akaunti ya Halmashauri na kutumia mifumo ya kielecktroniki ili kupunguza au kumaliza kabisa masuala ya “cash transactions”. Aidha, Halmashauri zikubaliane na wakala ni kiasi gani cha asilimia ya makusanyo kitalipwa kwa wakala na malipo yafanyike baada ya kukusanya na kuingizwa kwenye akaunti ya Halmashauri.

 

20. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kuziagiza Halmashauri zote nchini kwamba kuanzia tarehe Mosi Julai, 2016 zihakikishe zinatumia mifumo ya kielektroniki katika kukusanya mapato, katika kulipa, kuweka na kutekeleza kikamilifu mikakati madhubuti ya kuboresha makusanyo iwe yanakusanywa na Halmashauri au na Wakala.

 

UWAJIBIKAJI NA UADILIFU

 

21. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kuimarisha uwajibikaji na maadili kwa viongozi, watendaji na watumishi wa umma ili kujenga imani ya wananchi kwa viongozi na Serikali yao. Hatua hiyo inakusudia kuhakikisha kuna matumizi mazuri ya rasilimali za umma; kudhibiti mianya ya ukiukwaji wa maadili na rushwa; na kujenga ujasiri wa kusimamia sheria, kanuni, na taratibu za utumishi umma. Viongozi pia wanatakiwa kuepuka vitendo vya rushwa; mgongano wa maslahi; kushindwa kutoa Tamko la Rasilimali na Madeni au kutoa Tamko la Uongo; unyanyasaji wa kijinsia; kuomba, kupokea, kushawishi na kujipatia masilahi ya kifedha yasiyostahili; na kukiuka miiko ya uongozi. Serikali ya Awamu ya Tano haitasita kuchukua hatua stahiki kwa viongozi wa umma au watumishi wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma. Hivyo, kuzingatia maadili siyo suala la hiari bali ni lazima.

 

MAHAKAMA YA MAKOSA YA RUSHWA NA UFISADI

 

22. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao kutokana na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali katika kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi. Tulipoanza mapambano hayo baadhi ya watu walidhani ni nguvu za soda tu. Si kweli hata kidogo. Napenda kulitaarifu Bunge hili Tukufu kuwa zoezi hili ni endelevu na tangu mwezi Novemba, 2015, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani, mapambano hayo yamechukua sura ifuatayo:-

Kwanza: Uchukuaji wa hatua za kinidhamu dhidi ya mtumishi yeyote wa umma anayetuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa na ufisadi kwa kuwasimamisha kazi na kuendesha uchunguzi ili hatua stahiki za kisheria na kiutawala zichukuliwe; na

Pili: Kutengua teuzi au madaraka kwa viongozi juu walioshindwa kutekeleza wajibu wao.

 

23. Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya nyingine kubwa iliyochukuliwa ni uanzishwaji wa Mahakama Maalum ya kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi. Itakumbukwa kuwa wakati wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, aliyekuwa mgombea Urais wa CCM, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, aliahidi kuanzisha Mahakama hiyo na sasa ahadi hiyo kaitimiza. Kutimizwa kwa ahadi hiyo ndani ya kipindi cha miezi isiyozidi saba inaonesha dhamira thabiti ya Serikali kushughulikia makosa ya rushwa na ufisadi kwa utaratibu wa kudumu. Hivyo, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Mahakama hiyo itaanza rasmi kazi zake tarehe 1 Julai, 2016.

 

24. Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya faida za kuwa na Mahakama hii maalumu ni kama ifuatavyo:-


Kwanza: Mashauri ya rushwa na ufisadi yatasikilizwa kwa muda mfupi zaidi na hivyo haki kutendeka kwa pande zote mbili, yaani upande wa watuhumiwa na upande wa Jamhuri;

Pili: Majaji watakaosikiliza mashauri haya watakuwa na uelewa mpana zaidi kuhusiana na sheria za shughulikia masuala ya rushwa na ufisadi;

Tatu: Uwepo wa Mahakama hii utaimarisha zaidi taasisi za uwajibikaji nchini zinazohusika na mapambano dhidi ya rushwa, mathalan, Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Nchini (PCCB);

Nne: Mahakama itawafanya watu waliozoea rushwa na ufisadi kujiuliza mara mbili kabla ya kuufanya uhalifu huo, yaani kuwa deterrent, kwa kuwa sambamba na kuanzishwa kwa Mahakama hiyo. Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini Namba 11 ya Mwaka 2007 inafanyiwa marekebisho ili kuongeza ukubwa wa adhabu zinazotolewa hivi sasa;

Tano: Kuhamasisha watoa taarifa za rushwa na ufisadi, yaani Whistle Blowers, kwa kuwa Serikali imebaini kuwa ili Mahakama hiyo ifikie malengo ya kuanzishwa kwake budi iwepo sheria madhubuti ya kuwalinda wananchi wetu wanatoa taarifa. Hivyo, Serikali ipo katika mchakato wa kuipitia upya sheria husika ili kuwahakikishia usalama wao wanapotoa taarifa za kutendeka kwa makosa ya rushwa na ufisadi na kuwapa ujasiri wa kutoa ushahidi mahakamani; na

Sita: Kuhamasisha Wafanyabiashara kufanya biashara zao bila mashaka, muhimu kwao ni kulipa kodi kwa wale waliokuwa wanakwepa kulipa kodi. Pia kuwapa imani wafadhili wetu kwamba fedha wanayochangia haitapotea. Zoezi hilo linaendelea ili kuhakikisha hakuna fedha ya Serikali inayopotea.

 

25. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapenda kuwashukuru wananchi wote waliotoa taarifa zilizosaidia kubaini watumishi wa umma na raia ambao wanajihusisha na vitendo vinavyokiuka uadilifu na kuisababishia Serikali hasara. Ni kweli kwamba Serikali haiwezi kufanikiwa peke yake katika vita dhidi ya ufisadi na maovu mengine kama wananchi na wadau wengine hawataiunga mkono katika jitihada zake za kupambana na vitendo hivyo. Kwa hiyo natoa rai kwa wananchi na wadau wengine, hususan Asasi Zisizo za Serikali na Asasi za Kijamii kuendelea kutoa ushirikiano ipasavyo ili kufanikisha mikakati ya kupambana na rushwa na ufisadi na vitendo vingine visivyo vya kiadilifu katika Taifa letu. Aidha, ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa kufanya kazi kikamilifu kuanzia ngazi ya familia. Tabia ya baadhi ya vijana kuacha kufanya kazi na kujiingiza kwenye unywaji pombe ama kucheza “Pool” kwa siku nzima iachwe mara moja.

 

26. Aidha, kwa upande wa uwajibikaji wamiliki wa maeneo ya starehe bar na pubs wazingatie sheria na muda unaotakiwa kufungua biashara hizo. Kinyume cha hapo, hali hiyo ikiachiwa iendelee hivyo, nguvu kazi kubwa ya Taifa ambayo ni vijana itapotelea kwenye ulevi na hivyo kushindwa kutoa mchango wake kwa Taifa. Ili kudhibiti hali hiyo, nawaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini kuhakikisha vijana wanawajibika ipasavyo katika maeneo yao kwa kufanya kazi halali na kuhakikisha kwamba maeneo ya starehe (Bar na pubs) hayafunguliwi wakati wa muda wa kazi ili vijana na watu wengine waende kufanya kazi kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. Elimu kwa umma iendelee kutolewa na usimamizi uimarishwe.

 

HALI YA UPATIKANAJI WA CHAKULA NCHINI

 

27. Mheshimiwa Naibu Spika, uchambuzi wa awali wa taarifa ya hali ya chakula nchini uliofanywa mwezi Mei 2016, unaonesha kuwa, hali ya chakula nchini ni ya kuridhisha na matarajio ya uzalishaji kwa msimu wa 2015/2016 ni mzuri. Kati ya Halmashauri 174 zilizofanyiwa tathmini, Halmashauri 52 (asilimia 30) zitakuwa na ziada ya chakula, Halmashauri 116 (asilimia 66) zitakuwa na utoshelevu wakati Halmashauri 7 (asilimia 4) katika mikoa mitano ya Iringa, Kilimanjaro, Dodoma, Mwanza na Pwani zitakuwa na upungufu wa chakula kutokana na sababu mbalimbali kama vile mafuriko na upungufu wa mvua. Hata hivyo, hali halisi itadhihirika baada ya kukamilika kwa tathmini ya uzalishaji wa mazao ya chakula iliyomalizika tarehe 30 Juni, 2016. Tathmini hiyo itabainisha kwa undani viwango vya uzalishaji, mahitaji na utoshelevu wa chakula nchini. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ijipange vizuri kununua mahindi hayo kama nilivyoagiza kwa kuanzisha vituo vya ununuzi karibu na wananchi.

 

28. Mheshimiwa Naibu Spika, hadi tarehe 01 Julai, 2015, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ulikuwa na akiba ya nafaka tani 353,702. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 Wakala uliendelea na ununuzi wa nafaka katika kanda ya Songea, Makambako na Sumbawanga. Akiba hii imewezesha Serikali kukabiliana na uhaba wa chakula uliojitokeza sehemu mbalimbali nchini katika mwaka 2015/2016, ambapo jumla ya tani 31,666 zilipelekwa sehemu zenye uhaba wa chakula nchini. Hivyo, akiba ya chakula katika maghala hadi tarehe 09 Juni, 2016 tuna tani 62,312. Aidha, Wakala unatarajia kufunga mwaka tukiwa tuna kiasi cha tani 50,000 za nafaka. Katika mwaka ujao wa 2016/2017, Wakala umepanga kununua kiasi cha tani 100,000 za nafaka kutoka katika maeneo yenye ziada kubwa ya uzalishaji.

 

UPATIKANAJI WA SUKARI NCHINI

 

29. Mheshimiwa Naibu Spika, katika siku za hivi karibuni, Nchi yetu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upatikanaji na usambazaji wa sukari kutokana na ukweli kwamba mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji. Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 2015/2016, Serikali imetoa vibali vya kuingiza sukari nchini Tani 80,000 ili kufidia pengo lililopo. Hadi kufikia tarehe 9 Juni, 2016 jumla ya Tani 23,874.6  za sukari zilikuwa zimeingizwa nchini. Aidha, taarifa zilizopo zinaonesha kuwa hadi tarehe 30 Juni, 2016 tayari Tani 63,000 za sukari zimeingizwa na kusambazwa maeneo mbalimbali nchini. Kwa bahati mbaya, pamoja na kuingizwa nchini kiasi hicho kikubwa cha sukari katika kipindi kifupi, bado soko la sukari limeendelea kuyumba kutokana hisia tu kuwa sukari iliyopo haitoshi. Matokeo yake ni kwamba sukari imeendelea kuuzwa kwa bei ya rejereja ya kati ya Shilingi 2,500 na 3,000 kwa kilo katika makao makuu ya Mikoa na Wilaya. Serikali itaendelea kusimamia kushuka kwa bei hiyo ili mlaji wa chini amudu kuinunua kwa gharama ndogo zaidi na kazi hiyo inaendelea.

 

30. Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hali hiyo, njia pekee na endelevu ya kuondokana na uhaba wa sukari ambao umekuwepo miaka yote ni kuongeza uzalishaji wa sukari yetu wenyewe. Hivyo, Serikali inakamilisha Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Sukari kwa Miaka Mitano ijayo (2016/17-2020/21). Lengo kuu la Mpango Mkakati huo ni kuongeza uzalishaji kama  ifuatavyo:-

 

Kwanza: Kufanya tathmini upya ili kujua mahitaji halisi ya sukari nchini kwani pamoja na kiwango kilichoingia cha tani 63,000 bado kuna upungufu.

Pili: Kuongeza uzalishaji wa sukari katika viwanda vilivyopo hadi kufikia Tani 459,503 mwaka 2020/2021 kwa kuimarisha tija katika uzalishaji miwa na kuongeza ufanisi wa viwanda hivyo;

Tatu: Kuanzisha viwanda vipya vya sukari, ambapo vitaanzishwa  viwanda vya kati vitatu katika Wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero pamoja na kuanzisha viwanda vikubwa katika maeneo ya Bagamoyo, Rufiji, Kigoma na Kidunda.

Nne: Kuongeza tija na uzalishaji wa miwa inayolimwa na wakulima wadogo kwa kuboresha upatikanaji wa pembejeo, miundombinu ya umwagiliaji na kuboresha mfumo wa uendeshaji wa vyama vya wakulima wa miwa;

Tano: Kufanya marekebisho ya Sheria ya Sukari ya mwaka 2001 na kanuni zake, ili kuweka wigo mpana zaidi wa kusimamia na kuboresha huduma za udhibiti katika tasnia ya sukari; na

Sita: Kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuwajengea wakulima na wazalishaji wa sukari uwezo wa kitaalamu ili waweze kuendesha kilimo na kuzalisha kwa tija, kwa kuwafunza kanuni bora za uzalishaji miwa na sukari, kuboresha huduma za utafiti, mafunzo na ugani kwa wakulima wadogo.

 

MKAKATI WA UJENZI WA UCHUMI WA VIWANDA

 

31. Mheshimiwa Naibu Spika, dhima ya Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa Mwaka 2016/2017 – 2020/2021 ni kuanza ujenzi wa Taifa lenye Uchumi wa Kati unaoendeshwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. lli kufikia azma hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeandaa Mpango Kazi wa kutekeleza malengo hayo katika kipindi cha miaka mitano (2015 - 2020). Mpango huo utahusisha sekta zote za uchumi na huduma ili kutekeleza jukumu la kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa na kuongeza ajira kwa umma hususan kwa vijana na wanawake. Mpango huo unakusudia kuendeleza viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, na hususan kwenye sekta za kilimo na maliasili; viwanda vinavyozingatia fursa za kijiografia; viwanda vinavyotumia nguvu kazi zaidi (kuzalisha ajira); na viwanda vinavyoendana na ukuaji wa miji. Mpango huo unakusudia pia kuanzisha viwanda vitakavyozalisha bidhaa kukidhi mazingira ya kibiashara ndani na nje ya Nchi na kuwekeza zaidi kwenye rasilimali watu; na viwanda vinavyozaa viwanda vingine. Viwanda vinavyolengwa ni vya mbolea na kemikali zitokanazo na mafuta jamii ya petroli au gesi asilia, chuma (iron & steel), nguo na mavazi, usindikaji mazao ikiwemo mafuta ya kula, ubanguaji wa korosho, matunda, maziwa na bidhaa zitokanazo na maziwa pamoja na ngozi.

 

32. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maneno mengine, msingi wa maendeleo yetu kutoka sasa ni Sekta ya Viwanda. Serikali imechukua uamuzi huo kwa sababu imejiridhisha kuwa, kutokana na uzoefu na historia ya Nchi nyingine, ujenzi wa uchumi wa viwanda utaliweka Taifa letu katika kundi la mataifa yanayozalisha bidhaa bora na zenye ushindani wa soko la kimataifa badala ya kuwa chanzo cha malighafi na soko la bidhaa kwa viwanda vya mataifa mengine. Muhimu, ni Watanzania kubadili mtazamo na kujenga utamaduni unaolenga kuwa na Taifa lenye uchumi wa viwanda. Hiyo ni pamoja na kila mmoja wetu kwa uwezo wake kulenga kuwekeza katika viwanda na kupenda kununua bidhaa zinazozalishwa nchini.

 

33. Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tulizojifunza kutokana na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Viwanda vya Msingi (Basic Industrialization Strategy) miaka ya 1980, ambapo viwanda vingi vilivyoanzishwa chini ya usimamizi wa Serikali vilikufa kutokana na sababu mbalimbali, zimeifanya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza Mpango huo kuendelea kuipa sekta binafsi jukumu la ujenzi na uendeshaji viwanda na biashara nchini na Serikali ibaki na jukumu la kuweka mazingira wezeshi na rafiki ya kufanya biashara na uwekezaji. Huo ndiyo mwelekeo katika ujenzi wa sekta ya viwanda unaohamasishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

 

34. Mheshimiwa Naibu Spika; nimelazimika kutoa ufafanuzi huo wa kisera kwa sababu katika siku za karibuni kumekuwepo sintofahamu kwa baadhi ya watu kudhani sasa Serikali itajiingiza moja kwa moja katika ujenzi wa viwanda na kufanya biashara. Napenda kuihakikishia sekta binafsi kuwa itaendelea kuenziwa kwa sababu ni injini pekee ya ukuzaji uchumi na maendeleo ya viwanda katika karne hii. Aidha, Wizara husika zimejipanga vema katika kuhakikisha Watanzania wanashirikishwa ipasavyo katika kujenga uchumi wa viwanda.

 

35. Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha mafanikio yaliyokusudiwa yanapatikana, ni lazima kuzingatia yafuatayo:

 

Kwanza: Kuhakikisha viwanda vilivyopo vinafanya kazi kwa uwezo mkubwa na bidhaa toka nje zinatozwa ushuru stahiki na kukidhi viwango vya ubora ili kudhibiti ushindani usio halali nchini;

Pili: Kuhimiza na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vitakavyotumia malighafi ipatikanayo nchini, mathalan viwanda vya saruji kutumia gypsum na makaa ya mawe ambayo tayari yanapatikana hapa nchini kwetu kwa wingi zaidi;

Tatu: Kuondoa vikwazo vinavyopunguza uwezo wa kiushindani kwa viwanda vyetu kwa uboresha mazingira ya uwekezaji ili Tanzania iwe kivutio kwa wawekezaji wa ndani na nje, mathalan kwa kuhakikisha kunakuwepo umeme wa kutosha na wa uhakika, maji, uchukuzi na usafishaji wenye ufanisi, urahisi wa taratibu za udhibiti na usimamizi kwa kupunguza mlolongo wa taratibu na uwingi wa tozo;

Nne: Kuhamasisha wawekezaji wakubwa wa ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya viwanda katika ngazi ya kanda na Taifa;

Tano: Kuhakikisha kuwa viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi kwa ufanisi, ama kwa kuwataka wawekezaji wa viwanda husika kufanya uwekezaji mpya ndani ya miezi 12 na watakaoshindwa kunyang’anywa ili wapewe wawekezaji wapya na wenye uwezo;

Sita: Maafisa Biashara wa Mikoa kupewa jukumu mahsusi la kuwa kiungo kati ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika kusimamia na kuhamasisha uwekezaji wa viwanda katika Mkoa na pia Biashara na Masoko; na

Saba: Kila Mkoa kutenga maeneo mahsusi ya uwekezaji viwanda (Industrial Parks) yatakayowekewa miundombinu ya msingi ili kumuondolea mwekezaji usumbufu wa kutafuta eneo la uwekezaji ambao hivi sasa huchukua hata miaka mitatu kabla ya uwekezaji kuanza. Badala yake tunataka mwekezaji mwenye fedha aweze kuanza ujenzi wa kiwanda ndani ya mwezi mmoja. Na huo ndiyo mkakati wetu.

 

36. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuwasaidia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ambao wanakusudia kuwekeza katika viwanda ili kunufaika na mchango wake katika uchumi ikiwemo uzalishaji wa ajira kwa Watanzania. Natoa wito kwa wananchi na Watanzania wote kutambua fursa zilizopo kwa kubaini sehemu ambayo kila mmoja anaimudu katika mnyororo wa manufaa ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

 

37. Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika Hotuba yangu ya Bajeti (2016/2017), nilielekeza Mamlaka za Mikoa na Wilaya lazima zitenge maeneo kwa shughuli za viwanda na biashara. Chini ya utaratibu huo, Mamlaka za Mikoa zitawajibika kutenga maeneo ya ujenzi wa viwanda na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itawajibika kutoa ushauri wa kitaalam. Aidha, wizara na taasisi zinazohusika na ujenzi wa miundombinu wezeshi zitawajibika kuhakikisha maeneo hayo yanapatiwa huduma hizo muhimu. Mamlaka za Serikali za Mitaa zitabeba gharama za kutenga maeneo katika Kata, Tarafa na Wilaya.

 

38. Mheshimiwa Naibu Spika, katika ngazi ya kitaifa, tutaendeleza jitihada za kutenga na kuboresha maeneo maalum ya kiuchumi ili kurahisisha uwekezaji mkubwa katika sekta ya viwanda. Kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha kwamba fidia inalipwa kwa maeneo yaliyotengwa katika siku za nyuma. Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa hadi sasa, Halmashauri 10 tayari zimeshatenga jumla ya ekari 64,348 katika mikoa 10 ya Mara; Tanga; Ruvuma; Mtwara; Mwanza; Pwani; Arusha; Shinyanga; Iringa na Dar es Salaam.

Natoa wito kwa Halmashauri nyingine kutenga maeneo ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda. Aidha, Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zihakikishe kuwa Halmashauri zote nchini zinazingatia mahitaji ya viwanda kwa kutenga maeneo maalum katika mipango miji yake. Vilevile, nazitaka taasisi za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zianze kutekeleza agizo la Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, la kuitaka Mifuko hiyo iwekeze kwenye viwanda badala ya kujikita zaidi kwenye ujenzi wa majumba makubwa katikati ya miji.

 

HALI YA USHIRIKA NCHINI

 

39. Mheshimiwa Naibu Spika, ushirika nchini umeendelea kuwa sekta muhimu katika maendeleo ya jamii, kujenga uchumi wa wanachama na kuchangia pato la taifa. Umuhimu huu umetokana pia na kuwaunganisha wakulima na wanachama katika uzalishaji, ukusanyaji mazao na upatikanaji wa masoko. Pia ushirika umedhihirisha umuhimu wake kwa kujitokeza katika sekta mbalimbali za kiuchumi nchini zikiwemo sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, nyumba, usafirishaji, huduma, madini na fedha.

 

40. Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2015/16, Serikali imeendelea kufanya uhakiki wa kubaini uhai wa Vyama vya Ushirika ikiwa ni pamoja na kuboresha Daftari la Vyama vya Ushirika nchini. Hadi kufikia Juni 2016, uhakiki huo umebaini kuwa idadi ya vyama vya ushirika vilivyo hai ni vyama 8,766 ikiwa ni ongezeko la vyama vya ushirika 878 sawa na ongezeko la asilimia 11.1, ikilinganishwa na vyama 7,888 vilivyokuwepo Machi, 2015. Ushirika umechangia kutoa ajira za kudumu katika jamii ambapo kwa wastani kila chama huajiri takribani watendaji watano sawa na ajira 43,830 kwa idadi ya vyama vilivyopo.

Changamoto za Ushirika

 

41. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ushirika nchini kuendelea kuwa sekta muhimu katika maendeleo ya jamii, umekumbwa na changamoto zifutazo:-

Moja: Rasilimali za ushirika kuvamiwa na watu na taasisi mbalimbali.

Mbili: Vyama vya ushirika kuwa na madeni makubwa yasiyolipika.

Tatu: Ubadhirifu na wizi katika vyama vya ushirika.

Nne: Baadhi ya rasilimali za ushirika kutoendelezwa na kukosa hati miliki

Tano: Kesi nyingi za vyama vya ushirika kuchukua muda mrefu kutolewa maamuzi.

Sita: Mapungufu katika usimamizi na matumizi ya mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani kwa baadhi ya mazao.

Hatua zilizochukuliwa kukabiliana na changamoto

42. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imechukua hatua zifuatazo:-

Kwanza: Tume ya maendeleo ya ushirika imeandaa utaratibu wa kuzitambua mali za ushirika na kuweka mpango wa kuziendeleza kupitia mkutano ulioshirikisha wenyeviti na watendaji wakuu wa vyama vikuu na mabenki pamoja na Warajis Wasaidizi wa Mikoa.

Pili: Pia kupitia mkutano uliofanyika Dodoma wa Vyama Vikuu vya Ushirika uliwekwa utaratibu wa kuhakikisha madeni ya vyama vya ushirika yanapungua na kuisha kabisa. Aidha, Tume kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi itakutana na mabenki na taasisi nyingine za fedha kujadiliana na kuweka utaratibu rafiki wa kuhakikisha kuwa madeni haya yanakwisha na kutotengeneza madeni mapya.

Tatu: Tume ya maendeleo ya ushirika imeanza kuwaondoa viongozi wote wabadhirifu (wakiwemo Warajis Wasaidizi) madarakani na kuwachukulia hatua za kisheria.

Nne: Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika inawasiliana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kuhakikisha kesi zote za Vyama vya Ushirika zinashughuikiwa kwa haraka zaidi, ili hatua stahiki zichukuliwe.

Tano: Serikali inaendelea kurekebisha tozo za mazao mbalimbali ili kukidhi matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani kwa mazao kama korosho na mfumo wa stakabadhi ghalani utaendelea kutumika pamoja na marekebisho ya tozo yaliyofanywa.

43. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha ushirika nchini, Serikali itahakikisha kuwa Sheria ya Ushirika Na. 6 mwaka 2013 ambayo inaimarisha usimamizi wa ushirika nchini na kuainisha hatua kali ambazo zitachukuliwa dhidi ya wale wote wanaokiuka Sheria hiyo, inatekelezwa ipasavyo.

 

MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA

 

44. Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kuwa Jiji la Dar es Salaam, kwa muda mrefu, limekuwa linakabiliwa na changamoto ya usafiri kutokana na ukosefu wa miundombinu ya barabara, msongamano wa magari na wingi wa abiria. Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2002 inaonesha kwamba Jiji la Dar es Salaam lina watu wapatao Milioni 4.3 ambao wamekuwa wakipoteza muda mwingi njiani kutokana na msongamano wa magari. Hali hiyo imewaathiri sana kiuchumi na kijamii. Kutokana na hali hiyo, Serikali mwaka 2002 ilibuni Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) ambao utatumia mabasi yanayobeba abiria wengi kwa wakati mmoja na ambayo yanatumia muda mfupi kusafirisha abiria kutoka sehemu moja hadi nyingine na kwa gharama nafuu. Mradi huo unajengwa kwa awamu sita na utahusisha barabara zenye urefu wa jumla ya kilomita 130.3.

 

45. Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya awamu ya kwanza inayojumuisha barabara zenye urefu wa jumla ya kilometa 20.9 umekamilika. Maeneo yaliyokamilika ni pamoja na barabara kuu kutoka Kimara mwisho hadi Kivukoni, barabara ya Kawawa kuanzia Morocco hadi Magomeni Mapipa na Barabara ya Msimbazi hadi Kariakoo Gerezani. Ujenzi wa barabara hizo unajumuisha pia njia maalum za mabasi, njia za magari mchanganyiko na njia za waendesha baiskeli na waendao kwa miguu. Aidha, Vituo vidogo 27 vimejengwa katika barabara maalum za mfumo wa DART na Vituo Vikuu vitano yaani ‘Bus Terminals’ vimekamilika. Vituo Mlisho vinne yaani ‘Feeder Bus Stations’, karakana moja ya mabasi ‘Depot’, pamoja na madaraja ya watembeao kwa miguu katika maeneo ya Kimara, Ubungo na Morocco yamekamilika.

 

46. Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza, Serikali iliamua apatikane mtoa huduma ya mpito ‘Interim Service Provider’ ili miundombinu ianze kutumika. Mabasi hayo yalianza kutoa huduma tarehe 10 Mei, 2016 na idadi yake kwa sasa ni 140. Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa wananchi wengi wamejitokeza kupanda mabasi hayo na wanayafurahia na wanasafiri bila bughudha.

 

47. Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mradi huo unakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo mfumo usiokuwa na kasi ya kutosha ambao unasababisha msongamano wa abiria wakati wa utoaji  tiketi nyakati za asubuhi na jioni wakati mtandao unapokuwa umeelemewa; abiria kugombania kupanda mabasi kuwahi kupata viti; kutokupanga foleni wakati wa kukata tiketi na wakati wa kupanda mabasi; abiria kutofuata njia zilizobainishwa kuingia na kutoka kwenye vituo kama madaraja ya miguu, vivuko vya pundamilia na kutumia milango ya vituo vidogo; na ajali zinazotokana na vyombo vingine vya usafiri kutumia kimakosa barabara za DART zikiwemo bodaboda, baiskeli, magari, daladala na waenda kwa miguu.

 

48. Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuzipatia ufumbuzi wa haraka, changamoto hizo, Serikali imetoa maelekezo yafuatayo:-

Kwanza: Kila njia iwe na alama maalum kwa mfano namba au rangi ambayo itatumiwa na Mabasi Yaendayo Haraka yanayofanya safari kupitia njia hiyo ili iwe rahisi kwa abiria kutambua mabasi hayo kwa namba au rangi zake;

Pili: Abiria kujali usafi ndani ya mabasi na kwenye vituo vya abiria. Aidha, walinzi kwenye vituo vya abiria pamoja na majukumu yao ya ulinzi na usalama wafanye pia kazi ya kudhibiti uchafuzi wa mazingira katika vituo vya abiria vya mabasi hayo, kuhakikisha milango yote ya vituo imefungwa wakati wote;

Tatu: Muda wa kuanza safari uwe saa 11 alfajiri ili kuruhusu abiria kuanza safari mapema.

Nne: Maduka ya kununua kadi yatambulishwe haraka ili wananchi waanze kumiliki kadi hizo zitakazojulikana kama DART CARD.

Tano: Kuweka taa maalum za barabarani kwenye makutano hatari ya barabara ili kuzuia magari mengine yasipite wakati Mabasi Yaendayo Haraka yakipita. Lengo ni kuepusha ajali na mabasi hayo kutopata vikwazo katika safari zake.

Sita: Ni marufuku kwa chombo au mtu yeyote kutumia njia za mabasi hayo.

 

49. Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mabasi hayo yakitumia muda mfupi usiozidi dakika 45 kwa safari ya kutoka Kivukoni hadi Kimara na kuwezesha abiria kuwahi kwenye shughuli zao za kila siku. Kabla ya mradi huo kuanza, safari ya aina hiyo ilikuwa inatumia zaidi ya saa mbili. Aidha, kumekuwepo na faida za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wanaoishi karibu na barabara ya DART ambao wameacha kutumia magari yao binafsi na kuanza kupanda mabasi hayo. Kwa kufanya hivyo wameweza kuokoa fedha nyingi za kununulia mafuta ya vyombo vyao vya usafiri.

 

50. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza mchakato wa Mpango wa ujenzi wa Awamu ya Pili na Tatu katika barabara ya Mbagala na Gongo la Mboto ili wananchi wa maeneo hayo waanze kufaidi huduma hizo za Mabasi Yaendayo Haraka. Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi na wakazi wote wa Dar es Salaam ambao wamepata fursa ya kutumia huduma hii kutoa ushirikiano katika uendeshaji wa mradi huo. Tumeanza vizuri, nawaomba tushirikiane kutunza miundombinu iliyopo, ikiwa ni pamoja na kulinda mazingira. Aidha, vyombo vingine vya usafiri haviruhusiwi kutumia miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka kwa sababu vitayasababishia ajali mabasi hayo. Vyombo vya dola vihakikishe kuwa wale wote wanaotumia barabara hizo kinyume na utaratibu uliopo wanachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine.

 

MIRADI YA UMEME VIJIJINI

 

51. Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 23 – 27 Mei, 2016 nilipata fursa ya kumwakilisha Mheshimiwa Rais, Dkt.John Pombe Magufuli, kwenye Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) uliofanyika Lusaka – Zambia. Kaulimbiu ya Mkutano huo isemayo “LIGHT UP Africa using centralized and decentralized mini-grid solutions” inaakisi azma ya Serikali yetu kusambaza nishati ya umeme nchi nzima katika ngazi zote hadi vijijini. Hivyo, miongoni mwa maazimio ya Mkutano huo ilikuwa kuzitaka nchi za Afrika kutekeleza kaulimbiu hiyo kwa vitendo. Katika utekelezaji wa kaulimbiu hiyo:-

(i) Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kuyapatia maeneo yaliyo nje ya Gridi ya Taifa nishati bora ikiwa ni pamoja na maeneo ya visiwa. Wakala wa Usambazaji wa Umeme Vijijini (REA) inakamilisha taratibu za uendeshaji (Operating Guidelines) kwa waendelezaji wa mini-grids. Taratibu hizi zinategemewa kukamilika mwezi Julai, 2016 ili kuweza kushindanisha waendelezaji wa mini-grids, micro-grids na solar home systems. Aidha, Serikali za Sweden na Uingereza pia zimechangia katika Mfuko wa Nishati Vijijni ili kuendeleza mifumo hiyo. REA imeanzisha utaratibu wa kutoa mikopo, yaani Credit Facility, kwa ajili ya kukopesha waendelezaji wa nishati jadidifu (renewable energies) maeneo ya vijijini. Wakala pia imeanzisha Mfuko wa Ruzuku, yaani Revolving Fund Facility kwa waendelezaji nishati jadidifu ambao utachangiwa na wadau mbalimbali wa maendeleo.

(ii)    REA itashirikiana na Kampuni tanzu ya TANESCO na Tanzania Geothermal Development Company Ltd (TGDC) ili kuvipatia nishati bora vijiji vilivyo katika maeneo ambapo miundombinu ya jotoardhi itajengwa.

 

MPANGO WA TATU WA MIRADI YA REA

 

52. Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2015, Ibara ya 43(c) (iii), inaielekeza Serikali kutekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa REA ambao utalenga; kuongeza wigo wa usambazaji umeme kutoka REA I na II zilipoishia; kufikisha umeme kwenye huduma za jamii kama vile shule zote za sekondari, hospitali na vyanzo vya maji; kuongeza idadi ya vijiji ambavyo vinafikiwa na umeme; na kupeleka umeme maeneo yote ambayo si tija kwa TANESCO kuwekeza. Ili kutekeleza mipango hiyo, Serikali itatekeleza mambo yafuatayo:-

Kwanza: Mradi wa Densification kwa ajili ya kuongeza miundombinu ya nishati ya umeme kwenye maeneo ambayo REA I na II imepita lakini vijiji vingine havijapewa huduma ya umeme. Serikali za Norway na Sweden zimechangia fedha katika Mfuko wa Nishati Vijijini ili kutekeleza mpango huu; tunawashukuru sana.

Pili: Kufikisha huduma ya nishati bora kwa vijiji vyote ikiwa ni pamoja na maeneo/vijiji vilivyo nje ya Gridi (Off-Grid), lengo likiwa ni kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii na hatimaye kuongeza pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla; na

Tatu: Kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 534.4 za ndani na shilingi Bilioni 500 toka Benki ya Dunia, kwa muda wa miaka mitano, ili kuendeleza nishati vijijini. Wakala unaendelea kuhamasisha sekta za umma na binafsi ili zishiriki katika uendelezaji wa miundombinu ya nishati bora maeneo ya vijijini ambayo hayana tija kwa TANESCO kuwekeza kulingana na Sheria ya Nishati Vijijini ya mwaka 2005 na Sheria ya Umeme ya Mwaka 2008 zinatoa fursa na miongozo ya jinsi sekta hizi zinavyoweza kushiriki katika kutoa huduma hii muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi ili kukuza uchumi wetu.

 

UTEKELEZAJI WA MPANGO WA ELIMU BILA MALIPO

 

53. Mheshimiwa Naibu Spika; Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, ilianza utekelezaji wa ahadi ya utoaji wa elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi Kidato cha Nne kwa shule za umma kuanzia mwezi Januari 2016. Hii ni ahadi ambayo Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Makamu wa Rais waliitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Aidha, ahadi hii inazingatia Kifungu cha 52(a) cha Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, kinachohimiza uandaaji wa mfumo, mwenendo na taratibu nyumbufu za kutoa Elimu ya Awali na Elimu ya msingi bila malipo.

 

54. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, wadau mbalimbali pamoja na wananchi kwa kuunga mkono utekelezaji wa mpango huu. Aidha, niwashukuru wananchi ambao wametoa mwitikio chanya unaojidhihirisha kwa ongezeko kubwa na la kihistoria la uandikishaji wanafunzi katika ngazi mbalimbali. Kwa mfano; hadi mwezi Machi, 2016 wanafunzi wa elimu ya awali 971,717 waliandikishwa nchini kote, sawa na ongezeko la asilimia 10.74 ya wanafunzi 877,489 walioandikishwa mwaka 2015. Aidha, wanafunzi 1,896,584 wameandikishwa darasa la kwanza, sawa na ongezeko la asilimia 36.7 ikilinganishwa na wanafunzi 1,387,499 walioandikishwa mwaka 2015.

 

55. Mheshimiwa Naibu Spika; kila jambo jema halikosi changamoto, na ndivyo ilikuwa katika mpango huu. Hivyo, katika kuutekeleza mpango huo kumekuwapo na changamoto kadhaa ikiwemo upatikanaji wa miundombinu, samani pamoja na uelewa wa jamii juu ya wajibu wao kuhusu dhana ya elimu bila malipo. Katika kukabiliana na changamoto hizo, kati ya mwezi Desemba, 2015 hadi Mei 2016, Serikali imepeleka moja kwa moja katika ngazi ya shule jumla ya shilingi bilioni 94.2 kwa ajili ya fidia ya ada, michango mbalimbali na ruzuku ya uendeshaji wa shule. Aidha, kuanzia mwezi Julai, 2016 shule zenye idadi ndogo ya wanafunzi zitaanza kupelekewa kiwango maalumu ili kutosheleza uendeshaji wa shule kwa uwiano sawa na shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi. Katika kukabiliana na upatikanaji wa miundombinu mbalimbali shilingi bilioni 46.2 zimetengwa kupitia mipango na bajeti za Halmashauri kwa mwaka 2016/2017.

 

KUCHANGIA UPATIKANAJI WA MADAWATI

 

56. Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada za upatikanaji wa madawati zinaendelea vizuri kutokana na ushirikiano na michango kutoka kwa wadau mbalimbali. Mafanikio yaliyopatikana yametokana na kutumia fedha za makusanyanyo ya ndani ya Halmashauri, wadau kuchangia kwa hiari, harambee na uhamasishaji.

 

57. Mheshimiwa Naibu Spika; taarifa zilizokusanywa hadi kufikia tarehe 17 Juni, 2016 zinaonesha kuwa madawati mapya 552,630 yamepatikana kwa njia ya michango mbalimbali. Hatua hii ilifanya shule za msingi kuwa na madawati 2,632,392, sawa na asilimia 77 ya mahitaji. Hivyo bado kuna upungufu wa madawati 792,949 sawa na asilimia 23. Shule za sekondari zimefikisha madawati 1,395,138 sawa na asilimia 93 ya mahitaji. Hivyo bado kuna upungufu wa madawati 112,785 sawa na asilimia 7. Ni dhahiri kuwa kazi iliyofanyika ni kubwa na ya kutia matumaini sana ambayo imewezesha Halmashauri 25 kukamilisha mahitaji ya madawati kutoka mikoa 13 kwa madawati ya shule za msingi na Halmashauri 46 kutoka mikoa 19 kwa shule za sekondari. Napenda kutumia fursa hii kuwapongeza sana wadau mbalimbali kwa jitihada zao za kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais la kuhakikisha madawati ya kutosha yanapatikana shuleni linatekelezwa ipasavyo.

 

58. Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu napenda kuwapongeza sana wale wote waliochangia upatikanaji wa madawati ambao ni pamoja na:- Mheshimiwa Rais mwenyewe na Baraza lake la Mawaziri, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waheshimiwa Wabunge wenyewe kwenye maeneo yenu, Makatibu Wakuu wa Wizara, Benki Kuu ya Tanzania na Wafanyakazi wake ambao walikubali kutoa fedha zao kuchangia madawati, CRDB Bank, NMB, TANAPA, wafanyabiashara na wenye viwanda wakiongozwa na Dkt. Reginald Mengi, Vikundi vya Vijana, Mafundi Seremala, Msanii Naseeb Abdul Juma maarufu kama “Diamond” na mafundi magari wa gereji ya Tegeta. Niwapongeze pia Kamati ya Sherehe ya Harusi Ofisi ya Rais TAMISEMI ambao wametumia sehemu ya michango ya harusi ya watumishi wao kununua madawati 111 yenye thamani ya Shilingi Milioni 8.8, Tanzania China Peoples Friendship Promotion na wengine wengi ambao wamejitokeza kuchangia bila kusahau taasisi ya Hassan Maajar Trust (HMT) ambayo imechangia kwa miaka mitano mfululizo.  Huu ni mwamko wa kipekee ambao unaonesha kuwa jamii inaungana na Serikali katika kuchangia madawati bila kuzisahau Halmashauri zenyewe kwa kazi nzuri inayoendelea ya kukamilisha utengenezaji wa madawati.

 

59. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusisitiza kwamba Ofisi ya Rais TAMISEMI inakamilisha taarifa kamili ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa tarehe 15 Machi, 2016 kwa Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa, kuhakikisha wanamaliza tatizo la madawati ifikapo Juni 30, 2016. Nitapenda taarifa hiyo ikamilike kabla au ifikapo tarehe 15 Julai, 2016. Nitoe wito kwa wananchi na wasamaria wema, taasisi, mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa wote kwa ujumla kuona umuhimu wa kuchangia kwa hiari yao kutengeneza madawati ya kutosha kwa ajili ya watoto wetu. Kuhusu mgao kwa Waheshimiwa Wabunge, taratibu zinakamilishwa na mgao huo utatolewa hivi karibuni.

 

UGATUAJI WA MADARAKA

 

60. Mheshimiwa Naibu Spika, madhumuni ya kupeleka Madaraka kwa Wananchi ni kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi. Pia unazipa Mamlaka za Serikali za Mitaa uhuru wa kufanya maamuzi mbalimbali yahusuyo utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuwashirikisha katika kujiletea maendeleo na ustawi wao kwa ujumla. Hivyo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kutoa huduma za jamii kwa kuzingatia Ibara ya 145 na 146 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria za Serikali za Mitaa Sura 287 na 288. Endapo Mamlaka zitakwenda kinyume chake, Serikali Kuu inao wajibu wa Kikatiba na Kisheria kuingilia kati na kuchukua hatua stahiki dhidi ya Mamlaka hizo. Nitoe wito kwa Wakuu wa Wilaya wote kutimiza wajibu katika maeneo yao kwa mujibu wa Katiba ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali zinazoelekezwa katika maeneo husika.

 

61. Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa tija inapatikana katika madaraka ya kisiasa, majukumu, rasilimali fedha, rasilimali watu na muda; Serikali itaendelea kuelimisha wananchi juu ya sera ya kupeleka madaraka kwa wananchi (D by D) na kufanyia kazi sera na sheria zisizoendana na D by D ili kuzihuisha kulingana na mahitaji. Napenda kuziagiza Wizara husika za kisekta na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuweka mfumo na utaratibu wa kuwa na vikao vya kazi vya pamoja kufanya uchambuzi, tafsiri na tathmini ya utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia sera, sheria na hati idhini za kila Wizara kwa lengo la kupata ufanisi wa kutosha.

 

MIKOPO YA WANAFUNZI WA ELIMU YA JUU

 

62. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuimarisha mfumo wa utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu sambamba na kushughulikia changamoto mbalimbali zilizopo katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Ili kuhakikisha utoaji wa mikopo unafanyika kwa ufanisi; Serikali itabadilisha utaratibu wa kupanga na kutoa mikopo ili kuwafikia wanafunzi wote wenye uhitaji zaidi wakiwemo yatima na wenye uwezo mdogo kiuchumi bila kujali aina ya programu wanazozisoma. Kupitia Bunge lako tukufu napenda kuipongeza sana Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi kwa jitihada kubwa za kubaini ubadhirifu wa fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu. Serikali itaendelea kufanya uhakiki wa kina wa wanufaika wa mikopo na wote watakaobanika kujinufaisha binafsi watachukuliwa hatua kali za kisheria.

 

63. Mheshimiwa Naibu Spika, uwezo wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kuwahudumia walengwa unajengwa na fedha zinazotengwa kila mwaka katika mipango na bajeti pamoja na marejesho ya mikopo iliyoiva kutoka kwa wanaufaika. Serikali inaendelea kufanya maboresho ya kimfumo na kisheria ili kuimarisha urejeshwaji wa mikopo. Napenda kutumia nafasi hii kuwaagiza waajiri wote nchini kutekeleza wajibu wao wa kuingiza makato ya marejesho ya mikopo ya wanufaika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa baada ya kuwasiliana na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini.

 

USIMAMIZI NA UDHIBITI WA UBORA WA ELIMU

 

64. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba elimu bora ni msingi wa ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea. Ili kukidhi azma hii, Serikali imeweka kipaumbele katika kusimamia ubora wa elimu na kuhakikisha kuwa sera, sheria, kanuni, miongozo na viwango vya utoaji wa elimu nchini vinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuimarisha kaguzi za mara kwa mara katika shule zetu. Natoa wito kwa watendaji hususan Wakurugenzi wa Halmashauri na wadau wa elimu wote nchini, kupokea maoni na ushauri unaotolewa na wadhibiti ubora wa elimu na kuyafanyia kazi kwa wakati. Serikali itaimarisha idara hii ili iweze kukagua na kudhibiti shule zote na kutoa ushauri.

 

65. Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi kifupi nchi yetu imepata mafanikio makubwa ya kuongezeka kwa fursa za upatikanaji wa elimu nchini kutokana na kuongezeka kwa shule za awali, shule za msingi na sekondari, vyuo vya ufundi pamoja na vyuo vikuu. Ili kuhakikisha ukuaji wa sekta ya elimu unaambatana na ubora stahiki na kukidhi mahitaji ya sasa, Serikali itafanya mapitio na kuhuisha Sheria ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Vyuo Vikuu Nchini, kuimarisha mfumo wa ki-elektroniki wa udahili wa pamoja (Central Admission System) pamoja na kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuchukua hatua kali kwa taasisi zote za elimu zinazokiuka taratibu zilizowekwa.

 

HALI YA USALAMA NCHINI

 

66. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla hali ya usalama wa raia na mali zao ni shwari. Hata hivyo, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei 2016 kumekuwepo na matukio ya mauaji ambayo yameleta hofu kubwa kwa wananchi. Matukio hayo yametokea katika Mikoa ya Tanga, Geita, Mwanza, Mara na Dar es Salaam. Moja ya matukio hayo ni tukio la tarehe 18 Mei, 2016 lililotokea Ibanda relini mtaa wa Utemini Wilaya ya Nyamagana ambapo watu wapatao 15 wakiwa na mashoka, mapanga, visu na majambia, walivamia msikiti wa Masjid Rahman na kuwashambulia waumini waliokuwa wakiswali ndani ya msikiti huo. Wavamizi hao waliwaua kwa kuwakatakata mapanga watu watatu (3) na kumjeruhi mwanafunzi mmoja wa Shule ya Kiislam ya Jabaal.

 

67. Mheshimiwa Naibu Spika, matukio mengine ya mauaji makubwa ni yale yaliyotokea katika Mkoa wa Tanga mapema mwezi Aprili na mwishoni mwa mwezi Mei, 2016. Katika tukio la kwanza kundi la majambazi wakiwa na silaha mbalimbali zikiwemo za moto walivamia Super Market ya Central Bakery iliyopo mtaa wa Swahili jijini Tanga na kupora fedha ambapo watu watano walipigwa risasi na kufariki dunia papo hapo na mmoja kujeruhiwa. Aidha, tukio la pili lilitokea tarehe 31 Mei, 2016 usiku katika kitongoji cha Kibatini Kata ya Mzizima Tarafa ya Chumbageni ambapo watu wasiofahamika wakiwa na visu na mapanga waliwavamia wakazi wa eneo hilo lenye idadi ya nyumba 30 na kuua watu wanane kisha kutokomea katika msitu uliopo karibu na mapango ya Amboni.

 

68. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama ikiwemo Jeshi la Polisi imechukua hatua za haraka kwa kufanya operesheni maalum zilizowezesha kubainika na kukamatwa kwa baadhi ya watuhumiwa na wengine kuuawa baada ya kupambana na polisi kwa risasi za moto. Aidha, baadhi ya silaha zilikamatwa katika operesheni hizo na wote waliokamatwa wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria ili sheria ichukue mkondo wake. Nitumie fursa hii tena kuwapa pole viongozi na waumini wa Msikiti wa Masjid Rahman, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu waliouawa katika matukio yote ya mauaji kwa ujumla wao. “Mungu alaze Roho zao mahali pema peponi - Amina”.

 

69. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutumia vyombo vya usalama inaendelea na hatua za kuwatafuta wahusika wa matukio hayo yote waliokimbia ili wakipatikana wafikishwe kwenye vyombo vya dola kwa hatua zaidi za kisheria. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba matukio hayo ya kinyama kamwe hayatavumiliwa. Ni mwanzoni mwa juma hili tu ambapo kwa ujasiri mkubwa polisi wameweza kupambana na kiongozi wa wauaji wa raia kule Mwanza na Tanga na kufanikiwa kumuua. Serikali itawasaka wote waliohusika mpaka wapatikane ili sheria ichukue mkondo wake. Hata hivyo, ili kuwakamata wahusika, tunahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wananchi wenye mapenzi mema na nchi yao.

 

70. Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba matukio ya mauaji ya raia wasio na hatia hayakubaliki kabisa katika Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi na Watanzania wote kwamba jukumu la ulinzi na usalama wa nchi yetu ni la kila Mtanzania kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo basi, sote tuna wajibu wa kuzuia uvunjifu wa amani na uhalifu mahali tunapoishi au kufanyia kazi. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge, wanasiasa wote na viongozi wa madhehebu ya dini kutumia majukwaa ya siasa, mikutano ya dini na makongamano kusisitiza umoja wa kitaifa na hivyo kuungana na Serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu unaojitokeza.

 

71. Mheshimiwa Naibu Spika, nawasihi pia wanahabari wote kutumia kalamu zao na vyombo vya habari nchini kuandika habari zenye nia ya kuielimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuendelea kuifanya nchi yetu idumu kama kisiwa cha amani badala ya habari zenye kuleta hofu na uchochezi miongoni mwa jamii. Imani yangu ni kwamba tukifanikiwa kuleta amani kwenye nchi yetu, maendeleo yetu yatakua kwa kasi zaidi.

 

MATOKEO YA UCHUNGUZI WA MAABARA KUHUSU UGONJWA USIOJULIKANA KATIKA MKOA WA DODOMA

 

72. Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe 19 Juni, 2016, Serikali ilitoa taarifa kuhusu kuwepo kwa ugonjwa usiofahamika katika Wilaya za Chemba na Kondoa, Mkoani Dodoma ambapo jumla ya wagonjwa 21 na vifo 7 vilitokea. Hadi jana tarehe 29 Juni 2016 idadi ya wagonjwa ilikuwa imefikia 38 na vifo 10. Aidha, jumla ya wagonjwa 35 wamepatiwa huduma za matibabu katika Hospitali za Dodoma.

 

73. Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ugonjwa huo Serikali imepeleka jopo la Wataalam wa Afya kwenye maeneo yaliyoathirika ili kutambua kiini chake. Aidha, Sampuli mbalimbali zimekusanywa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Maabara ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TDFA), maabara ya Taifa ya Magonjwa ya Binadamu na maabara ya Hospitali ya KCMC. Hadi sasa, ni sampuli ya aina moja tu ya nafaka (hususan mahindi) ambayo matokeo yake yanaonesha kuwepo kwa uchafu wa sumukuvu (aflatoxin). Uchunguzi wa sampuli za aina nyingine bado unaendelea na tunatarajia kuzipeleka pia nchini Marekani kwa uchunguzi zaidi.

 

74. Mheshimiwa Naibu Spika, tangu kujitokeza kwa ugonjwa huo hadi sasa Serikali imechukua hatua zifuatazo:

Kwanza: Kukusanya sampuli, kuziwasilisha na kuzichunguza kwenye maabara mbalimbali;

Pili: Kutoa matibabu kwa wananchi walioathirika na ugonjwa huu; na

Tatu: Kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi za uandaaji wa chakula utakaosaidia kupunguza kiasi cha aflatoxin. Njia hizo ni pamoja na kuchambua na kuondoa nafaka zilizoharibika yaani zilizoooza, zilizovunjika, na zilizoharibika rangi.

 

75. Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kuwapa pole wote waliothirika na ugonjwa huu na tunawaombea waweze kupona haraka. Aidha, nawapa pole ndugu na jamaa wote waliopoteza ndugu zao. Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Serikali inafanya juhudi kuhakikisha ugonjwa huu unatokomezwa. Kwa maana hiyo, nawaagiza watendaji wanaohusika kuhakikisha matokeo ya sampuli zilizokusanywa yanapatikana mapema ili chanzo cha ugonjwa huo kijulikane.

 

76. Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuhitimisha hoja yangu napenda kusisitiza maeneo machache yafuatayo:-

Moja: Tumepitisha bajeti ya Serikali ambayo inategemea sana ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi wa wafadhili kutoka nje. Tuongeze juhudi za kukusanya na za kupanua wigo wa kutoza kodi ili mapato yaongezeke na hivyo kukusanya kodi ya kutosha. Aidha tushirikiane kwa dhati kubaini wakwepaji kodi na kuziba mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali.

Mbili: Pamoja na juhudi za kukusanya kodi tujenge utamaduni wa kudai risiti kila tunaponunua bidhaa yoyote dukani. Natambua changamoto zilizoko kwa wafanyabiashara ndogondogo ikiwa ni pamoja na wanaofanya biashara sokoni na katika minada ya wazi. Tutaendelea kujenga uwezo wa watumishi wanahusika na ukusanyaji wa mapato ili kukabiliana na changamoto hizo.

Tatu: Tumedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ili kuongeza mchango wa viwanda katika pato la Taifa na kuongeza ajira hususan kwa vijana na wanawake. Tuisaidie Serikali katika kubaini maeneo mazuri ya kuwekeza viwanda na kushiriki katika mnyororo wa uchumi kwa manufaa ya wananchi wote. Aidha, Mamlaka za Serikali za Mitaa zitenge maeneo maalum ya wafanyabiashara wadogo wakiwemo Wamachinga na Mama Lishe ili wafanye shughuli zao bila bughudha badala ya utaratibu wa sasa wa kuwaona kama wahalifu.

Nne: Tunao mradi mzuri wa Mabasi Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam. Niwaombe wananchi na wakazi wote wa Dar es Salaam kutoa ushirikiano katika kutunza miundombinu ya mradi huu, na kushiriki katika kutunza mazingira. Aidha, kwa waendesha pikipiki, baiskeli, na watembea kwa miguu, wanaombwa kuwa waangalifu na kuacha kabisa tabia ya kupita kwenye barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka.

Tano: Bado tunalo jukumu la kila mwananchi kushiriki katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi yetu. Tushirikiane kubaini matukio yoyote yanayoashiria uvunjifu wa amani na usalama wa raia.

Sita: Kwa watumishi wa umma, tuendelee kuhimiza umuhimu wa maadili katika sehemu zetu za kazi. Wote kwa pamoja tujenge utamaduni wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa umma.  Tujiepushe na vitendo vyovyote vya kukiuka taratibu za utumishi katika maeneo yetu ya kazi.

 

HITIMISHO

 

77. Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo, napenda nitumie nafasi hii kumpa pole Mheshimiwa Spika na tunamtakia apone haraka arudi tufanye naye kazi za kuwahudumia wananchi. Pia nikushukuru wewe binafsi, Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kusimamia vizuri na kwa weledi mkubwa vikao vyote vya mkutano huu. Niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu. Ninashukuru pia watendaji wa Serikali kwa kusaidia Mawaziri, Naibu Mawaziri katika kujibu hoja za Wabunge. Niwashukuru madereva wote kwa kuwaendesha Mawaziri, Wabunge na Watendaji wote kwa usalama kabisa. Kipekee nimshukuru Katibu wa Bunge na timu yake kwa kutuwezesha kukamilisha mkutano huu bila vikwazo.

 

78. Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahitimisha mkutano huu leo na kuelekea katika majimbo yetu, nitumie muda huu kumwomba Mwenyezi Mungu awalinde na awaongoze katika safari ya kurejea nyumbani. Aidha, tunapokaribia kuumaliza Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, napenda niwatakie Waislam wote na waumini wote kwa ujumla Idd - El - Fitr njema.

 

79. Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi tarehe 06 Septemba, 2016, siku ya Jumanne, Saa 3:00 asubuhi litakapokutana katika ukumbi huu hapa Dodoma.


80. Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.

 
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday120
mod_vvisit_counterYesterday170
mod_vvisit_counterThis week420
mod_vvisit_counterLast week1020
mod_vvisit_counterThis month4059
mod_vvisit_counterLast month4201
mod_vvisit_counterAll days447153
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved