Logo
Feature Stories

DocumentsDate added

Order by : Name | Date | Hits [ Ascendant ]

Ugawaji wa chakula cha msaada ulivyofanikiwa katika mkoa wa Manyara.

"Wananchi  ndio walioshika mpini wa misaada ya Chakula".

Hakuna shaka kuwa wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa misaada inayotolewa na Serikali imekuwa haiwafikii walengwa na  hata ikiwafikia walengwa si katika kiwango kile ambacho Serikali ilichokilenga .

Kutokana na athari ya  ukame ulioikumba  nchi yetu mwaka 2009 na hatimaye kuifanya baadhi ya mikoa  kaya zake kuathiriwa na njaa ,Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa chakula cha msaada kwa Mikoa 15 kwa ajili ya kusambazwa katika Wilaya 59 za Mikoa hiyo iliyokuwa na upungufu mkubwa wa chakula, Chakula hicho kilisambazwa kati ya mwezi Februari 2009 na Februari 2010.

Miongoni mwa mikoa 15 iliyopata chakula kutoka  Ofisi ya Waziri Mkuu ni mkoa wa Manyara ambao Wilaya zake tano (5)  ambazo ni: Kiteto,Simanjiro, Babati(V), Hanang na Mbulu ,zimenufaika na chakula cha msaada cha Serikali katika kipindi cha Februari 2009 na Februari 2010.

Kwa kutambua kuwa wananchi ndio wenye muarobaini pekee wa kuweza kuboresha ugawaji wa misaada itolewayo na serikali hasa ya Chakula, Mwezi Februari, 2010, Ofisi ya Waziri Mkuu ilifuatilia usambazaji wa chakula hicho.

Ofisi ya Waziri Mkuu ilifanya ufuatiliaji huo kwa madhumuni ya kujiridhisha na  kuhakikisha kuwa msaada huo umewafikia walengwa kwa wakati na wamepewa  kwa kiasi kilichopangwa. Aidha, lengo lingine ni kupata mrejesho (feedback) toka kwa mikoa, wilaya  na walengwa wenyewe juu ya utaratibu uliotumika kuainisha walengwa mahususi  wa kugawiwa chakula hicho.

Msemaji  wa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. David Kirway ambaye pia alishiriki katika kufanya tathmini katika Mkoa wa Manyara  anaeleza kuwa kwa kutambua kuwa  jamii ndiyo yenye mpini wa  ugawaji msaada wa chakula , Ofisi ya Waziri Mkuu ili wahoji walengwa ili Kupata taarifa za namna walivyogawiwa ama kuuziwa chakula kwa bei au kwa  kiasi  kilichopangwa na Serikali.

’’Pamoja na wajumbe wa Timu ya Ufuatiliaji kufanya mazungumzo na viongozi wa Mkoa, Wilaya na Vijiji vilivyogawiwa chakula cha  msaada lakini wajumbe wa Timu waliweza kufanya mazungumzo na wananchi walionufaika na chakula hicho kutoka katika vijiji viwili vya kila wilaya kutoka kata mbili tofauti, ambapo walengwa hao waliweza kutoa maoni yao.’’ Alisema Kirway

Katibu Tawala msaidizi wa mkoa wa  Manyara Dr. Elibariki Olomi anabainisha siri ya Mkoa wa Manyara kufanikiwa kugawa  na kuuza chakula kilichotolewa na Serikali  kwa bei nafuu  kwa wale walengwa kuwa ni ushirikishaji wa wanachi katika mchakato wa ugawaji chakula cha msaada kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.

Dr. Olomi anafafanua kuwa Mkoa wa Manyara ulichokifanya ni kufuata  vyema mwongozo wa  serikali  wa namna ya kuchagua walengwa na kuuza  chakula kwa kaya zilizoathirika na njaa ambapo kwa mujibu wa Mwongozo Kamati za maafa za Mkoa, na Wilaya  wanashirikiana kwa kuwahusisha wananchi  kupitia kamati yao ya Maafa ya kijiji ili kuhakikisha wananchi ndio wenye mamlaka ya kutambua walengwa wa misaada ya Maafa.

Kutokana na tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikiwakabili viongozi  wanao husika na ugawaji wa misaada ya Chakula kuwa huuza chakula cha msaada badala ya kuwagawia walengwa,  Mjumbe  Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Hanang Bw. Lukumay Marco anaeleza jinsi walivyo tegua kitendawili hicho.

 

Bw. Marco anafafanua kuwa uwazi katika ugawaji wa Chakula ndio hasa umeufanya mkoa wa Manyara kufanya vizuri katika ugawaji wa Chakula cha msaada kilichotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu.

''Mara tu tulipopata Chakula cha msaada kutoka mkoani tulichokifanya ni kukiweka chakula hicho  eneo la wazi ambapo kila mwanakijiji alikuwa ana uwezo wa kuona kiasi cha magunia tuliyopewa huku walinzi wa chakula hicho wakiwa ni miongoni mwa wanakijiji wenyewe waliowapendekeza kwa uaminifu wao’’Anasema Bw. Marco.

Anaendelea kueleza kuwa siku ya ugawaji chakula, Watendaji wa vijiji nao  walishirikishwa vilivyo pamoja na Kamati nzima ya kijiji, huku chakula kikiwekwa eneo la wazi  ambapo mlengwa mmoja mmoja anaitwa mbele ya walengwa wengine  na kupewa chakula kwa kiasi kilicho ridhiwa katika tathmini iliyo fanywa na kamati ya kijiji kwa kushirikiana na wanavijiji wenyewe.

Mlengwa wa msaada wa chakula cha Msaada cha Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Pepetua Rafaeli anadhihirisha jinsi  alivyo ridhishwa na utaratibu wa ugawaji wa chakula kwa kueleza kuwa kila kaya iliyo athirika na njaa  katika kijiji chao cha Galapo hakuna anaye nungunika aidha kwa kupewa au kuuziwa kiasi kisicho sitahiki jambo lilofanya watu kuweza kuikabili njaa.

 

Bi. Pepetua anafafanua kuwa wananchi walishuhudia kwa macho yao chakula cha msaada kikigawiwa siku moja katika eneo moja  la wazi mpaka mtu wa mwisho anamalizia chakula kwa kugawiwa kiasi chake  na kujulishwa na viongozi wa Kamati za Maafa za vijiji utaratibu mzima wa ugawaji chakula ulivyofanywa hadi chakula kinaisha.

Pamoja na mafanikio katika ugawaji wa chakula cha Msaada cha Ofisi ya Waziri Mkuu zipo changamoto ambazo Kamati za maafa hukabiliana nazo katika kuhakikisha ugawaji chakula cha msaada  unakuwa bora na manufaa kwa walengwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya  ya Hanang Bi. Goody Kapamba  anabainisha  kuwa  uharibifu wa miundo mbinu ya barabara hasa kipindi cha mvua hufanya usambazaji wa chakula kutoka wilayani hadi vijiji husika kuwa mgumu .

 

''Magari yanayobeba chakula hukwama hata zaidi ya siku tatu jambo ambalo hufanya gharama kuwa kubwa ya kusambaza chakula lakini pia kufanya usambazaji wa chakula kutokuwa wa wakati '' alisisitiza Bi Kapamba.

Bi. Kapamba anafafanua kuwa ongezeko la walengwa wa chakula cha msaada ni changamoto pekee , kwani kutokana na muda uliopangwa kugawa chakula unapochelewa kutokana na miundo mbinu kuwa mibovu hufanya  muda ambao chakula kinawafikia walengwa hao  kuongezeka hali ambayo hutengeneza mazingira magumu ya ugawaji wa chakula cha msaada kutoka ofisi ya Waziri Mkuu.

Pamoja na Kamati ya maafa ya wilaya kujipanga vizuri katika ugawaji wa misaada ya chakula lakini ushirikiano mzuri wa kamati za vijiji za maafa zilizo kuwa zikiwashirikisha watendaji wa vijiji na vitongonji ilikuwa ni nguzo pekee ya kuwapa wananchi kushika mpini wa kusamabaza chakula kwa walengwa wa misaada  ya chakula kutoka ofisi ya Waziri Mkuu na hatimaye zoezi la ugawaji chakula kufanikiwa.

"Wananchi wakishirikishwa, Msaada wa chakula utawafikia walengwa".

Mwisho.

 

Page 3 of 3
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved