Logo
Feature Stories

DocumentsDate added

Order by : Name | Date | Hits [ Ascendant ]

Athari za Ukame zinapunguzika jamii husika ikijengewa uwezo

Historia inaonesha kuwa Maafa ya ukame hutokea kila baada ya miaka minne.

Mwaka 1991 – 2001, ukame umetokea mara 8, na kuwaathiri watu 3,629,239.

Maafa ni tukio kubwa ambalo husababisha upotevu wa maisha ya watu, wanyama, majeraha, uharibifu wa mali na mazingira na kuvuruga kabisa mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii iliyoathirika na haiwezi kukabili hali hiyo kwa uwezo wake wenyewe bila msaada toka sehemu tofauti.

Misemo mingi ya waswahili hudhihirisha hali halisi ya maisha ya  jamii yetu kwa kuakisi mambo yaliyomo katika jamii, tukiangalia msemo huu ‘Mcheka kovu ni yule ambaye hajafikwa na jeraha’  kwa mantiki hii ni kuwa suala ambalo umepata athari zake huwezi kudharau kuchukua hatua za haraka, hivyo hivyo katika jitihada za kupunguza Athari za Maafa  zitadhihirika tu kwa jamii ambayo itazitambua athari za maafa.

Ili jamii iweze kushiriki kikamilifu katika kupunguza athari za Maafa, Serikali haina budi kuijengea jamii husika uwezo wa kupunguza athari hizo. Serikali na wadau wa maendeleo wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kukabiliana na maafa, miongoni mwa Maafa hayo ni yanayoikumba nchi yetu ambayo ni Ukame, Mafuriko, Magonjwa ya mlipuko na wadudu waharibifu wa mazao,  Ajali za vyombo vya usafiri, , Matukio ya moto (majumbani, viwandani, majengo ya umma na misituni), Matetemeko ya ardhi na Maporomoko ya ardhi.

Historia inaonesha kuwa Maafa ya ukame hutokea kila baada ya miaka minne. Ndani ya kipindi cha miaka 10 kati ya mwaka 1991 – 2001, ukame umetokea mara 8, na kuwaathiri watu 3,629,239. Maeneo yanayoathiriwa mara kwa mara ni mikoa ya kati ya Dodoma, Singida, na Tabora. Baadhi ya maeneo ya Pwani, Shinyanga, Mwanza na Mara, pia huathiriwa na ukame. Maeneo hayo yana  mvua kidogo, hupata mvua ya kati ya 200 – 600mm kwa mwaka.

Maafa ya Ukame yanaathari kubwa kwa nchi yetu ila iaminike kuwa jamii ikishirikishwa kwa kuelimishwa juu ya athari hizo ni dhahiri jamii yetu itaweza kupunguza athari za maafa hayo. Ni vyema ieleweke kuwa shughuli za kibinadamu zinachangia sana kutokea kwa ukame. Shughuli hizo za kibinadamu ni ni kama vile; ukataji na uchomaji wa miti ovyo, matumizi mabaya ya kemikali, ongezeko la uchafuzi wa hali ya hewa na uharibifu wa vyanzo vya maji.

Tayari serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Idara ya Uratibu Mwa Shughuli za Maafa inaratibu mradi unaojikita kuikwamua jamii kukabiliana  na adui ukame anayehatarisha  maisha ya watu, mimea na wanyama. Mradi  huo wa kuijengea jamii uwezo wa kupunguza athari za maafa kwa mikoa iliyoathirika zaidi na ukame ikiwemo, Shinyanga Vijijini, Kilimanjaro, Pwani, Tabora, Mwanza, Mara, Morogoro na Tanga.

Mratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye pia ni mratibu wa mradi huo Bw. Harrison Chinyuka, anafafanua kuwa Mradi huo ulizinduliwa Wilayani Same mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba, 2013 ukiwa na kauli mbiu inayosema “Athari za Ukame zinapunguzika jamii husika ikijengewa uwezo”, lengo kuu la mradi ni kuisaidia jamii kuwa katika mazingira salama kwa kuzingatia michango inayotolewa ikiwemo kuainisha vihatarishi vya ukame, kuwajengea uwezo wadau wakiwa ni; Vijana, Wanahabari na  Viongozi.

“Mradi huu ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji Wakuu, utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 na tunaamini kuwa utaweza kuijengea jamii husika uwezo wa kukabiliana na athari za maafa yatokanayo na ukame kwa  kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huu ni kutoa mafunzo ya  Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa kwa wataalam wa ngazi ya kata ambao watahusika kuwaelimisha wananchi wa kata zao husika ili kila mwananchi katika kata husika awe na uwezo wa kuainisha vihatarishi vya ukame.” Alisisitiza Chinyuka.

Ni vyema ikaeleweka kuwa Serikali kupitia  Ofisi ya Waziri Mkuu , Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa imekuwa ikifanya juhudi za kukabiliana na maafa ikiwa ni pamoja na kutoa misaada pindi maafa ya ukame yanapotokea. Katika kipindi cha kuanzia Julai, 2009 mpaka Juni 2014, Serikali ilitoa jumla ya Tani 326,459.06 za chakula zilizosambazwa kwa waathirika wa ukame kwenye maeneo yote yaliyokumbwa na ukame. Serikali ilitumia jumla ya Shilingi 21,783,811,446.49/= kwa ajili ya usafirishaji wa chakula hicho kutoka kwenye maghala ya chakula ya NFRA (National Food Reserve Agency). kwenda kwa waathirika wa ukame”.

Lakini pia Serikali  kwa mwaka  2009 ilitoa jumla ya Shilingi bilioni 1.76 kutoka Mfuko wa Maafa kwa ajili ya kununua jumla ya tani 1,091 za mbegu za aina mbalimbali za mazao ya chakula. Wilaya zilizohusika ni Arusha, Monduli, Rombo, Mwanga, Same, Lindi Vijijini, Simanjiro, Bunda, Rorya, Musoma Vijijini, Kwimba, Magu, Misungwi, Ukerewe, Nanyumbu, Bariadi, Kishapu, Shinyanga Vijijini, Singida, Manyoni, Uyui, Tabora Mjini, Bahi, Chamwino, Dodoma Manispaa, Kondoa, Kongwa, Mpwapwa, Kilombero, Kilosa, Morogoro Mjini, Morogoro Vijijini, Mvomero, Tanga, Pangani, Muheza, Mkinga, Korogwe, Lushoto, Handeni na Kilindi.

Katika msingi huo Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Idara ya Uratibu wa Maafa imeamua kuzijengea uwezo  halmashauri husika  kwa kuendesha mafunzo ya kujengea jamii uwezo wa kupunguza athari za maafa ya ukame kwa Mikoa inayoathirika sana na maafa ya ukame ikiwemo, Wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga na Same mkoani Kilimanjaro .

Mratibu wa shughuli za Maafa Wilayani Same Bw. Ally Mngwaya anabainisha kuwa mafunzo ya kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na athari zitokanazo na maafa kwa  wataalam wa ngazi ya kata katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala wa kata ya Hedaru, Makanya na Vunta ni muhimu sana kwa kuwa kupitia wao ndio njia pekee ya kuishirikisha jamii katika juhudi za kupunguza athari za maafa.

“Katika mafunzo haya wataalam wa ngazi ya kata wanapata elimu juu ya matumizi ya taarifa za hali ya hewa, dhana ya maafa, jinsi ya kubaini vihatarishi vya upungufu wa chakula, tathimini ya upungufu wa chakula na mwongozo wa ugawaji wa chakula cha msaada ambapo, vikundi vinavyowezeshwa na mradi huu wa  kuijengea jamii uwezo wa kupunguza athari za maafa watapata kuelimishwa na wataala hawa” alisisitiza Mngwaya

Ieleweke kuwa wataalam katika ngazi ya kata ndio walio karibu na wananchi katika jamii yetu, kimsingi wataalam hawa wanapokuwa na utaalam wa namna ya kukabiliana na athari hizo za ukame ni wazi kuwa jamii ya nchi yetu itaweza kuelimishwa ipasavyo katika kukabiliana na athari za ukame na hatimaye kushiriki kikamilifu katika juhudi zakukabiliana na athari za ukame.

Katika mkoa wa Shinyanga tayari nao umeshanufaika na mradi wa kuzijengea jamii uwezo Kupunguza athari za Ukame. Wataalam katika Sekta ya Kilimo, Mifugo, Afya, Elimu na Utawala  wa kata ya Mwamalasa, Masanga na Langana Wilayani Kishapu watashirikishwa katika Kuijengea Jamii Uwezo wa kupunguza Athari Za Maafa katika kata zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Bi, Jane Mutagurwa anaeleza kuwa, inawezakana kupunguza athari za ukame ikiwa wataalam katika Sekta ya Kilimo, Mifungo, Afya, Elimu na Utawala watashirikishwa katika kuijengea jamii uwezo wa kukabiliana na athari za maafa ya ukame.

“Wilaya yetu ya Kishapu imekuwa ikiathiriwa sana na ukame hali ambayo hupelekea kuwa na upungufu mkubwa  wa chakula lakini kupitia Mradi huu jamii itajengewa uwezo wa kukabili athari hizo, Kwa mfano Maafisa Ugani kwa utaalam wao kutokana na mvua kutonyesha mara kwa mara katika wilaya yetu, kupitia mafunzo haya wataelewa matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa ili waweza kuwashauri wakulima matumizi ya mbegu na pembejeo za kilimo kwa kipindi muafaka cha kulima mazao yanayostahimili ukame, na hatimaye kuepukana athari ya ukame ambayo ni wilaya yetu kuwa na upungufu mkubwa wa chakula” alisema Mutagurwa.

Katika Wilaya ya Kishapu kata tatu za  wilaya hiyo jumla ya vikundi kumi (10) vimenufaika na mradi wa kuijengea jamii uwezo wa kupunguza athari za ukame, ambapo kati ya vikundi hivyo vikundi sita (6) ni vya Wanawake na vikundi vinne (4) ni vya vijana.

Mratibu wa shughuli za maafa Wilayani Kishapu Bw. Ponsian Kuhabwa anaeleza kuwa vikundi vya wilayani kishapu vimewezeshwa kwa kupewa mbuzi  (50) kwa kila kikundi pamoja na kilimo cha bustani.

“Mbuzi 480 tayari zimeshagawiwa kwa vikundi vinne ambapo  kwa kikundi chenye watu kumi kila mwanakikundi amepata mbuzi watano na tayari baadhi ya mbuzi wao wameanza kuzaa  na tayari viriba vya miche 2500 vimegawiwa katika shule za wilaya hii ikiwa lengo ni kufikia miche 5000”.  alisisitiza Kuhabwa

Kuhabwa alifafanua kuwa lengo la mradi huu ni kuhakikisha jamii inashirikishwa kikamilifu katika kupunguza athari za ukame kwani jamii inajengewa uwezo wa kupunguza umasikini kwa kupitia ufugaji wa mbuzi na kilimo cha bustani ambapo wafugaji wamepewa dawa za kuogesha mifugo na vifaa vya kuogesha mifugo pamoja na chanjo za mifugo yao na kwa wanaojihusisha na kilimo nao pembejeo za kilimo kama mbegu, mbolea, madawa ya wadudu, madawa ya magonjwa na pampu za kupulizia dawa .

Pamoja na hayo kama inavyofahamika vijana ni jeshi kubwa katika utendaji na utekelezaji hivyo hawakusahaulika katika kupewa elimu juu ya mbinu za kujikwamua na kuwa na Kilimo endelevu, kujihusisha na upandaji miti. Mradi wa kuijengea jamii uwezo umejikita katika kilimo cha miti kwa kuwashirikisha wanafuzi mashuleni.

Kimsingi inafurahisha ukifika katika baadhi ya shule wilayani kishapu na ukabahatika kukutana na wanafunzi wanaojiita mabibi na mabwana miti. Shule ya Msingi Hindawashi ni shule mojawapo itakayo kufurahisha kwani inao mabwana na mabibi miti takribani 150 wakiwa na wanafuzi wa darasa ltatu hadi la Saba.

Mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi Hindawashi, Nuru Mhangwa anaeleza kwa ujasiri kuwa anajisiskia furaha sana kwa kushiriki katika juhudi za kupunguza athari za ukame kwa kupanda miche ya miti inayastahimili ukame. Nuru anafafanua kuwa miti husabaisha mvua kunyesha katika  eneo husika na hatimaye jamii husika kuweza kupanda mazo ambayo huweza kuisaidia kupata chakula .

Kimsingi Waratibu wa Elimu katika kata na Watendaji wa Kata hawana budi kuhimiza upandaji wa miti katika kata zao, kwakuwa miti ikipandwa kwa wingi inaweza kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya Tabia Nchi ikiwemo ukame, hii ni kuhakikisha mazingira yanakuwa adui wa maafa ya ukame, kwa kuzingatia maafa yana athari kwa makundi yote, watoto, walemavu, vijana, wazee na wanawake.

Bila shaka utaweza kukubaliana nami kuwa kupitia mradi wa kuijengea jamii uwezo wa kukabili athari zitokanazo na ukame wananchi wameshika mpini wa kupunguza athari hizo kwani shughuli za mrdi huo zimeibuliwa na jamii husika ambayo huathiriwa na athari za ukame na hatimaye wanajamii wa kike na kiume vijana kwa wazee wanashiriki kikamilifu katika juhudi za kupunguza thari za maafa na hii inaifanya serikali kushika ncha tu ya juhudi hizo, kwa mantiki hii malengo ya serikali ni kuifanya jamii ya kitanzania yenyewe iwe na uwezo wa kupunguza athari za ukame .

‘Athari za Ukame zinapunguzika jamii husika ikijengewa uwezo’

Mwisho.

Wanawake na Wasichana ni nguvu kwa kinga dhidi ya maafa tuitambue.

Kwa kuanza na Usemi usemao“Ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii nzima”,   bila shaka utajiuliza ni jinsi gani  mwanamke mmoja  aweza kuielimisha jamii nzima, kimsingi usemi huu unalenga kutambua kuwa mwanamke anayo majukumu makubwa katika kuimarisha jamii, bali ni kwa nadra sana kwa jamii husika hutambua Umuhimu wa wanawake na wasichana.

Kwa mantiki hiyo, kwa mwaka huu Mwezi Oktoba tarehe 12, Tanzania na nchi nyingine duniani wanaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Athari za Maafa, Lengo kuu la maadhimisho hayo ni kutambua na kukubali kuwa mamilioni ya Wanawake na Wasichana ndio huifanya jamii kuwa imara katika kinga dhidi ya Maafa na athari za hali ya hewa ili kuweza kuleta manufaa na kulinda maendeleo katika uwekezaji.

Pamoja na kazi yenye mafanikio makubwa ya wanawake ya kupunguza athari za maafa lakini  ni kwa kiwango kidogo mchango wao hutabuliwa kutoonekana katika kufanya maamuzi.  Ujumbe wa Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa wa mwaka huu 2012 umetilia mkazo wa dhati wa kuifahamisha jamii kuwa  mchango wa wanawake katika kuilinda na kuijenga jamii kabla na  baada ya Maafa huwa hautambuliwi, hivyo jamii husika haina budi kutambua mchango wao.

Ni wazi kuwa sababu kuu inayosababisha maafa kutokea ni kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu hatua za kuchukua, kuzuia, kujiandaa au kupunguza athari za  maafa. Kwa kuwa msingi wa jamii ni mwanamke, hivyo mwanamke akielimishwa ni dhahiri kuwa jamii nzima inaweza kuwa na uelewa mkubwa wa kujiandaa, kukabili na kupunguza athari za maafa.

Kabla hatujaona nguvu ya mwanamke katika kinga dhidi ya maafa, tuelewe kuwa kutokana na jamii kutokuwa na ufahamu wa kutosha jamii hujiingiza katika hatari nyingine zinazosababisha maafa kama vile; kuwa karibu na eneo la janga au kukimbilia kwenye maeneo ya hatari, uharibifu wa mazingira, kuongezeka kwa idadi ya watu hususan kwenye maeneo yasiyofaa kwa makazi ya binadamu, kupanuka kwa miji bila kufuata sheria za mipango miji.

Ningependa ifahamike kuwa Maafa ni matokeo ya janga ambalo  huathiri kwa kiwango kikubwa mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii kwa kusababisha vifo, majeraha, upotevu au uharibifu mkubwa wa mali au mazingira  ambao jamii iliyoathirika haiwezi kukabili kwa uwezo au rasilimali zake bila msaada kutoka nje ya jamii hiyo.

Ukizungumzia athari za maafa duniani, akilli ya mtu itakumbuka kwa haraka  maafa ya miaka ya hivi karibuni ya tetemeko kubwa la ardhi lililoambatana na mawimbi ya bahari maarufu kama TSUNAMI katika miji ya SENDAI na FUKUSHIMA nchini JAPAN yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali,  makazi ya watu na mali nyingi.

Kwa hapa  nyumbani watanzania tumeshuhudia pia maafa mbalimbali. Maafa hayo  ni pamoja na yale ya milipuko ya mabomu huko Mbagala mwaka 2008 na Gongo la Mboto mwaka 2009 Jijini Dar es Salaam ; mafuriko mwaka 2011 ya Jijini Dar es Salaam; kuzama kwa meli Mv Spice Islender mwaka 2011, MV SKAGIT mwaka 2012 na milipuko ya magonjwa ya kipindupindu pamoja na moto viwandani, ofisini na kwenye nyumba za kuishi.  Athari za maafa hayo zimekuwa ni kubwa kutokana na kutokuchukua hatua za tahadhari mapema.

Utajiuliza kwa nini maadhimisho hayo yalenge kuthibitisha vitendo na jitihada wafanyazo  Wanawake na Wasichana kuwa ni nguvu kwa kinga dhidi ya   maafa? Jibu li wazi kuwa sote ni mashahidi kuwa mwanamke ni mtu muhimu duniani,  ukitoa  dhima kubwa aliyonayo ya malezi ya familia lakini ndiye kinara  na chachu  wa maendeleo ya familia, jamii na pia ndiye mjenzi wa amani katika familia na jamii yake.

Jumuiya ya Kimataifa tayari imetambua nafasi na dhamana ya wanawake katika kulinda na kudumisha misingi ya amani duniani na inaendelea kuthamini mchango makini uliotolewa na wanawake wawili kutoka Liberia: Hawa ni Rais Elle Johnson Sirleaf na Bibi Leymah Gbowee pamoja na Tawwakkol Karman, mwanamke kutoka Yemen. Hawa ndio waliojinyakulia tuzo ya Amani kwa Mwaka 2011.

Aidha hata yale mafanikio  wanayopata wanaume utakuta kuwepo kwa mchango wa mwanamke. Lakini kutokana na kutokuwepo kwa uwiano na usawa wa jinsia kama ilivyo sasa katika jumuiya, kunaizuia jamii kutambua uwezo wao  kamili katika shughuli zote zinazohusu maendeleo ya uchumi, jamii na maeneo ya siasa hatimaye juhudi mbali mbali za kimataifa  za kuleta maendeleo duniani zimekuwa zikidolola.

Kwa mantiki hiyo, Ili kupunguza athari za maafa duniani, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ya Mkakati wa Kupunguza Athari za Maafa (United Nations Secretariet for International Strategy for Disaster Reduction). Kwa mwaka 2012, Sekretarieti hiyo imechagua kaulimbiu ya Kampeni ya Dunia kuwa ni “Wanawake na Wasichana – Nguvu isiyoonekana kwa kinga dhidi ya Maafa”.

Kauli mbiu hii inalenga kufafanua kuwa uwezo wa wanawake na wasichana katika kutoa mchango wao wa kupunguza athari za maafa hauonekani kwa sababu za kutoshirikishwa katika kutoa maamuzi katika Upunguzaji Athari za maafa katika ngazi za uongozi, mpangilio wa progamu na uelewa mdogo wa usawa wa kijinsia, hatimaye nguvu ya wanawake katika kinga dhidi ya maafa haionekani.

Serikali kwa kutambua hilo imefanikiwa kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbali mbali za uongozi wa kisiasa na kiutendaji. Mathalan,Wabunge Wanawake wameongezeka kutoka asilimia 11 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 36 mwaka 2011.  Kwa upande wa Mawaziri wameongezeka kutoka asilimia 12 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 27.5 mwaka 2011.

Tukizingatia ushiriki huo na mfumo wetu wa kukabiliana na maafa ambao una Kamati za Maafa kwenye ngazi ya mkoa, wilaya hadi kijiji ambazo zina majukumu ya kusimamia masuala ya maafa katika maeneo yao. Hivyo Wanawake na Wasichana wanaweza kushiriki kikamilifu katika hatua zote za Upunguzaji Athari za maafa.

Katika ngazi ya  uongozi wa kiutendaji Wakurungezi wa Halmashauri wameongezeka pia kutoka asilimia 6 mwaka 1991 hadi kufikia asilimia 26 mwaka 2011 wakati  Majaji wanawake wameongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2011, hivyo wanawake wa Tanzania wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wao katika kutoa maamuzi ya Upunguzaji Athari za maafa

Ieleweke kuwa Asilimia 52% ya watu Duniani ni Wanawake na Wasichina, hivyo utaelewa kuwa nusu ya watu duniani ni wanawake na wasichana ndio maana Kampeni hii ya Dunia inayoendelea hivi sasa inajikita katika kujiandaa na maafa ili kukinga au kupunguza athari za maafa kwa kuhakikisha nguvu ya wanawake na Wasichana katika kukinga na kukabiliana na maafa inatambuliwa na jamii na kwakuwa wao ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa maafa.

Hili lilijidhihirisha wakati mvua kubwa zilizonyesha usiku wa tarehe 19 Desemba, 2011 hadi tarehe 22 Desemba, 2011 Mkoa wa Dar es Salaam Kutokana na mafuriko yaliyotokea, nyumba nyingi zilizo mabondeni ziliathirika kwa kuzingirwa na mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kutokea kwa miaka mingi na kusababisha watu zaidi ya 5000 kuondoka katika makazi yao. Watu 40 (wanawake 10 na wanaume 30) walipoteza maisha.

Kampeni hii pia inajikita katika kuongeza uelewa wa  wananchi na serikali katika ngazi zote juu ya umuhimu wa kujikinga na kupunguza athari za maafa kwa kuwawezesha Wanawake na Wasichana katika kuchangia kuleta maendeleo endelevu kupitia Upunguzaji wa Athari za Maafa, hususani katika nyanja za  Mazingira na Usimamizi wa Mali asili, Utawala, Mipango miji, Matumizi bora ya ardhi na mipango ya kijamii na kiuchumi zikiwa ni mihimili ya kinga dhidi ya  maafa.

Nchini Tanzania inakadiriwa kwamba wanawake hasa wa vijijini wanatoa asilimia 80 ya wafanyakazi katika eneo la kijiji na hivyo kutoa asilimia 60 ya chakula kinachozalishwa.  Ingawa wanawake ndiyo wazalishaji wakubwa wa mazao ya biashara, mazingira hayawaruhusu kumiliki mali zao. Pia jamii haitambui nguvu ya mwanamke anayo itumia kuikinga na maafa ya njaa.

Hii inadhahirisha kuwa mlimaji akiwa mmoja (mwanamke) na walaji wakawa wengi jamii hiyo ni vigumu kukwepa janga la njaa na hasa jamii hiyo ikikumbwa na ukame, matokeo yake Serikali huchukua hatua za ziada  za kuipeleka chakula cha msaada kwa jamii yenye upungufu wa chakula.

Mfano hai ni kutokana na athari ya  ukame ulioikumba  nchi yetu mwaka 2009 na hatimaye kuifanya baadhi ya mikoa  na kaya zake kuathiriwa na njaa , Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa chakula cha msaada kwa Mikoa 15 kwa ajili ya kusambazwa katika Wilaya 59 za Mikoa hiyo, iliyokuwa na upungufu mkubwa wa chakula. Chakula hicho kilisambazwa kati ya mwezi Februari 2009 na Februari 2010.

Kama kampeni hii inavyotaka kuwa Wanawake na Wasichana wawezeshwe katika Matumizi bora ya ardhi na mipango ya kijamii na kiuchumi, tayari Serikali imepitisha sheria kadhaa katika kutoa upendeleo kwa wanawake kwa mfano “Sexual Offences Special Provision Act of 1998, Land Law Act of 1999 na Village Land Act of 1999.

Sheria hiyo ya kwanza inawalinda wanawake, wasichana na watoto kutokana na kunyanyaswa kijinsia na matendo mabaya.  Sheria mbili za mwisho zinahuisha na kufuta sheria za awali zinazohusu masuala ya ardhi na hivyo kuwawezesha wanawake kufaidi haki sawa na wanaume za kuweza  kupata, kumiliki na kudhibiti ardhi.

Aidha Kampeni hii inasisitiza kuwa ili nguvu ya mwanamke katika kinga dhidi ya maafa ionekane  na jamii husika iweze kupata matokeo mazuri ya Upunguzaji wa Athari za Maafa ni vyema Wanawake na Wasichana wakashirikishwa katika mikakati ya mabadiliko ya hali ya hewa ili kuweza kuleta mafanikio katika masuala ya Maafa na lazima wahususishwe katika sera, mipango na utekelezaji wa maandalizi hayo.

Mshindi wa tuzo ya Amani kwa Mwaka 1984, Desmond Tutu alipata kunena kuwa “Kama tunataka kuona maendeleo ya kweli Duniani, basi Uwekezaji mzuri ni Wanawake”

Kimsingi Tutu alikuwa akikisitiza wanawake wasibaguliwe katika shughuli za maendeleo, ambapo kampeni hii inataahadharisha kuwa kutokuwepo kwa uwiano na usawa wa jinsia katika jamii ni hatari sana pindi yanapotokea majanga kwa kuwa jamii hukosa uwezo wa kuwashirikisha watu wote katika hatua za kukabili maafa.

Serikali ya Tanzania tayari kauli ya Tutu ilishaitekeleza kwa Mwaka 2009, kupitia  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kuratibu uanzishizwaji wa Benki ya Wanawake Tanzania.  Benki hii ilizinduliwa rasmi tarehe 4 Septemba 2009. Hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2011 jumla ya akaunti zilizokuwa zimefunguliwa zilikuwa 18,824 ambapo akaunti 14,787 sawa na asilimia 78.6 ni za wanawake, akaunti 3,578 sawa na asilimia 21.4 ni za wanaume.

Ifahamike kuwa Uwiano sawa na jinsia huanza na elimu, kama wasichana na wavulana watahusishwa kikamilifu katika maisha ya kila siku, katika ukuaji wa vijana wa kike na kiume hii itasaidia kuondoa vikwazo vya wasichana kushiriki katika elimu ambapo hufundishwa ni namna gani wanaweza kujiandaa, kukabiliana na kupunguza athari za maafa. Kutokana na mazingira hayo Wizara imefanikiwa kueneza uelewa wa wananchi.

Kwa hapa Tanzania Matokeo ya uelewa huo ni pamoja na kuongezeka kwa uwiano wa wavulana na wasichana katika shule za msingi na sekondari ambao umefikia asilimia 50 kwa 50.

Ofisi ya Waziri Mkuu,  Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Mamlaka ya Elimu Tanzania  tayari wameshaanza mchakato wa kuingiza masuala ya maafa katika mitaala ya Elimu ya msingi na Sekondari, ikiwa ni nia ya Serikali ya kuongeza uelewa wa masuala ya maafa kwa vijana wa kiume na kike ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchukua hatua za kuzuia, kujiandaa au kupunguza athari za maafa.

Dira ya Maendeleo ya 2025 ya Tanzania inalengo la kuwapatia watu wake hali ya juu ya maisha, kufanikiwa katika kupata utawala bora wa kuheshimu sheria pamoja na kuendeleza uchumi imara na wa ushindani.  Ili kufanikiwa kuleta usawa wa jinsia na kuwapa uwezo wanawake katika maeneo ya jamii, uchumi, uhusiano wa siasa na utamaduni lazima yatiliwe maanani.

Kwa kuwa jinsia ni mkondo mkuu ambao vipengele vyote vya maendeleo hupita ili kuimarisha uchumi wa Taifa, siasa na masuala ya jamii na utamaduni. Hatuna budi kuwashirikisha na kutambua michango ya wananwake na Wasichana katika kuzuia, kujiandaa au kupunguza athari za maafa na hatimaye tutaewza kupata Usalama wa nchi yetu dhidi ya maafa.

WAWEZESHE WANAWAKE NA WASICHANA KWA USALAMA WA KESHO.

Mwisho.

 

 

 

 

 

Wahitimu vyuo vikuu wanaweza kutumia  taaluma zao kutengeneza ajira

“Taasisi yenu iwe mfano wa kuigwa na vijana wengine wahitimu katika fani mbalimbali kuona namna ambayo wanaweza kutumia elimu na utaalamu wanaoupata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kuweka mipango madhubuti ya kujiajiri”  anasisitiza Nagu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk. Mary Nagu (Mb) alilisitiza hayo hivi karibuni wakati alipoongoza matembezi ya “Saidia Mama Mjamzito Kujifungua Salama” yaliyoandaliwa na Taasisi ya Madaktari wahitimu wa Vyuo Vikuu Tanzania (TPHI) yaliyoanzia katika hospitali ya Manispaa ya Temeke mpaka Ofisi za Manisipaa hiyo, Jijini Dar es Salaam.

Ni dhahiri kuwa  maendeleo ya elimu  nchini yamechochea kuongezeka kwa vyuo vikuu hapa nchini na idadi ya wahitimu katika vyuo hivyo , ikiwa ni ishara ya uthubutu na utayari wa serikali katika kuwekeza na kusimamia sekta ya elimu hapa nchini,

Lakini bado idadi ndogo ya wahitimu wanaoweza kupata ajira  katika sekta ya umma na binafsi kutokana na ufinyu wa nafasi hizo.

Ni jambo la kuzingatia kuwa Fani ya Udaktari ni fani ambayo inauhakika wa ajira lakini pamoja na kulitambua hilo wametambua kuwa njia bora ya kujikwamua na kujiwezesha kujiajiri ni kuazisha kikundi chenye kutumia taaluma yaolakini pia ikiwa ni sehemu ya chachu ya kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto zinazowakabili mama wajawazito hapa nchini.

“Kwa niaba ya serikali napenda kuwapongeza Taasisi ya Madaktari Wahitimu wa Vyuo Vikuu Tanzania kwa kuwa chachu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika  kuwezesha vijana kujiajiri na napenda kuwahakikishia kuwa serikali inatambua mchango wenu wa kuunga mkono serikali katika kuboresha huduma za afya kwa akina mama na watoto”  alisema Nagu

Wahitimu katika fani mbalimbali hawanabudi kuona namna ambayo wanaweza kutumia elimu na utaalamu wanaoupata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kuweka mipango madhubuti ya kujiajiri kwa kujitoa kwa dhati katika kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwa upendo na hatimaye kupunguza idadi kubwa ya kukosa ajira.

Aidha  Nagu anafafanua kuwa pamoja na kuwa Taasisi hiyo kuwa  inatengeneza ajira kwa vijana jambo kubwa  inalolitekeleza vizuri ni kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha afya ya Mama mjamzito hapa nchini ,mpango wenye lengo la kupunguza  vifo kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Hayumukiniki kuwa zipo changamoto kwa wahitimu katika kutumia taaluma zao kujiajiri lakini kwa nia anayo idhihirisha Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji na Uwezeshaji ni wazi kuwa wahitimu watakao thubutu wanaweza kufanikiwa kujiajiri lakini pia taaluma yao kuweza kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Pamoja na juhudi zinazofanywa na TPHI lakini pia zipo changamoto wanazo kabiliana nazao ambapo  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Madaktari Wahitimu Vyuo vikuu Tanzania, Dk. Teresphory Kyaruzi anabaibisha  changamoto kubwa waliyonayo ni jinsi ya kuwapelekea huduma wanachi kwa wakati na kwa gharama wanazoweza kuzimudu.

“Ukubwa wa changamoto hii unatokana na jinsi ya kuwafikia wananchi hasa akina mama wajawazito na watoto walioko vijijini na wanao ishi kwenye mazingira magumu.” Alisisitiza  Kyaruzi .

Takwimu zinabainisha kuwa Katika mwaka 2010 kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupungua kwa vifo vya mama wajawazito na wototo kufikia 454 kati ya watoto 1000 kutoka 578 kwa mwaka 2005.

Katika kusisitiza hili ni vyema tukatambua kuwa kidole kimoja hakivunji chawa hivy o hata wahitimu wahitimu katika fani mbalimbali katika umoja wao kwa kuzingatia elimu na utaalamu wanaoupata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kuweka mipango madhubuti ya kujiajiri wanaweza kupunguza matatizo yanayo ikabili wananchi.

Serikali katika kutekeleza hili tayari imeshaanza kutekeleza kwa vitendo kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia katika Mpango wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na Kuongeza ajira (JK Fund), Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) na Mfuko wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF).

Ni dhahiri kuwa tukishirikiana na Mifuko ya serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tunaweza kuutokomeza umasikini kwa kujiajiri wenyewe lakini pia kutumia fani zetu kwa kutatua matatizo yanayo ikabili jamii inayotuzunguka.

Mwisho.

Utekelezaji wa mikakati madhubuti utapunguza athari za maafa nchini

YANAPOTOKEA maafa mbalimbali nchini, njaa, magonjwa na vifo huweza kutokea kwa mtu yeyote na mara nyingine huwa ni vigumu kuyazuia  kwani hutokea katika mazingira yasiyotarajiwa.

Hivyo serikali za nchi mbalimbali duniani kwa kushirikiana na wadau tofauti wamekuwa hawana budi kuwekeza fedha zitakazotumika mara hali hiyo itakapojitokeza ili angalau kukabiliana nayo lengo likiwa ni kupunguza maafa.

Nchini tayari tumekwishashuhudia kutokea kwa maafa mbalimbali yaliyosababaishwa na maporomoko ya ardhi, vimbunga, mafuriko, Tsunami, tufani iliyoambatana na dhoruba kali, moto na hata ajali za barabarani.

Hivi karibuni jamii imejionea miji yetu ikikumbwa na maafa mbalimbali yakiwemo maafa ya milipuko ya mabomu ya Mbagala Dar es Salaam, mafuriko ya mvua katika maeneo mbalimbali ya miji yetu ambapo athari kubwa zaidi ilitokea mjini Kilosa mwishoni mwa mwaka 2009 hadi mwanzoni mwa mwaka huu.

Athari za maafa haya wakati mwingine zimekuwa kubwa kutokana na kutokuchukua hatua za tahadhari mapema. Matokeo yake ni serikali kuingia gharama kubwa kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa.

Kutokana na hilo, katika kufikia malengo ya kukabiliana na matukio hayo dunia iliona kuna sababu kwa kila nchi ulimwenguni kuifanya Oktoba 13, 2010, kuwa ni siku ya Kimataifa ya Upunguzaji Athari za Maafa (International Day for Disaster Reduction). Siku hii huadhimishwa Jumatano ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka.

Siku hii iliwekwa maalum ili kuamsha uelewa wa wananchi kuzuia na kupunguza uwezekano wa athari za maafa yanayoweza kutokea na kuwafanya wawe tayari wakati wote kujihami na maafa.

Uhalisia ni kwamba maafa yanapotokea huathiri maisha ya watu, kuharibu mali na mazingira. Mbali na hayo hayachagui yanapotokea iwe vijijini au mijini, kutokana na hilo  ili kuweza kupunguza athari zinazoletwa na maafa ni lazima kuchua hatua za tahadhari mapema.

Kila mwaka Baraza la Umoja wa Mataifa hutoa kauli mbiu kwa wananchi kwa madhumuni ya kusisitiza mambo ya kuzingatiwa katika mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2010 ni ‘Kukinga miji yetu dhidi ya Maafa’ (Making Cities Resillient)

Hata hivyo yanapotolewa matamko mbalimbali na serikali juu ya kujikinga na maafa jamii hujiuliza kama kweli maafa yanaweza kukingwa. Hii inatokana na ukweli kwamba maafa hutokea bila kutarajiwa.

Katika tamko la mwaka huu alilolitoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda Oktoba 13 mwaka huu amesema, athari za maafa huweza kupunguzwa kama hatua za tahadhari zitachukuliwa wakati wote na pia kuweza kuimarisha Miji nchini.

Vilevile miji inaweza kukingwa na maafa kama tutachukua hatua za kuboresha miundombinu ya miji na vijiji kama kutengeza mifereji bora ya kupitisha maji, kuwa na mifumo bora ya kupitisha maji safi na maji taka hii itasaidia kupunguza maafa na miji itakuwa salama pindi maafa yatakapotokea.

Kwani baadhi ya maafa maporomoko ya ardhi yanapotokea kama ilivyokuwa Wilayani Same eneo la Same miamba mawe, ardhi vilisogea kwenye mtelemko wa mlimani na kusukuma miti, nyumba na hatimaye kusababisha vifo vya watu takribani 21. Katika Alpi za Ulaya takriban watu 100 hufariki kila mwaka kutokana na maporomoko ya ardhi.

Chanzo kingine cha maafa ni Kimbunga ambayo ni dhoruba kali inayoanza juu ya bahari katika maeneo ya tropiki yenye upepo mwenye kasi ya zaidi ya 117 kilometa kwa saa.

Mara nyingine huanza juu ya bahari ya kitropiki penye maji yenye halijoto juu ya 26 °C. Hewa joto yenye mvuke nyingi inaanza kupanda juu na kuzunguka. Mzunguko huo unaongezeka kasi kuwa dhoruba. Kasi ikifikia mwendo wa 117 kilometa kwa saa na  kusababisha hasara kubwa ikigusa meli baharini na zaidi mwambaoni inapofikia nchi kavu au visiwa.

 

Hatari zake zingine ni kasi ya upepo pamoja na kiasi kikubwa cha mvua. Kasi ya upepo inaweza kuinua vitu vizito kama miti, paa za nyumba au magari na kuvirusha mbali. Watu huuawa na mali kuharibiwa. Uwingi wa mvua husababisha mafuriko.

Mafuriko ni hali ya kuwa na maji mengi yanayofunika nchi kavu pasipo na maji kwa kawaida. Hivyo yanapotokea popote baada ya mvua kali maji mengi yasiyo na njia hutawanyika kwenda kusikotarajiwa na kuleta madhara kwenye mashamba na hata kuharibu miundombinu ya barabara ama reli kama ilivyotokea wilayani Kilosa mwaka huu.

Mafuriko mara nyingi ni hatari kwa binadamu huleta hatari kwa maisha, mali na nyumba. Njia za kujiokoa ni pamoja na kuhama haraka penye miinuko au nchi ya juu zaidi. Nchini janga hilo ndilo limekuwa likiathiri sana jamii ya Watanzania kutokana na wengi kuishi sehemu za mabondeni ambako maji hukimbilia.

Pia maafa mengine husababishwa na tetemeko la ardhi ambalo kwa Tanzania limekuwa aliathiri sana linapotokea. Hili hutokea baada ya mshtuko wa ghafla wa chini ya ardhi. Limekuwa likitokea mara kwa mara lakini idadi kubwa ni hafifu mno haisikiki na wanadamu ila tu inapimwa na mitambo ya wataalamu.

Athari zingine za matetemeko ya ardhi ni kuweza kusababisha uharibifu mkubwa na vifo hasa kutokana na majengo yanayoanguka. Kwa upande wa baharini tetemeko mara nyingi husababisha tsunami.

Tsunami ambalo ni neno linapotokana na lugha ya Kijapani likimaanisha bandari ya mawimbi kutokea na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Wakati mwingine inaweza kutokea bila kuleta madhara yoyote.

Nchini lilipotokea Desemba 26, 2004 kwenye ufukwe wa Coco Beach jijini jumla ya watu saba walifariki wakati karibu na pembe ya kaskazini ya Sumatra kwenye mstari ambako bamba la Uhindi linajisukuma chini ya bamba ndogo la Burma lililoua takriban watu 275,000.

Kutokana na hilo ili miji iweze kushiriki kikamilifu katika kupunguza athari za maafa ni lazima iwe na mifumo mizuri ya kutoa tahadhari za awali, uwezo wa kukabili maafa pale yanapotokea na kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika tamko lake aliitaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni miji ambayo wananchi wanashiriki kupanga na kuamua masuala ya mji husika kwa kushirikiana uongozi wa serikali za mitaa kulingana na rasilmali walizonazo.

Mifumo mingine ni ule wa uongozi makini na wenye kuwajibika na wenye mipango miji endelevu yenye kukubalika na makundi yote, mji ambao maafa yanaweza kuzuiwa kwa sababu wakazi wanaishi kwenye makazi yenye miundombinu imara kama vile umeme, maji ya bomba, mifereji ya maji safi na maji taka, barabara zinazopitika majira yote na huduma za jamii ambazo ni za uhakika.

Alizitaja huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, uzoaji takataka na upatikanaji wa huduma za dharura. Pia iwe ni miji ambayo watu wake wanaishi kwenye majengo yaliyofuata vipimo sahihi na ambayo hayakujengwa kwenye mabonde au miinuko kwa sababu ya ukosefu wa maeneo ya makazi.

Hivyo kwa wadau wote wa udhibiti maafa hawana budi kuchukua hatua madhubuti kwa kuifanya miji yao kuwa inayoelewa madhara ya maafa kwa kuandaa taarifa za kutosha kuhusu hatari hizo na kuwaelimisha wananchi wake kwamba ni wakati gani wanajiweka kwenye hatari hizo na akina nani wanaweza kudhurika.

Masuala mengine ni kujihami na maafa endapo yatatokea, kutenga kiasi cha rasilmali zake ili kujihami na maafa, kuweza  kukarabati kwa haraka na kurejesha mapema huduma za jamii na shughuli za kiuchumi endapo zitakuwa zimeharibiwa na maafa, kutambua kwamba yote yaliyotajwa hapo juu yanategemea uwezo wao wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hivyo tamko la mwaka huu linabainisha pia kuwa na kampeni ya miaka miwili kwa kila mji duniani kujiwekea malengo ya kujihami, kukabiliana na maafa na kuwa tayari kurekebisha madhara yatakayoletwa na maafa ili maisha ya watu yarudie katika usalama wa awali.

Serikali tayari kwa upande wake kama alivyosema Pinda tayari imeweka rasilimali na miundombinu mbalimbali katika miji na majiji nchini kama hatua za kuboresha makazi huku ikitia maanani kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.

Aidha kutekelezwa kwa kampeni hii kutasaidia kuepukwa kwa majanga ya moto yanayoendelea kutokea kote nchini ukiachia mbali ule lililojitokeza kwenye jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambao uliteketeza jengo zima, huku askari wa Kikosi cha Zimamoto, polisi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwa wameduwaa, wasijue la kufanya.

Kampeni hii ya miaka miwili kuanzia mwaka 2010/11 ina lengo la kuorodhesha walau viongozi wa serikali za mitaa wapatao 1,000 ambao wako tayari kuwekeza rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji ya upunguzaji athari za maafa ikiwemo kuboresha mipango miji, miundombinu na ujenzi salama; kuimarisha mifereji ya maji machafu ili kupunguza mafuriko na magonjwa ya mlipuko; kuweka mifumo ya kubaini maafa kabla hayajatokea na kutoa mafunzo ya kujihami au kujihadhari na maafa kwa wananchi.

Hivyo tungependa kuishauri Serikali na kuiasa kwamba wakati sasa umefika wa kubuni mikakati endelevu ya kupambana na majanga ya moto katika nchi yetu. Kwa hali ilivyo hivi sasa, tunaweza kusema kwamba maafa sasa yamekuwa matukio ya kawaida na ahadi za viongozi kuyamaliza zimekuwa zikichukuliwa na wananchi kama ngonjera zisizokwisha, kutokana na serikali kuonesha wazi kwamba haina ujasiri wa  kupambana nayo.

Baadhi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na serikali ni kuhakikishe kwamba kitengo cha Maafa kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu siyo tu kipewe vifaa, bali pia kipandishwe hadhi kama taasisi inayojitegemea ili kiondokane na urasimu usiokuwa wa lazima.

Mwisho.

 

 

 

 

 

Mkojo wa binadamu nao umeweza kuzalisha Magunia 25 ya mahindi katika Shamba la ekari moja  kwa msimu sawa na mbolea nyingine.

Matumizi yake yafanya  Chakula cha msaada kuwa historia katika kijiji cha Mbola.

Ongezeko la chakula laongeza pia ufaulu wa wanafunzi wa shule za  msingi kwa kupata chakula cha mchana.

“Kabla ya kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu wa  ugani wa mradi wa Vijiji vya Milenia Mbola,  katika shamba langu la ekari  moja nilikuwa navuna magunia 5 hadi 6 ya mahindi, lakini baada ya kufundishwa na wataalamu hao jinsi ya kutumia  mbolea ya mkojo wa binadamu, mbegu bora , kupanda kwa nafasi, kulima na kupalilia kwa wakati  nimeweza kuvuna magunia 25 ya mahindi  katika ekari  moja.”   Anasema Bi. Paskazia Petro.

Bi. Paskazia Petro ni miongoni mwa wakulima wengi wa kijiji cha Milenia Mbola waliojikwamua kutokana na kujishughulisha na Kilimo. Kufuatia kuongezeka kwa mavuno kutoka magunia 5 ya mahindi katika ekari moja hadi kufikia  magunia 25 ya mahindi katika ekari hiyo  moja,  chakula kimekuwa cha kutosha  na mahindi mengine yameweza kuuzwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya msingi ya familia.

Mratibu wa Sayansi wa Mradi wa Vijiji vya Milenia Mbola Dk. Gerson Nyadzi anabainisha kuwa awali  wakazi wa vijiji vya milenia Mbola kila mwaka walikuwa wanapata msaada wa chakula kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu  ili waweze kuikabili njaa iliyowakabili lakini tangu mwaka 2006 Mradi ulipoanza kufanya kazi katika vijiji hivyo hakuna msaada wa chakula unaohitajika tena.

“Kabla ya Mradi wa Vijiji vya Milenia Mbola haujaanza kutekelezwa  katika vijiji vya Mbola uzalishaji wa mazao ya chakula ulikuwa  kidogo, ambapo ilikuwa ni chini ya tani moja kwa ekari, lakini baada ya wananchi kupata huduma za ugani za kisayansi, kiwango cha uzalishaji wa mazao  ya chakula umeongezeka kutoka tani tano kwa ekari moja.” Anaeleza Dk.  Nyadzi.

 

Ni mtego wa wazi kuwa ardhi mbaya inatoa mavuno duni na mavuno duni yanafanya kaya kutokuwa na uwezo wa kuboresha ardhi na hatimaye kukumbwa na njaa. Ulimaji na mavuno ya huko nyuma ulichosha ardhi kwa sababu wakulima wa Mbola hawakuweza kumudu kupata kununua mbolea za viwandani ama za mboji. Lakini kwa msaada mdogo wa mbolea za kukuzia na matumizi ya  mbolea ya mkojo wa binadamu, Mbola imeanza kupata mafanikio na kuanza kuongeza uwezo kukabili umaskini.

“Wanavijiji wa  Mbola wameweza  kuelewa nini maana ya Kilimo bora kwa kulima kwa nafasi, kuandaa mashamba na mbegu kwa wakati na matumizi ya pembejeo. Mbolea ya mkojo wa binadamu nayo imeongeza uzalishaji na ni rahisi kupatikana na kutumiwa na mkulima wa kawaida, kwani katika kaya  nyingi za Kitanzania zina watu si chini ya watano ambapo binadamu mmoja kwa mwaka anaweza kuzalisha kg 10 za  mbolea ya mkojo wa binadamu hivyo kaya yenye watu 10 inaweza kuzalisha kg 50 za mbolea hiyo”  Anasisitiza Dk. Nyadzi .

Dk. Nyadzi  anafafanua kuwa mtaalamu kutoka Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani Prof. Ray Well ndiye aliyewaeleza wananchi wa Vijiji vya Milenia Mbola kuwa hata wao binadamu wanayo mbolea ambayo ni mkojo wao wenyewe kwani kwa kuichanganya na maji ni mbolea nzuri kwa kupandia mahindi.

“Prof. Ray Well kutoka Chuo Kikuu cha Columbia aliwaelimisha  kuwa matumizi ya mbolea ya mkojo wa binadamu ni rahisi kwa mkulima wa kawaida kwani lita 5 za mkojo wa binadamu zinachanganywa katika lita 15 za maji, ama mkojo na maji vinachanganywa katika uwiano wa 1- 4  ambapo mkojo uwiano wake ni 1 na maji ni 4.” anafafanua  Dk. Nyadzi

Swali la kujiuliza ni je, utawezaje kuhifadhi  mkojo wa binadamu  mpaka kipindi cha msimu wa kulima shamba ili uweze kupanda mazao shamba ulilo liandaa katika wakati mwafaka?

Mkulima wa kijiji cha Milenia Mbola ambaye pia amepewa cheti cha mkulima bora na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh: Jakaya Kikwete Bi. Paskazia Petro anaelezea kuwa baada ya kuuchanganya mkojo na maji huwa anamwagilia katika shamba lake ambapo ikifika kipindi cha msimu tayari ardhi inakuwa imesharutubishwa na mbolea ya mkojo wa binadamu.

“Ninapo ukusanya mkojo nauweka  katika dumu langu la lita ishirini na ninauchanganya kwa viwango nilivyo elekezwa na wataalamu wa kilimo na kunyunyizia katika kila mche lita moja. Msimu uliopita nilitumia  mbolea tofauti katika matuta manne ya mahindi, ambapo tuta la kwanza niliweka mbolea aina ya CAN, tuta la pili nikaweka UREA, tuta la tatu  nikaweka DAP na la nne nikaweka mkojo wa binadamu, mbolea zote zilichaji (akimaanisha kufanya kazi) lakini Mkojo wa binadamu ulichaji zaidi.”  Anafafanua Bi. Paskazia.

Mratibu wa Sayansi wa Mradi wa Vijiji vya Milenia Mbola Dkt. Gerson Nyadzi anafafanua kuwa  kutokana na ongezeko la uzalishaji katika Vijiji vya Milenia Mbola, shule zote za msingi  zilizopo katika Vijiji vya Milenia Mbola wanafunzi wanapata chakula cha mchana shuleni.

“Tulipoanza Mradi huu mwaka 2006 tuliwawezesha wananchi katika vijiji vyote 17 vya milenia  kwa kuwapa pembejeo  ambapo kila kaya iliyopata pembejeo ilitakiwa kuchangia magunia mawili ya mahindi shuleni ambapo  tulifanikiwa kukusanya magunia elfu kumi kwa vijiji vyote 17 vya milenia, hivyo mwezi Januari 2008 wanafunzi walianza kula chakula cha mchana shuleni.” Anasema Dk. Nyadzi.

Hili suala la wazazi kuchangia chakula cha mchana kwa shule za msingi Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete analiunga mkono na anaamini kuwa ndilo suluhisho la wanafunzi kupata chakula cha  mchana shuleni kwa kubainisha kuwa  Serikali haina uwezo wa kuigharamikia kila shule ya msingi  nchini kwa chakula.

Mnamo tarehe 15 June 2010 wajumbe wa Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walimtembelea  Ikulu  Rais wa Jamhuri wa Muungano Tanzania Mh: Jakaya Kikwete, ambapo watoto hao  walipata fursa ya kumuuliza maswali  Mh; Rais maswali mbalimbali yanayowahusu watoto  wa Tanzania.

Swali mojawapo miongoni mwa maswali mengi yaliyoulizwa na wajumbe wa Baraza la Watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni lile lililoulizwa na mwakilishi wa watoto kutoka katika kituo cha kulea watoto yatima cha KIWOHEDE, Resta Philipo aliyetaka kujua Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wanafunzi wa shule za msingi chakula cha mchana shuleni.

Mhe: Rais Kikwete  akijibu swali hilo  alifafanua kuwa Serikali inapenda sana wanafunzi wa shule za msingi  kupata mlo wa mchana shuleni lakini Serikali kwa sasa bado serikali haijajipanga katika  kutekeleza mpango huo na badala yake wazazi wenyewe wajipange na kuchangishana ili  kuhakikisha watoto wao wanapata chakula hicho shuleni wakati serikali inaliangalia suala hilo.

“Wananchi hawana budi kuiga mfano wa kijiji cha milenia Mbola, nilipowatembelea wananchi walinieleza wanachangia chakula cha mchana kwa watoto wao wa shule za msingi na asiye changa wanamuadhibu hasa kwa kunyimwa pembejeo kwani kila aliyepata pembejeo lazima achangie chakula cha watoto wa shule na huo unitaratibu waliokubaliana nao.” Anasisitiza kikwete.

Dk. Nyadzi anafafanua kuwa chakula cha mchana shuleni ni cha muhimu sana kwani baada ya kila kaya ya Vijiji vya Milenia Mbola kuchangia chakula cha mchana shuleni, idadi ya uandikishaji wanafunzi imeongezeka shuleni, utoro umepungua na ufaulu wa wanafunzi umeongezeka.

“Chakula cha mchana shuleni kimepelekea idadi ya uandikishaji kuongezeka katika Vijiji vya Milenia Mbola toka wanafunzi 7,500 mwaka 2006 mpaka wanafunzi 8,100 katika shule zote 17 na mahudhurio yameongezeka toka asilimia 60 mpaka 98 halikadhalika ufaulu wa wanafunzi umeongezeka ambapo mwanafunzi bora katika matokeo ya darasa la saba (MOCK) ametokea katika Vijiji vya Milenia Mbola,” anasisitiza Dkt. Nyadzi.

Aidha, Dkt. Nyadzi anabainisha kuwa Changamoto kubwa inayokabili sekta ya kilimo ni wakulima kutofuata maelekezo ya wataalamu  pamoja na kuwa na upungufu wa pembejeo na mbolea ya kupandia na kukuzia.

Si kweli kuwa kila mwamba ngoma huvutia kwake bali ukweli utabaki pale pale kuwa mradi wa vijiji vya Milenia mbola umefanikiwa katika kutekeleza malengo nane ya milenia.

Mshauri wa Malengo ya Milenia nchini Dkt. George Sempeho anabainisha kuwa kilimo ili kiwe na manufaa kwa mkulima lazima sekta nyingine ziimarishwe kwa kuzingatia hayo ndiyo maana Mradi wa vijiji vya Milenia Mbola umejenga miundo mbinu, umeimarisha sekta ya afya, elimu, maji, nishati na biashara.

“Wakuu wa nchi 189 zilizo wajumbe wa Umoja wa Mataifa, Tanzania ikiwa ni mojawapo, walifanya kikao maalum kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Jijini New York kati ya tarehe 6 na 8 Septemba, 2000 na kupitisha kwa kauli moja Maazimio 8 muhimu yanayojulikana kama Malengo ya Milenia (UN Millennium Development Goals) na kati ya maazimio hayo yote ni lakini lilio muhimu lakini lilo sisitizwa ni lile la kuhakikisha kuwa umaskini na tatizo la njaa linaondolewa kwa asilimia 50.” Anasema Dkt. Sempeho.

Dkt. Sempeho anafafanua kuwa  suala la kilimo katika Mradi wa Vijiji Vya Milenia Mbola, kwa kuwa azimio zito kuliko yote ni lile la kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 nchi zote (189) zihakikishe umaskini na tatizo la njaa linaondolewa kwa asilimia 50.

“Malengo ya Milenia  yapo manane yakilenga kutokomeza umaskini, kutoa elimu ya msingi kwa watu wote, kuleta usawa wa jinsia, kupunguza vifo vya watoto wachanga, upatikanaji wa huduma bora za uzazi, kupambana na UKIMWI, malaria na magonjwa mengine; na la mwisho ambalo ni muhimu sana kwa nchi maskini ni kujenga na kuleta mshikamano wa kimaendeleo duniani.”Anaeleza Dkt. Sempeho

Aidha, Dkt. Sempeho anaelaeza kuwa malengo hayo nane ya Milenia iliamualiwa kutekelezwa katika kijiji cha Mbola kilichopo wilayani Uyui, Tabora  kwa kigezo cha kijiji masikini kwa kulinganisha na vijijji vingine Tanzania ambapo malengo ya milenia yangeweza kutekelezwa.

“Kwa hapa Tanzania kijiji cha Mbola  kilichoko wilayani Uyui, Mkoani Tabora,  ambaccho ni miongoni mwa vijiji kadhaa vya Afrika  vilivyo kusini mwa Jangwa la Sahara ambavyo viko chini ya Mpango wa Vijiji vya Milenia  wa Umoja wa Mataifa vilivyoanzishwa kuwa mfano wa utekelezaji wa Malengo ya Milenia,” anasisitiza Dkt. Sempeho.

 

Miradi mingi sana iliyopitishwa huko nyuma haikuonyesha tumaini kwa sababu mbalimbali zikiwamo kutowashirikisha wananchi wenyewe, mipango isiyo na muda, mingine haikushirikisha jumuia za kimataifa, yaani kila nchi ilitekeleza mipango hiyo kivyake na mipango mingine kutotekelezeka.

Dkt. Sempeho anatoa jibu la swali ambalo ungejiuliza na pengine limeshajenga  dhana potofu kwa wananchi juu ya mikakati mbalimbali inayolenga kutokomeza umasikini hasa  njaa kwamba kwa nini Mradi wa Vijiji vya Milenia Mbola umeleta matumaini makubwa kwa Viongozi wa Dunia?  Hapa kuna sababu nne zinazofanya Mradi huu kupewa heshima.

“Mosi, Mradi huu unatekelezeka; pili, Mradi wa Vijiji vya Milenia ni wa  watu si viongozi, una muda maalumu wa utekelezaji, yaani miaka 15; tatu, unapimika; nne, ni Mradi unao lenga ushiriki wa dunia kwa pamoja katika kutimiza malengo yake nane, yaani kushirikiana na kusaidiana kwa nchi maskini na tajiri na pia kushirikisha asasi za kijamii.” Anafafanua Dkt. Sempeho

 

Kijiji cha Mbola kiko mamia ya kilomita kutoka mji wa bandari wa Dar es Salaam kwenye Bahari ya Hindi na kiko karibu na mji wa Tabora. Hivyo, mtu angeweza kufikiri kuwa kwa  vile kijiji cha Mbola  kiko mbali na njia kuu za dunia ni rahisi kusahauliwa kimaendeleo. Lakini kwa kuwashirikisha wananchi wa Mbola wameweza kujikwamua  na  umasikini hasa katika upungufu wa chakula.

Ni dhahiri kuwa mpiga zumari ndiye mchagua wimbo, hivyo kama jamii itahamasishwa ipasavyo katika kutekeleza miradi yao kama ilivyotokea kwenye Mradi  wa Vijiji vya Milenia Mbola  shughuli hizo zitakuwa endelevu,hivyo litakuwa ni jukumu tu la  serikali na wadau wengine kuwasaidia panapotakiwa.

Mwisho

 

 

Page 2 of 3
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved