Logo
Feature Stories

DocumentsDate added

Order by : Name | Date | Hits [ Ascendant ]


“Hakuna Kuomba Kura kwa Kufunika Kiganja” – Sheria Mpya ya Gharama za Uchaguzi

Katika Mkutano wake wa 18, uliofanyika mwezi Januari 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya kuweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu Mapato, Matumizi  na Gharama za Kampeni na Uchaguzi wa Vyama vya  Siasa na Wagombea (Election Expenses Act 2009).  Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 17 Machi, 2010 ili iweze kutumika.

Kutungwa kwa sheria hii ni kutokana na nia ya dhati  ya kukuza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini, aliyoionesha Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati akizindua Bunge  tarehe 30 Desemba 2005 huko Dodoma , kwa  kusema;

“Taifa tumeanza kuwa na fikra kuwa vyama vya siasa vimeweza kununuliwa kwa fedha. Kama hii ni kweli , lazima tuwe waangalifu sana na kuhakikisha kuwa Taifa letu haliwezi hata siku moja kuwekwa rehani kwa fedha  ili mradi tu mtu  fulani anataka kuingia Ikulu. Lakini siyo sahihi hata kidogo kununua  ushindi . Lazima tulipige vita jambo hili, kwa hali hii tunapashwa  kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi. Hali  hii itatufanya tuwe na muafaka wa wazi wa kisheria kwa chama  au mgombea kupata fedha kwa matumizi ya kampeni, na kwa matumizi ya wazi na halali na udhibiti wake.”

Mheshimiwa Rais alibainisha kuwa wenye fedha huwa na maslahi yao na hutaka kuchagua mtu atakayelinda maslahi yao.  Alisema kuwa udhibiti wa matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi ni muhimu lakini pia udhibiti huo lazima ufanyike kwa umakini mkubwa kwani ukidhibiti sana watu wanapitia mlango wa nyuma.

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa  ambayo ni nyumba ya demokrasia, chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa Bw. John Tendwa, iliandaa muswada wa sheria ya kuweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu Mapato , Matumizi  na Gharama za Kampeni na Uchaguzi wa Vyama vya  Siasa na Wagombea (Election Expenses Act 2009).

Ili kuhakikisha kuwa Sheria hii inapata ushiriki wa kutosha kutoka kwa wadau wote, Serikali kwa kupitia gazeti la serikali ilitoa Tangazo No. 50 la tarehe 11 Desemba 2009 na kutangaza muswada No. 17 wa Serikali kuhusu kuweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato na matumizi na gharama za kampeni na uchanguzi wa Vyama vya Siasa na mgombea(Election Expenses Act 2009).

Baada ya kukusanya maoni kutoka kwa mtu mmoja mmoja, Taasisi zisizo za Serikali  na vyama vya siasa  na hatimaye kuwasilishwa kwa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba. Muswada uliweza kujadiliwa tarehe 11 Februari 2010 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na kupitishwa rasmi kama Sheria itakayoanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu  Oktoba 2010.

Katika kuboresha maoni ya wadau mbalimbali, kabla  ya Wabunge kupitisha Sheria hiyo lakini pia walishiriki katika kuiandika sheria hiyo kwa wabunge wa Upinzani na Chama tawala kwa kushirikiana  bila kujali itikadi za vyama vyao bali kwa kuweka maslahi ya Taifa mbele, lengo likiwa ni kuzuia kabisa matumizi ya fedha chafu katika kujipatia uongozi  wa kisiasa katika ngazi zote.

Ni vyema Watanzania wakaelewa Sababu kuu na Madhumuni ya  kutungwa kwa Sheria ya Gharama za uchaguzi.

Sababu kuu za kutunga Sheria ya Gharama za uchaguzi ni kuweka utaratibu wa kisheria wa kusimamia mapato na matumizi ya gharama za Kampeni za Vyama  vya siasa na wagombea.

Sababu nyingine ni kuweka utaratibu utakaowezesha serikali kuchangia gharama za uchaguzi na kampeni kwa vyama vya siasa.

Vilevile utaratibu wa kisheria wa kuratibu zawadi, misaada na michango itakayotolewa na wagombea wakati wa Kampeni za uchaguzi.

Lakini pia Sheria hii inalenga katika kuweka utaratibu wa kudhibiti matumizi ya fedha wakati wa Kampeni za Uchaguzi na kuweka mfumo wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma .

Pamoja na mambo mengine, Sheria hii inabainisha utaratibu wa adhabu kwa watakaokiuka  masharti yaliyomo  kwenye Sheria yenyewe.

Madhumuni ya Sheria hii ya Gharama za Uchaguzi ni kuweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya Kampeni.

Sheria itasaidia kudhibiti matumizi ya fedha na vitendo vya rushwa kwenye Kampeni za Uchaguzi kwa kuwepo kwa utaratibu wa fedha zitakazotumika katika Kampeni na Uchaguzi ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea.

Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa katika nchi nyingi kama vile: Ujerumani, Msumbiji, Zambia, Kenya , Uingereza , Ufaransa na Malawi imedhihirika kuwa kukosekana kwa sheria ya udhibiti wa matumizi ya fedha wakati wa kampeni na uchaguzi, hakuleti usawa katika mfumo mzima wa vyama vya siasa.

Ndani ya vyama vya siasa vyenyewe, wale wenye mifuko ya fedha wana sauti kubwa  ndani ya vyama, hivyo hii ni pamoja na uongozi ndani ya vyama na uteuzi wa wagombea kwa nafasi za juu za kiserikali.

Akichangia mswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi Bungeni, Mbunge wa Ukerewe, Mhe. Getrude Mongela alionyesha kusikitishwa kwake kwa hali ilivyo sasa katika kampeni na chaguzi za hapa nchini, akisema kwa kawaida  kiganja cha mtu anayeomba huwa chini  na anayetoa huwa juu kwa kumpa mwombaji, lakini sasa anayeomba anafunika kiganja cha anayemwomba.

“Wakati nagombea ubunge kwa mara ya kwanza nilikuwa ni mwanafunzi tu wa kutoka Chuo Kikuu na nilikuwa nagombea ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki, sikuanzia katika Bunge la Tanzania, lakini niliomba kura  kwa wabunge  kwa mikono yangu miwili wakati ule ilikuwa pale katika ukumbi wa Karimjee Hall, na bila hiyana wabunge walinichagua kuwa mbunge, kama wangetaka niwafunike viganja nisingeweza kwa maana ya kuwapa chochote lakini walichoangalia ni uwezo wangu wa kujieleza na kujiamini kwangu kwa jinsi ninavyoweza kuwatumikia wananchi’’ alisema Mhe. Mongela.

Kwa upande mwingine Chama chenye fedha nyingi au vyanzo vingi vya fedha kina nafasi  kubwa na uwezo mkubwa dhidi ya vyama vingine  ambavyo havina fedha na uwezo kidogo wa kupata fedha. Hali hii huleta tofauti kubwa baina ya vyama hivyo wakati wa ushindani  wa kisiasa ndani ya Kampeni na Uchaguzi.

Ni vyema ikaeleweka kuwa Sheria hii ya  Kudhibiti Matumizi ya Fedha wakati wa Kampeni na Uchaguzi  inazingatia vigezo vya  mazingira ya nchi yetu ya kisiasa, kama  ilivyo katika nchi nyingine zote duniani lakini vigezo vikuu vya mazingira ya kisiasa  ambavyo sheria  hiyo imejikita  ni katika mambo kadhaa.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na ukomo wa michango, michango inayozuiliwa, ukomo wa matumizi, muda mwafaka wa kampeni, kutangaza kwa mali au fedha za kampeni na uchaguzi (public disclosure), mchango wa Serikali.

Sheria ya Gharama za Uchaguzi imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo  ni jina, tarehe ya kuanza kutumika  kwa sheria hii katika Tanzania Bara na Zanzibar  na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.

Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa  na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.

Sehemu  ya Tatu inahusu masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi , uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama  ambazo Vyama vya Siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti  kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.

Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokelewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya Kampeni za Uchaguzi, Matumizi ya gharama kwa vyama na Taasisi za kiserikali  wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.

Sehemu ya Tano inahusu masharti  yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi  hayo ni yale yanayohusu  gharama kwa vitendo vinavyozuiwa  au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.

Sehemu ya sita ya Sheria ya Gharma za Uchaguzi  inapendekeza makosa ya  ujumla  pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya Sheria hii.

Sehemu ya saba inaweka masharti  kuhusu haki ya mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari, wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia  haki  hiyo.

Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa kutumia  vyombo vya ulinzi  na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya Siasa, wagombea wao na  wapiga kampeni wanafikia wapiga kura bila ubaguzi wala  kupewa vitisho.

Sehemu ya Nane ya Sheria inafanya marekebisho katika Sheria ya Vyama  vya Siasa ili kuoanisha masharti  ya Sheria hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza  kifungu cha 13A katika Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii wakati wa kampeni za uchaguzi. Aidha, kifungu hicho kinaweka utaratibu utakaowezesha kuhifadhi utambulisho wa watoa taarifa (whistle blowers).

Ifahamike kuwa dhana ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi  imetokana na maamuzi ya Umoja wa Nchi za Kiafrika (African Union – AU) ya kupiga vita  rushwa na kuzuia rushwa wakati wa kampeni na uchaguzi. yaliyofanyika Jiini Maputo Msumbiji mwaka 2003.

Maamuzi hayo yalitaka nchi wanachama kutunga sheria zitakazosimamia udhibiti  wa matumizi ya  fedha wakati wa kampeni na uchaguzi na kuzitaka nchi hizo  kutunga sheria yenye kujikita katika vifungu vikuu viwili ambavyo ni : Vifungu  vinavyokataza matumizi na upatikanaji wa fedha haramu kwa vyama vya siasa pamoja na kuweka kifungu chenye kuonyesha uwazi (transparency) na uwajibikaji kwa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi na kampeni.

Hakuna anayeweza kupinga kuwa rushwa katika demokrasia changa huondoa uwajibikaji katika Serikali, hali ambayo pia hukomaza rushwa ndani ya vyama vya siasa ambapo katika hali hii uwajibikaji katika serikali hupungua hasa kwa nchi isiyokuwa na  sheria ya kudhibiti  gharama za uchaguzi na kampeni.

Tanzania imefanya uamuzi wa kijasiri kwani  nchi nyingi za  Bara la Afrika hazina sheria ya uwazi na udhibiti  wa matumizi ya   fedha wakati wa  kampeni na uchaguzi .  Hivyo, kwa nchi zilizo kusini kwa Afrika (SADC) Tanzania imeamua kukuza demokrasia nchini kwa kuwa na sheria hiyo tofauti na nchi nyingine.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mheshimiwa Philpo Marmo wakati akiwasilisha hoja ya Sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi  aliwabainishia Wabunge kuwa pamoja na kutungwa sheria hii ili iweze kusimamiwa  na kutekelezwa  kwa umakini inahitaji kuungwa mkono na wadau wote kwa vitendo lakini pie Serikali ipo tayari kuiboresha kwa kadri itakavyoona kuna umuhimu.

“Sheria hii mpya ya Gharama za Uchaguzi ili ifanikiwe  inahitaji  utashi wa kisiasa, elimu kwa umma  kutolewa juu ya Sheria hii ambapo Serikali itaiandika katika lugha ya Kiswahili ili kila mwananchi aielewe lakini  pia  Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa Vyama vya Siasa vya Upinzani na Chama Tawala kuunga mkono Sheria hii ili kuzuia matumizi ya fedha chafu katika Kampeni na Uchaguzi.” Alisisitiza Marmo.

MwishoWanawake na Wasichana ni nguvu kwa kinga dhidi ya maafa tuitambue.

Kwa kuanza na Usemi usemao“Ukimuelimisha mwanamke umeielimisha jamii nzima”,   bila shaka utajiuliza ni jinsi gani  mwanamke mmoja  aweza kuielimisha jamii nzima, kimsingi usemi huu unalenga kutambua kuwa mwanamke anayo majukumu makubwa katika kuimarisha jamii, bali ni kwa nadra sana kwa jamii husika hutambua Umuhimu wa wanawake na wasichana.

Kwa mantiki hiyo, kwa mwaka huu Mwezi Oktoba tarehe 12, Tanzania na nchi nyingine duniani wanaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupunguza Athari za Maafa, Lengo kuu la maadhimisho hayo ni kutambua na kukubali kuwa mamilioni ya Wanawake na Wasichana ndio huifanya jamii kuwa imara katika kinga dhidi ya Maafa na athari za hali ya hewa ili kuweza kuleta manufaa na kulinda maendeleo katika uwekezaji.

Pamoja na kazi yenye mafanikio makubwa ya wanawake ya kupunguza athari za maafa lakini  ni kwa kiwango kidogo mchango wao hutabuliwa kutoonekana katika kufanya maamuzi.  Ujumbe wa Siku ya Kimataifa ya Upunguzaji wa Athari za Maafa wa mwaka huu 2012 umetilia mkazo wa dhati wa kuifahamisha jamii kuwa  mchango wa wanawake katika kuilinda na kuijenga jamii kabla na  baada ya Maafa huwa hautambuliwi, hivyo jamii husika haina budi kutambua mchango wao.

Ni wazi kuwa sababu kuu inayosababisha maafa kutokea ni kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu hatua za kuchukua, kuzuia, kujiandaa au kupunguza athari za  maafa. Kwa kuwa msingi wa jamii ni mwanamke, hivyo mwanamke akielimishwa ni dhahiri kuwa jamii nzima inaweza kuwa na uelewa mkubwa wa kujiandaa, kukabili na kupunguza athari za maafa.

Kabla hatujaona nguvu ya mwanamke katika kinga dhidi ya maafa, tuelewe kuwa kutokana na jamii kutokuwa na ufahamu wa kutosha jamii hujiingiza katika hatari nyingine zinazosababisha maafa kama vile; kuwa karibu na eneo la janga au kukimbilia kwenye maeneo ya hatari, uharibifu wa mazingira, kuongezeka kwa idadi ya watu hususan kwenye maeneo yasiyofaa kwa makazi ya binadamu, kupanuka kwa miji bila kufuata sheria za mipango miji.

Ningependa ifahamike kuwa Maafa ni matokeo ya janga ambalo  huathiri kwa kiwango kikubwa mfumo wa kawaida wa maisha ya jamii kwa kusababisha vifo, majeraha, upotevu au uharibifu mkubwa wa mali au mazingira  ambao jamii iliyoathirika haiwezi kukabili kwa uwezo au rasilimali zake bila msaada kutoka nje ya jamii hiyo.

Ukizungumzia athari za maafa duniani, akilli ya mtu itakumbuka kwa haraka  maafa ya miaka ya hivi karibuni ya tetemeko kubwa la ardhi lililoambatana na mawimbi ya bahari maarufu kama TSUNAMI katika miji ya SENDAI na FUKUSHIMA nchini JAPAN yaliyosababisha vifo vya maelfu ya watu na uharibifu mkubwa wa miundombinu mbalimbali,  makazi ya watu na mali nyingi.

Kwa hapa  nyumbani watanzania tumeshuhudia pia maafa mbalimbali. Maafa hayo  ni pamoja na yale ya milipuko ya mabomu huko Mbagala mwaka 2008 na Gongo la Mboto mwaka 2009 Jijini Dar es Salaam ; mafuriko mwaka 2011 ya Jijini Dar es Salaam; kuzama kwa meli Mv Spice Islender mwaka 2011, MV SKAGIT mwaka 2012 na milipuko ya magonjwa ya kipindupindu pamoja na moto viwandani, ofisini na kwenye nyumba za kuishi.  Athari za maafa hayo zimekuwa ni kubwa kutokana na kutokuchukua hatua za tahadhari mapema.

Utajiuliza kwa nini maadhimisho hayo yalenge kuthibitisha vitendo na jitihada wafanyazo  Wanawake na Wasichana kuwa ni nguvu kwa kinga dhidi ya   maafa? Jibu li wazi kuwa sote ni mashahidi kuwa mwanamke ni mtu muhimu duniani,  ukitoa  dhima kubwa aliyonayo ya malezi ya familia lakini ndiye kinara  na chachu  wa maendeleo ya familia, jamii na pia ndiye mjenzi wa amani katika familia na jamii yake.

Jumuiya ya Kimataifa tayari imetambua nafasi na dhamana ya wanawake katika kulinda na kudumisha misingi ya amani duniani na inaendelea kuthamini mchango makini uliotolewa na wanawake wawili kutoka Liberia: Hawa ni Rais Elle Johnson Sirleaf na Bibi Leymah Gbowee pamoja na Tawwakkol Karman, mwanamke kutoka Yemen. Hawa ndio waliojinyakulia tuzo ya Amani kwa Mwaka 2011.

Aidha hata yale mafanikio  wanayopata wanaume utakuta kuwepo kwa mchango wa mwanamke. Lakini kutokana na kutokuwepo kwa uwiano na usawa wa jinsia kama ilivyo sasa katika jumuiya, kunaizuia jamii kutambua uwezo wao  kamili katika shughuli zote zinazohusu maendeleo ya uchumi, jamii na maeneo ya siasa hatimaye juhudi mbali mbali za kimataifa  za kuleta maendeleo duniani zimekuwa zikidolola.

Kwa mantiki hiyo, Ili kupunguza athari za maafa duniani, Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ya Mkakati wa Kupunguza Athari za Maafa (United Nations Secretariet for International Strategy for Disaster Reduction). Kwa mwaka 2012, Sekretarieti hiyo imechagua kaulimbiu ya Kampeni ya Dunia kuwa ni “Wanawake na Wasichana – Nguvu isiyoonekana kwa kinga dhidi ya Maafa”.

Kauli mbiu hii inalenga kufafanua kuwa uwezo wa wanawake na wasichana katika kutoa mchango wao wa kupunguza athari za maafa hauonekani kwa sababu za kutoshirikishwa katika kutoa maamuzi katika Upunguzaji Athari za maafa katika ngazi za uongozi, mpangilio wa progamu na uelewa mdogo wa usawa wa kijinsia, hatimaye nguvu ya wanawake katika kinga dhidi ya maafa haionekani.

Serikali kwa kutambua hilo imefanikiwa kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbali mbali za uongozi wa kisiasa na kiutendaji. Mathalan,Wabunge Wanawake wameongezeka kutoka asilimia 11 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 36 mwaka 2011.  Kwa upande wa Mawaziri wameongezeka kutoka asilimia 12 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 27.5 mwaka 2011.

Tukizingatia ushiriki huo na mfumo wetu wa kukabiliana na maafa ambao una Kamati za Maafa kwenye ngazi ya mkoa, wilaya hadi kijiji ambazo zina majukumu ya kusimamia masuala ya maafa katika maeneo yao. Hivyo Wanawake na Wasichana wanaweza kushiriki kikamilifu katika hatua zote za Upunguzaji Athari za maafa.

Katika ngazi ya  uongozi wa kiutendaji Wakurungezi wa Halmashauri wameongezeka pia kutoka asilimia 6 mwaka 1991 hadi kufikia asilimia 26 mwaka 2011 wakati  Majaji wanawake wameongezeka kutoka asilimia 6 mwaka 1990 hadi kufikia asilimia 35 mwaka 2011, hivyo wanawake wa Tanzania wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wao katika kutoa maamuzi ya Upunguzaji Athari za maafa

Ieleweke kuwa Asilimia 52% ya watu Duniani ni Wanawake na Wasichina, hivyo utaelewa kuwa nusu ya watu duniani ni wanawake na wasichana ndio maana Kampeni hii ya Dunia inayoendelea hivi sasa inajikita katika kujiandaa na maafa ili kukinga au kupunguza athari za maafa kwa kuhakikisha nguvu ya wanawake na Wasichana katika kukinga na kukabiliana na maafa inatambuliwa na jamii na kwakuwa wao ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa maafa.

Hili lilijidhihirisha wakati mvua kubwa zilizonyesha usiku wa tarehe 19 Desemba, 2011 hadi tarehe 22 Desemba, 2011 Mkoa wa Dar es Salaam Kutokana na mafuriko yaliyotokea, nyumba nyingi zilizo mabondeni ziliathirika kwa kuzingirwa na mafuriko makubwa ambayo hayajawahi kutokea kwa miaka mingi na kusababisha watu zaidi ya 5000 kuondoka katika makazi yao. Watu 40 (wanawake 10 na wanaume 30) walipoteza maisha.

Kampeni hii pia inajikita katika kuongeza uelewa wa  wananchi na serikali katika ngazi zote juu ya umuhimu wa kujikinga na kupunguza athari za maafa kwa kuwawezesha Wanawake na Wasichana katika kuchangia kuleta maendeleo endelevu kupitia Upunguzaji wa Athari za Maafa, hususani katika nyanja za  Mazingira na Usimamizi wa Mali asili, Utawala, Mipango miji, Matumizi bora ya ardhi na mipango ya kijamii na kiuchumi zikiwa ni mihimili ya kinga dhidi ya  maafa.

Nchini Tanzania inakadiriwa kwamba wanawake hasa wa vijijini wanatoa asilimia 80 ya wafanyakazi katika eneo la kijiji na hivyo kutoa asilimia 60 ya chakula kinachozalishwa.  Ingawa wanawake ndiyo wazalishaji wakubwa wa mazao ya biashara, mazingira hayawaruhusu kumiliki mali zao. Pia jamii haitambui nguvu ya mwanamke anayo itumia kuikinga na maafa ya njaa.

Hii inadhahirisha kuwa mlimaji akiwa mmoja (mwanamke) na walaji wakawa wengi jamii hiyo ni vigumu kukwepa janga la njaa na hasa jamii hiyo ikikumbwa na ukame, matokeo yake Serikali huchukua hatua za ziada  za kuipeleka chakula cha msaada kwa jamii yenye upungufu wa chakula.

Mfano hai ni kutokana na athari ya  ukame ulioikumba  nchi yetu mwaka 2009 na hatimaye kuifanya baadhi ya mikoa  na kaya zake kuathiriwa na njaa , Ofisi ya Waziri Mkuu ilitoa chakula cha msaada kwa Mikoa 15 kwa ajili ya kusambazwa katika Wilaya 59 za Mikoa hiyo, iliyokuwa na upungufu mkubwa wa chakula. Chakula hicho kilisambazwa kati ya mwezi Februari 2009 na Februari 2010.

Kama kampeni hii inavyotaka kuwa Wanawake na Wasichana wawezeshwe katika Matumizi bora ya ardhi na mipango ya kijamii na kiuchumi, tayari Serikali imepitisha sheria kadhaa katika kutoa upendeleo kwa wanawake kwa mfano “Sexual Offences Special Provision Act of 1998, Land Law Act of 1999 na Village Land Act of 1999.

Sheria hiyo ya kwanza inawalinda wanawake, wasichana na watoto kutokana na kunyanyaswa kijinsia na matendo mabaya.  Sheria mbili za mwisho zinahuisha na kufuta sheria za awali zinazohusu masuala ya ardhi na hivyo kuwawezesha wanawake kufaidi haki sawa na wanaume za kuweza  kupata, kumiliki na kudhibiti ardhi.

Aidha Kampeni hii inasisitiza kuwa ili nguvu ya mwanamke katika kinga dhidi ya maafa ionekane  na jamii husika iweze kupata matokeo mazuri ya Upunguzaji wa Athari za Maafa ni vyema Wanawake na Wasichana wakashirikishwa katika mikakati ya mabadiliko ya hali ya hewa ili kuweza kuleta mafanikio katika masuala ya Maafa na lazima wahususishwe katika sera, mipango na utekelezaji wa maandalizi hayo.

Mshindi wa tuzo ya Amani kwa Mwaka 1984, Desmond Tutu alipata kunena kuwa “Kama tunataka kuona maendeleo ya kweli Duniani, basi Uwekezaji mzuri ni Wanawake”

Kimsingi Tutu alikuwa akikisitiza wanawake wasibaguliwe katika shughuli za maendeleo, ambapo kampeni hii inataahadharisha kuwa kutokuwepo kwa uwiano na usawa wa jinsia katika jamii ni hatari sana pindi yanapotokea majanga kwa kuwa jamii hukosa uwezo wa kuwashirikisha watu wote katika hatua za kukabili maafa.

Serikali ya Tanzania tayari kauli ya Tutu ilishaitekeleza kwa Mwaka 2009, kupitia  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa kuratibu uanzishizwaji wa Benki ya Wanawake Tanzania.  Benki hii ilizinduliwa rasmi tarehe 4 Septemba 2009. Hadi kufikia tarehe 31 Mei, 2011 jumla ya akaunti zilizokuwa zimefunguliwa zilikuwa 18,824 ambapo akaunti 14,787 sawa na asilimia 78.6 ni za wanawake, akaunti 3,578 sawa na asilimia 21.4 ni za wanaume.

Ifahamike kuwa Uwiano sawa na jinsia huanza na elimu, kama wasichana na wavulana watahusishwa kikamilifu katika maisha ya kila siku, katika ukuaji wa vijana wa kike na kiume hii itasaidia kuondoa vikwazo vya wasichana kushiriki katika elimu ambapo hufundishwa ni namna gani wanaweza kujiandaa, kukabiliana na kupunguza athari za maafa. Kutokana na mazingira hayo Wizara imefanikiwa kueneza uelewa wa wananchi.

Kwa hapa Tanzania Matokeo ya uelewa huo ni pamoja na kuongezeka kwa uwiano wa wavulana na wasichana katika shule za msingi na sekondari ambao umefikia asilimia 50 kwa 50.

Ofisi ya Waziri Mkuu,  Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Mamlaka ya Elimu Tanzania  tayari wameshaanza mchakato wa kuingiza masuala ya maafa katika mitaala ya Elimu ya msingi na Sekondari, ikiwa ni nia ya Serikali ya kuongeza uelewa wa masuala ya maafa kwa vijana wa kiume na kike ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuchukua hatua za kuzuia, kujiandaa au kupunguza athari za maafa.

Dira ya Maendeleo ya 2025 ya Tanzania inalengo la kuwapatia watu wake hali ya juu ya maisha, kufanikiwa katika kupata utawala bora wa kuheshimu sheria pamoja na kuendeleza uchumi imara na wa ushindani.  Ili kufanikiwa kuleta usawa wa jinsia na kuwapa uwezo wanawake katika maeneo ya jamii, uchumi, uhusiano wa siasa na utamaduni lazima yatiliwe maanani.

Kwa kuwa jinsia ni mkondo mkuu ambao vipengele vyote vya maendeleo hupita ili kuimarisha uchumi wa Taifa, siasa na masuala ya jamii na utamaduni. Hatuna budi kuwashirikisha na kutambua michango ya wananwake na Wasichana katika kuzuia, kujiandaa au kupunguza athari za maafa na hatimaye tutaewza kupata Usalama wa nchi yetu dhidi ya maafa.

WAWEZESHE WANAWAKE NA WASICHANA KWA USALAMA WA KESHO.

Mwisho.

 

 

 

 

 

Wahitimu vyuo vikuu wanaweza kutumia  taaluma zao kutengeneza ajira

“Taasisi yenu iwe mfano wa kuigwa na vijana wengine wahitimu katika fani mbalimbali kuona namna ambayo wanaweza kutumia elimu na utaalamu wanaoupata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kuweka mipango madhubuti ya kujiajiri”  anasisitiza Nagu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji) Dk. Mary Nagu (Mb) alilisitiza hayo hivi karibuni wakati alipoongoza matembezi ya “Saidia Mama Mjamzito Kujifungua Salama” yaliyoandaliwa na Taasisi ya Madaktari wahitimu wa Vyuo Vikuu Tanzania (TPHI) yaliyoanzia katika hospitali ya Manispaa ya Temeke mpaka Ofisi za Manisipaa hiyo, Jijini Dar es Salaam.

Ni dhahiri kuwa  maendeleo ya elimu  nchini yamechochea kuongezeka kwa vyuo vikuu hapa nchini na idadi ya wahitimu katika vyuo hivyo , ikiwa ni ishara ya uthubutu na utayari wa serikali katika kuwekeza na kusimamia sekta ya elimu hapa nchini,

Lakini bado idadi ndogo ya wahitimu wanaoweza kupata ajira  katika sekta ya umma na binafsi kutokana na ufinyu wa nafasi hizo.

Ni jambo la kuzingatia kuwa Fani ya Udaktari ni fani ambayo inauhakika wa ajira lakini pamoja na kulitambua hilo wametambua kuwa njia bora ya kujikwamua na kujiwezesha kujiajiri ni kuazisha kikundi chenye kutumia taaluma yaolakini pia ikiwa ni sehemu ya chachu ya kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto zinazowakabili mama wajawazito hapa nchini.

“Kwa niaba ya serikali napenda kuwapongeza Taasisi ya Madaktari Wahitimu wa Vyuo Vikuu Tanzania kwa kuwa chachu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika  kuwezesha vijana kujiajiri na napenda kuwahakikishia kuwa serikali inatambua mchango wenu wa kuunga mkono serikali katika kuboresha huduma za afya kwa akina mama na watoto”  alisema Nagu

Wahitimu katika fani mbalimbali hawanabudi kuona namna ambayo wanaweza kutumia elimu na utaalamu wanaoupata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kuweka mipango madhubuti ya kujiajiri kwa kujitoa kwa dhati katika kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu na kwa upendo na hatimaye kupunguza idadi kubwa ya kukosa ajira.

Aidha  Nagu anafafanua kuwa pamoja na kuwa Taasisi hiyo kuwa  inatengeneza ajira kwa vijana jambo kubwa  inalolitekeleza vizuri ni kwa kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha afya ya Mama mjamzito hapa nchini ,mpango wenye lengo la kupunguza  vifo kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Hayumukiniki kuwa zipo changamoto kwa wahitimu katika kutumia taaluma zao kujiajiri lakini kwa nia anayo idhihirisha Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji na Uwezeshaji ni wazi kuwa wahitimu watakao thubutu wanaweza kufanikiwa kujiajiri lakini pia taaluma yao kuweza kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Pamoja na juhudi zinazofanywa na TPHI lakini pia zipo changamoto wanazo kabiliana nazao ambapo  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Madaktari Wahitimu Vyuo vikuu Tanzania, Dk. Teresphory Kyaruzi anabaibisha  changamoto kubwa waliyonayo ni jinsi ya kuwapelekea huduma wanachi kwa wakati na kwa gharama wanazoweza kuzimudu.

“Ukubwa wa changamoto hii unatokana na jinsi ya kuwafikia wananchi hasa akina mama wajawazito na watoto walioko vijijini na wanao ishi kwenye mazingira magumu.” Alisisitiza  Kyaruzi .

Takwimu zinabainisha kuwa Katika mwaka 2010 kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupungua kwa vifo vya mama wajawazito na wototo kufikia 454 kati ya watoto 1000 kutoka 578 kwa mwaka 2005.

Katika kusisitiza hili ni vyema tukatambua kuwa kidole kimoja hakivunji chawa hivy o hata wahitimu wahitimu katika fani mbalimbali katika umoja wao kwa kuzingatia elimu na utaalamu wanaoupata katika vyuo mbalimbali hapa nchini kwa kuweka mipango madhubuti ya kujiajiri wanaweza kupunguza matatizo yanayo ikabili wananchi.

Serikali katika kutekeleza hili tayari imeshaanza kutekeleza kwa vitendo kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia katika Mpango wa Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi na Kuongeza ajira (JK Fund), Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF) na Mfuko wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF).

Ni dhahiri kuwa tukishirikiana na Mifuko ya serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi tunaweza kuutokomeza umasikini kwa kujiajiri wenyewe lakini pia kutumia fani zetu kwa kutatua matatizo yanayo ikabili jamii inayotuzunguka.

Mwisho.

Vikundi vya Kuweka na kukopa ni Daraja la kumkomboa Mwananchi Kiuchumi

Vinatoa mikopo kwa masharti nafuu

“Ni wazi kwamba Serikali inalitambua tatizo kubwa la umasikini hasa umasikini wa kipato kwa wananchi wake mijini na vijijini ambao unasababisha wananchi kuishi katika hali duni. Ukosefu wa mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi za wananchi ni moja ya zababu zinazochangia katika umasikini wa wananchi.” alisema Nagu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu mwenye dhamana ya Uwezeshaji na Uwekezaji Dk. Mary Nagu anabainisha kuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mitaji kwa ajili ya kuwekeza katika sekta mbalimbali ni benki za biashara. Hata hivyo benki hizo zimekuwa na masharti magumu ya kutoa mikopo ambayo wananchi walio wengi hawawezi kuyatimiza na kupata mikopo.

“Masharti hayo ni pamoja na riba kubwa katika muda mfupi na dhamana kwa kutumia mali isiyohamishika kama vile hati ya shamba na kiwanja, ambazo wananchi walio wengi hawana, hawana si kwasababu nyingine bali umasikini unaowakabili” anasisitiza Nagu.

Hapa ndo tunajiuliza ni jinsi gani wananchi wenye kipato cha chini wanaweza kujikomboa kiuchumi kwa kupata mitaji kwa  mikopo  yenye masharti nafuu na hatimaye kuongeza kipato,  kupata ajira na kupunguza umasikini.

Katika kukabiliana na tatizo hili Serikali imebuni Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004, ikiwa inalenga kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fursa za kushiriki katika Shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali.

Jukumu la Utekelezaji wa Sera hii ni la wote kwa maana ya Serikali na taasisi zake, Sekta binafsi na wananchi wote kwa ujumla.

“Moja ya mahitaji ya Sera hiyo ni kuhamasisha uanzishwaji wa ushirika wa kuweka na kukopa, zikiwemo SACCOS, VICOBA na aina nyingine za ushirika ili wananchi wengi zaidi wajiunge na kuweza kuongeza uwezo wao wa kimtaji ” anaeleza Nagu.

Hapa Dk.Nagu anafafanua kuwa vikundi vya kuweka na kukopa ndio daraja la kuwakomboa watanzania kiuchumi kutokana na mabenki kusita au kushindwa kutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wananchi wenye kipato cha chini.

Anasema vikundi hivyo ni njia endelevu katika kukusanya akiba na kuchochea upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kuendeleza juhudi za ujasiriamali za kupambana na  umasikini .

Akitoa mfano wa Jumuiya ya Kukuza Uchumi Ilala (JUKUILA) kama vikundi vinavyotekeleza mpango wa kuweka na kukopesha wanakikundi ambapo sifa za mkopeshwaji ni kuwa mwananchama wa vikundi vya JUKUILA na rekodi safi za uwekaji akiba na ukopaji.

Jambo la kutambua ni kuwa mwamko wa wananchi wa kujiumga na Ushirika wa  Vikundi vya kuweka na kukopa kuwa ni mkobozi wao kiuchumi umekuwa mkubwa, baada ya kugundua kuwa  ndiyo njia bora ya kupata mikopo  yenye masharti nafuu, kuongeza kipato,  ajira na kupunguza umasikini.

Matokeo ya uhamasishaji wa uanzishwaji wa vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (SACCOS) na VICOBA yanaonesha kuongezeka kwa vyama hivyo mara tatu kutoka 1,875 mwaka 2005 hadi 5,344  mwaka 2010, na kuongezeka kwa idadi ya wanachama wa vyama hivyo kutoka 1,360,850 hadi 2,100,000.

Aidha  matokeo hayo yanabainisha kuwa Akiba na amana za wananchama zimeongezeka zaidi ya mara tano , kutoka shilingi bilioni 31.4 mwaka 2005, hadi shilingi 174.6 mwaka2010.

Kutokana na fedha  wanazokopeshana  wanavikundi hutumia fedha hizo kwa ajili ya uzalishaji mali na huduma mbalimbali ikiwemo Utengenezaji wa sabuni, mishumaa, dawa za choo, majiko na viatu. Ufugaji wa kuku wa kisasa wa mayai na nyama. Hivi vyote vimekuza kipato na ajira na hivyo kupunguza unyonge na umasikini.

Nagu anafafanua  kuwa pamoja na kuwa wananchi walio wengi katika vikundi hivyo kuwa na kipato cha chini  na hivyo kushindwa kuchangia kiwango kikubwa cha hisa kwenye kikundi lakini hawana budi ikiwezekana kuongeza thamani ya hisa hizo ili mfuko uwe mkubwa zaidi.

“Ili uweze kupata mtaji mkubwa wa kuwekeza kwenye shughuli inayolipa zaidi na kukuwezesha kuwa na maisha bora inategemea sana kiwango cha akiba ulichochangia katika mfuko wa kikundi” alisema Nagu.

Anasema Uchumi wetu unategemea sana upatikanaji wa mitaji kutokana na uwezo wa kuweka akiba kupitia vikundi , mtu mmoja mmoja na taasisi katika mfumo wetu wa kibenki, ambapo kutokana na akiba hizo benki na taasisi za fedha zinzpata uwezo mkubwa zaidi wananchi kuwekeza katika miradi yao.

Nagu anasisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha umuhimu wa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili kuwezesha kukua kwa kiwango cha akiba kwa ajili ukopeshaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

MWISHO

Utekelezaji wa mikakati madhubuti utapunguza athari za maafa nchini

YANAPOTOKEA maafa mbalimbali nchini, njaa, magonjwa na vifo huweza kutokea kwa mtu yeyote na mara nyingine huwa ni vigumu kuyazuia  kwani hutokea katika mazingira yasiyotarajiwa.

Hivyo serikali za nchi mbalimbali duniani kwa kushirikiana na wadau tofauti wamekuwa hawana budi kuwekeza fedha zitakazotumika mara hali hiyo itakapojitokeza ili angalau kukabiliana nayo lengo likiwa ni kupunguza maafa.

Nchini tayari tumekwishashuhudia kutokea kwa maafa mbalimbali yaliyosababaishwa na maporomoko ya ardhi, vimbunga, mafuriko, Tsunami, tufani iliyoambatana na dhoruba kali, moto na hata ajali za barabarani.

Hivi karibuni jamii imejionea miji yetu ikikumbwa na maafa mbalimbali yakiwemo maafa ya milipuko ya mabomu ya Mbagala Dar es Salaam, mafuriko ya mvua katika maeneo mbalimbali ya miji yetu ambapo athari kubwa zaidi ilitokea mjini Kilosa mwishoni mwa mwaka 2009 hadi mwanzoni mwa mwaka huu.

Athari za maafa haya wakati mwingine zimekuwa kubwa kutokana na kutokuchukua hatua za tahadhari mapema. Matokeo yake ni serikali kuingia gharama kubwa kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa.

Kutokana na hilo, katika kufikia malengo ya kukabiliana na matukio hayo dunia iliona kuna sababu kwa kila nchi ulimwenguni kuifanya Oktoba 13, 2010, kuwa ni siku ya Kimataifa ya Upunguzaji Athari za Maafa (International Day for Disaster Reduction). Siku hii huadhimishwa Jumatano ya wiki ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka.

Siku hii iliwekwa maalum ili kuamsha uelewa wa wananchi kuzuia na kupunguza uwezekano wa athari za maafa yanayoweza kutokea na kuwafanya wawe tayari wakati wote kujihami na maafa.

Uhalisia ni kwamba maafa yanapotokea huathiri maisha ya watu, kuharibu mali na mazingira. Mbali na hayo hayachagui yanapotokea iwe vijijini au mijini, kutokana na hilo  ili kuweza kupunguza athari zinazoletwa na maafa ni lazima kuchua hatua za tahadhari mapema.

Kila mwaka Baraza la Umoja wa Mataifa hutoa kauli mbiu kwa wananchi kwa madhumuni ya kusisitiza mambo ya kuzingatiwa katika mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu wa 2010 ni ‘Kukinga miji yetu dhidi ya Maafa’ (Making Cities Resillient)

Hata hivyo yanapotolewa matamko mbalimbali na serikali juu ya kujikinga na maafa jamii hujiuliza kama kweli maafa yanaweza kukingwa. Hii inatokana na ukweli kwamba maafa hutokea bila kutarajiwa.

Katika tamko la mwaka huu alilolitoa Waziri Mkuu Mizengo Pinda Oktoba 13 mwaka huu amesema, athari za maafa huweza kupunguzwa kama hatua za tahadhari zitachukuliwa wakati wote na pia kuweza kuimarisha Miji nchini.

Vilevile miji inaweza kukingwa na maafa kama tutachukua hatua za kuboresha miundombinu ya miji na vijiji kama kutengeza mifereji bora ya kupitisha maji, kuwa na mifumo bora ya kupitisha maji safi na maji taka hii itasaidia kupunguza maafa na miji itakuwa salama pindi maafa yatakapotokea.

Kwani baadhi ya maafa maporomoko ya ardhi yanapotokea kama ilivyokuwa Wilayani Same eneo la Same miamba mawe, ardhi vilisogea kwenye mtelemko wa mlimani na kusukuma miti, nyumba na hatimaye kusababisha vifo vya watu takribani 21. Katika Alpi za Ulaya takriban watu 100 hufariki kila mwaka kutokana na maporomoko ya ardhi.

Chanzo kingine cha maafa ni Kimbunga ambayo ni dhoruba kali inayoanza juu ya bahari katika maeneo ya tropiki yenye upepo mwenye kasi ya zaidi ya 117 kilometa kwa saa.

Mara nyingine huanza juu ya bahari ya kitropiki penye maji yenye halijoto juu ya 26 °C. Hewa joto yenye mvuke nyingi inaanza kupanda juu na kuzunguka. Mzunguko huo unaongezeka kasi kuwa dhoruba. Kasi ikifikia mwendo wa 117 kilometa kwa saa na  kusababisha hasara kubwa ikigusa meli baharini na zaidi mwambaoni inapofikia nchi kavu au visiwa.

 

Hatari zake zingine ni kasi ya upepo pamoja na kiasi kikubwa cha mvua. Kasi ya upepo inaweza kuinua vitu vizito kama miti, paa za nyumba au magari na kuvirusha mbali. Watu huuawa na mali kuharibiwa. Uwingi wa mvua husababisha mafuriko.

Mafuriko ni hali ya kuwa na maji mengi yanayofunika nchi kavu pasipo na maji kwa kawaida. Hivyo yanapotokea popote baada ya mvua kali maji mengi yasiyo na njia hutawanyika kwenda kusikotarajiwa na kuleta madhara kwenye mashamba na hata kuharibu miundombinu ya barabara ama reli kama ilivyotokea wilayani Kilosa mwaka huu.

Mafuriko mara nyingi ni hatari kwa binadamu huleta hatari kwa maisha, mali na nyumba. Njia za kujiokoa ni pamoja na kuhama haraka penye miinuko au nchi ya juu zaidi. Nchini janga hilo ndilo limekuwa likiathiri sana jamii ya Watanzania kutokana na wengi kuishi sehemu za mabondeni ambako maji hukimbilia.

Pia maafa mengine husababishwa na tetemeko la ardhi ambalo kwa Tanzania limekuwa aliathiri sana linapotokea. Hili hutokea baada ya mshtuko wa ghafla wa chini ya ardhi. Limekuwa likitokea mara kwa mara lakini idadi kubwa ni hafifu mno haisikiki na wanadamu ila tu inapimwa na mitambo ya wataalamu.

Athari zingine za matetemeko ya ardhi ni kuweza kusababisha uharibifu mkubwa na vifo hasa kutokana na majengo yanayoanguka. Kwa upande wa baharini tetemeko mara nyingi husababisha tsunami.

Tsunami ambalo ni neno linapotokana na lugha ya Kijapani likimaanisha bandari ya mawimbi kutokea na kusababisha vifo vya maelfu ya watu. Wakati mwingine inaweza kutokea bila kuleta madhara yoyote.

Nchini lilipotokea Desemba 26, 2004 kwenye ufukwe wa Coco Beach jijini jumla ya watu saba walifariki wakati karibu na pembe ya kaskazini ya Sumatra kwenye mstari ambako bamba la Uhindi linajisukuma chini ya bamba ndogo la Burma lililoua takriban watu 275,000.

Kutokana na hilo ili miji iweze kushiriki kikamilifu katika kupunguza athari za maafa ni lazima iwe na mifumo mizuri ya kutoa tahadhari za awali, uwezo wa kukabili maafa pale yanapotokea na kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika tamko lake aliitaja baadhi ya mifumo hiyo kuwa ni miji ambayo wananchi wanashiriki kupanga na kuamua masuala ya mji husika kwa kushirikiana uongozi wa serikali za mitaa kulingana na rasilmali walizonazo.

Mifumo mingine ni ule wa uongozi makini na wenye kuwajibika na wenye mipango miji endelevu yenye kukubalika na makundi yote, mji ambao maafa yanaweza kuzuiwa kwa sababu wakazi wanaishi kwenye makazi yenye miundombinu imara kama vile umeme, maji ya bomba, mifereji ya maji safi na maji taka, barabara zinazopitika majira yote na huduma za jamii ambazo ni za uhakika.

Alizitaja huduma hizo ni pamoja na elimu, afya, uzoaji takataka na upatikanaji wa huduma za dharura. Pia iwe ni miji ambayo watu wake wanaishi kwenye majengo yaliyofuata vipimo sahihi na ambayo hayakujengwa kwenye mabonde au miinuko kwa sababu ya ukosefu wa maeneo ya makazi.

Hivyo kwa wadau wote wa udhibiti maafa hawana budi kuchukua hatua madhubuti kwa kuifanya miji yao kuwa inayoelewa madhara ya maafa kwa kuandaa taarifa za kutosha kuhusu hatari hizo na kuwaelimisha wananchi wake kwamba ni wakati gani wanajiweka kwenye hatari hizo na akina nani wanaweza kudhurika.

Masuala mengine ni kujihami na maafa endapo yatatokea, kutenga kiasi cha rasilmali zake ili kujihami na maafa, kuweza  kukarabati kwa haraka na kurejesha mapema huduma za jamii na shughuli za kiuchumi endapo zitakuwa zimeharibiwa na maafa, kutambua kwamba yote yaliyotajwa hapo juu yanategemea uwezo wao wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hivyo tamko la mwaka huu linabainisha pia kuwa na kampeni ya miaka miwili kwa kila mji duniani kujiwekea malengo ya kujihami, kukabiliana na maafa na kuwa tayari kurekebisha madhara yatakayoletwa na maafa ili maisha ya watu yarudie katika usalama wa awali.

Serikali tayari kwa upande wake kama alivyosema Pinda tayari imeweka rasilimali na miundombinu mbalimbali katika miji na majiji nchini kama hatua za kuboresha makazi huku ikitia maanani kuzuia, kujiandaa na kukabiliana na maafa pindi yanapotokea.

Aidha kutekelezwa kwa kampeni hii kutasaidia kuepukwa kwa majanga ya moto yanayoendelea kutokea kote nchini ukiachia mbali ule lililojitokeza kwenye jengo la Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambao uliteketeza jengo zima, huku askari wa Kikosi cha Zimamoto, polisi na viongozi mbalimbali wa mkoa huo wakiwa wameduwaa, wasijue la kufanya.

Kampeni hii ya miaka miwili kuanzia mwaka 2010/11 ina lengo la kuorodhesha walau viongozi wa serikali za mitaa wapatao 1,000 ambao wako tayari kuwekeza rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji ya upunguzaji athari za maafa ikiwemo kuboresha mipango miji, miundombinu na ujenzi salama; kuimarisha mifereji ya maji machafu ili kupunguza mafuriko na magonjwa ya mlipuko; kuweka mifumo ya kubaini maafa kabla hayajatokea na kutoa mafunzo ya kujihami au kujihadhari na maafa kwa wananchi.

Hivyo tungependa kuishauri Serikali na kuiasa kwamba wakati sasa umefika wa kubuni mikakati endelevu ya kupambana na majanga ya moto katika nchi yetu. Kwa hali ilivyo hivi sasa, tunaweza kusema kwamba maafa sasa yamekuwa matukio ya kawaida na ahadi za viongozi kuyamaliza zimekuwa zikichukuliwa na wananchi kama ngonjera zisizokwisha, kutokana na serikali kuonesha wazi kwamba haina ujasiri wa  kupambana nayo.

Baadhi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na serikali ni kuhakikishe kwamba kitengo cha Maafa kilichopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu siyo tu kipewe vifaa, bali pia kipandishwe hadhi kama taasisi inayojitegemea ili kiondokane na urasimu usiokuwa wa lazima.

Mwisho.

 

 

 

 

  • «
  •  Start 
  •  Prev 
  •  1 
  •  2 
  •  3 
  •  Next 
  •  End 
  • »
Page 1 of 3
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved