Logo
Details for Serikali yajizatiti katika Mwelekeo wa Kazi za mwaka 2013/2014.
PropertyValue
NameSerikali yajizatiti katika Mwelekeo wa Kazi za mwaka 2013/2014.
Description

Serikali yajizatiti katika Mwelekeo wa Kazi za mwaka 2013/2014.

Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye majukumu ya kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali katika sekta zote na Bungeni. Tangazo la Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba, 2010 limeainisha majukumu hayo ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Hivi karibuni, Mwezi Aprili mwaka huu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Peter Pinda (Mb) aliwasilisha shughuli ambazo Serikali imetekeleza kwa kipindi kilichopita cha mwaka 2012/2013. Aidha, Waziri Mkuu alibainisha Mwelekeo wa Kazi zitakazofanyika mwaka 2013/2014.

Ifahamike tu, kuwa mzunguko wa mwaka wa fedha wa Serikali katika utekelezaji wa Bajeti yake huanza ifikapo tarehe 1 Julai ya kila mwaka na huisha tarehe 30 Juni ya kila mwaka .Hivyo tunapozungumzia mwaka 2013/2014, hii inabainisha kuanzia tarehe1 Julai 2013 hadi tarehe 30 Juni 2014.

Unaweza ukajiuliza kwani ipo haja ya wananchi kujua mwelekeo wa kazi za Serikali yao ile hali  Bunge liliipokea na kuijadili Taarifa  ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2012/2013 na Mwelekeo kwa mwaka  wa fedha  2013/2014.

Kimsingi kila mwananchi anayo haki ya msingi ya kikatiba ya kujua nini Serikali itatekeleza katika kipindi cha mwaka wa fedha ujao, hii huimarisha misingi ya kidemokrasia kwa wananchi ya kuwahoji watu waliowaweka madarakani Kama wametekeleza yale waliyo waahidi.

Ni vyema pia  ikaeleweka kuwa Mwelekeo wa kazi zitakazofanyika kwa mwaka 2013/2014 umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010; Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Malengo ya Maendeleo ya Milenia na Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.

Nidhahiri kuwa Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali chache tulizonazo ili kutekeleza Miradi ya Maendeleo ya Kipaumbele ambayo itachochea ukuaji wa haraka wa uchumi.

Hakuna shaka kuwa Mwelekeo wa kazi za Serikali zitakazofanyika kwa mwaka 2013/2014 umezingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2010.

Hali ya Siasa; Ili Serikali itekeleze Ilani hiyo haina budi iimarishe Demokrasia na Wananchi washiriki kikamilifu kwenye siasa. Pia Viongozi wote wa Vyama vya Siasa wanao wajibu mkubwa wa kuendesha Siasa za kistaarabu zinazozingatia maadili ya Kitanzania na kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu ili amani, Utulivu na Umoja wetu ambao umewekezwa kwa miaka mingi tuweze kuuenzi.

Katika mwaka 2013/2014, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa itaandaa mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010, na kuboresha Baraza la Vyama vya Siasa. Hatua hizo zitazidi kuimarisha Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi; Katika mwaka 2013/2014, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaboresha Daftari la Wapiga Kura ambapo Awamu ya Kwanza itakamilika mwezi Desemba, 2013. Uboreshaji huo utawezesha kuchapishwa Kwa Daftari la Wapiga Kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2014. Kazi za awali za uchaguzi huo zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kupitia upya Kanuni za Uchaguzi zitakazojumuisha maoni ya wadau mbalimbali.

Ili kufanikisha uchaguzi huo, tayari Serikali imeshazitaka Halmashauri zote Nchini kuanza maandalizi mapema kwa kupitia na kuhakiki orodha ya Vitongoji, Vijiji na Mitaa.  Baada ya kuhakiki orodha hiyo, maombi mapya ya kugawa Vitongoji, Vijiji au Mitaa yatawasilishwa katika ngazi husika kabla ya tarehe 31 Desemba 2013 kwa kuzingatia Sheria na Taratibu zilizopo.

Mabadiliko ya Katiba; Kwa mwaka 2013/2014 serikali inaendelea kuratibu mchalato wa Katiba, kwa sasa tayari Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeshatoa Rasimu ya Katiba Mpya ambapo wananchi wanaendelea kuichambua ili wapate kutoa maoni yatakayo tupatia Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotokana na ridhaa ya Wananchi wenyewe ifikapo mwaka 2014.

Vitambulisho vya Taifa; Tarehe 07 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi Mfumo wa Utambuzi na Usajili wa Watu, Jijini Dar es Salaam.

Vilevile, tarehe 13 Februari 2013, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamedi Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, alizindua Zoezi hilo kwa upande wa Zanzibar. Kuzinduliwa rasmi kwa mfumo huo ni mwanzo wa utoaji wa Vitambulisho vya Taifa ambavyo vitasaidia kuwatambua na kuwahudumia Wananchi ipasavyo.

Katika mwaka 2013/2014, kazi ya Utambuzi na Usajili wa Watu katika Mikoa mbalimbali Nchini itaendelea sambamba na utoaji wa Vitambulisho kwa wale walioandikishwa na kuhakikiwa.

Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano; Katika kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo kwa haraka,  Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ulipitishwa na Bunge Mwaka 2011/2012.

Serikali imeona ni muhimu kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa kuanzisha Mfumo imara zaidi wa kupanga Vipaumbele, kufuatilia na kutathmini Utekelezaji wa Miradi ya Kimkakati ya Maendeleo.

Mfumo huo utasimamiwa na Chombo Maalum (President’s Delivery Bureau) chini ya Ofisi ya Rais, Ikulu, unazingatia uzoefu wa Nchi ya Malaysia.

Tayari zoezi la kuainisha maeneo sita ya kwanza ya kipaumbele yamefanyiwa uchambuzi wa kina kwa utaratibu unaojulikana kama Maabara (Labs).

Maeneo yaliyojadiliwa katika awamu ya kwanza ni Nishati na Gesi Asilia, Uchukuzi, Kilimo, Elimu, Maji na Kupanua wigo wa Mapato ya Serikali. Baada ya uchambuzi huo kukamilika, matokeo yake ikiwemo miradi iliyoandaliwa pamoja na Bajeti ya utekelezaji itawekwa hadharani ili kila Mtanzania ajue kitakachofanyika, kutoa maoni na kufuatilia kwa kina utekelezaji.

Ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na uwajibikaji wa kutosha katika kutekeleza vipaumbele vya Kitaifa, Chombo kitakachoanzishwa (President’s Delivery Bureau) kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kwamba kila Waziri wa Kisekta na Watendaji Wakuu wanawajibika kusimamia  utekelezaji wa miradi ya kipaumbele na pia kufanya tathmini za mara kwa mara kupima matokeo.

Katika Mwaka 2013/2014, kutafanyika uchambuzi wa kina wa maeneo mengine ya kipaumbele ambayo yatasaidia Serikali kupanga Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka 2014/2015

Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji; Sekta Binafsi na Uwekezaji inaendelea kupewa kipaumbele kwa kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini.

Katika utekelezaji wa Mpango Kazi huo, kwa mwaka 2013/2014 Serikali imeazimia kupunguza muda unaotumika kupitisha mizigo Bandarini na Mipakani kwa kuanzisha utaratibu wa kubadilishana taarifa zinazohusu mizigo kwa njia za kielektroniki kabla mizigo haijafika kwenye Vituo vya Forodha.

Maendeleo ya Sekta Binafsi na Uwekezaji; Serikali imekamilisha Mkakati na Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Sera ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP). Vilevile, Mwongozo wa Utendaji kwa ajili ya kutekeleza Sera, Sheria na Kanuni za Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi umekamilika.

Mikakati hiyo itaweza kuimarisha ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ili kuibua fursa zilizopo na kupata ufumbuzi wa changamoto za kisera, kisheria na kitaasisi zitakazokwamisha biashara na uwekezaji kwa mwaka 2013/2014.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi; Serikali inadhihirisha nia ya dhati ya kuwawezesha wananchi wake kiuchumi kwa kuendelea kuratibu na kufanya tathmini ya Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa mwaka 2013/2014, lengo ikiwa ni kuwa mifuko hiyo iwawezeshe walengwa.

Mifuko hiyo ni pamoja na Mfuko wa Uwezeshaji wa Mwananchi, Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, SIDO, SELF, Agriculture Input Trust Fund na Presidential Trust Fund.

Mifuko mingine ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Mfuko wa Udhamini wa Mikopo kwa Mauzo ya Nje na Mfuko wa Kudhamini Taasisi za Fedha Kutoa Mikopo kwa Miradi Midogo na ya Kati.

Katika  Makubaliano yaliyofikiwa baina ya Serikali na Taasisi za Fedha zilizoteuliwa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ni kwamba Taasisi hizo zikopeshe mara tatu zaidi ya dhamana iliyotolewa na Serikali.

Wananchi hatuna budi kuchangamkia fursa hizo kwani tangu tarehe 15 Agosti 2012, awamu ya tatu ya TASAF ilizinduliwa Mjini Dodoma na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Awamu hiyo itakayogharimu jumla ya Shilingi Bilioni 440 inatekeleza Mpango wa  Kunusuru  Kaya  Maskini  Zilizo Katika Mazingira Hatarishi. Mpango huo unalenga kuziwezesha kaya maskini kupata chakula na kujiongezea fursa za  kipato kwa kuzipatia fedha ili  kumudu mahitaji ya msingi kama vile lishe bora, huduma za afya na elimu.

Mpango huo utakaotekelezwa kwa awamu katika Halmashauri zote Tanzania Bara na Zanzibar, umeanza kwa utambuzi wa Kaya maskini katika Vijiji 20 vya Halmashauri ya Bagamoyo ambapo jumla ya Kaya 3,056 zimetambuliwa. Zoezi hilo linaendelea kwenye Halmashauri nyingine 13 na ifikapo Juni 2014, Halmashauri zote Nchini zitafikiwa.

Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa; Katika kudumisha amani, upendo, uzalendo na ukakamavu miongoni mwa vijana wa Tanzania, Serikali imeanza kuchukua Vijana watakaojiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa Sheria.

Mafunzo ya JKT Kwa mujibu wa Sheria yameanza mwaka huu kwa kuchukua Vijana 4,711 sambamba na Vijana 5,893 wa kujitolea wakiwemo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge vijana waliojiunga na mafunzo ya JKT mwaka huu. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuchukua vijana kwa ajili ya mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria. 

Kilimo cha Mazao ya Chakula na Biashara; Kila Mtanzania anatambua tukiwa na chakula cha kutosha ni dhahiri kuwa uzalishaji utaongezeka, Serikali katika kipindi cha mwaka 2013/2014 inaedelea kutekeleza mipango na mikakati ya kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara.

Utekelezaji huo unajikita katika Azma ya KILIMO KWANZA, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP), Mpango wa Utoaji wa Ruzuku ya Pembejeo na Dawa za Kilimo, Programu ya Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).

Programu Kabambe ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (Comprehensive Africa Agriculture Development Programme – CAADP) na kuboresha huduma za ugani na utafiti katika Sekta ya Kilimo.

Hatua nyingine ni pamoja na kuvutia Wawekezaji katika Sekta ya Kilimo, kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji, kuongeza fursa za upatikanaji wa zana bora za kilimo hasa matrekta, kuimarisha masoko na kurahisisha upatikanaji wa mitaji kutoka Vyombo vya Fedha, hususan kupitia Dirisha la Kilimo katika Benki ya Maendeleo Tanzania.

Ili kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya  mbolea na mbegu bora pamoja  na  tija  katika  uzalishaji  wa mazao ya kilimo,  Serikali imeboresha mfumo huo na kuanzia mwaka 2013/2014 ruzuku ya pembejeo za kilimo itatolewa kwa Mikopo kupitia Vikundi vya Wakulima badala ya utaraibu wa vocha kama ilivyokuwa awali.

Umwagiliaji; Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuimarisha kilimo cha umwagiliaji kwa kuanza ujenzi wa mabwawa matatu ya Idodi (Iringa); Manyoni (Singida) na Masengwa (Shinyanga Vijijini).

Kilimo cha matunda na mboga kina mchango mkubwa katika ukuaji uchumi, fursa za ajira, lishe na kupunguza umaskini. Kwa kuzingatia umuhimu huo.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itatoa mafunzo ya teknolojia za uzalishaji wa miche bora ya mazao ya bustani hususan kwa vikundi vya Vijana. 

Mwenendo Wa Bei Za Mazao Makuu; Ili kilimo kiwe na tija tayari Serikali imeangalia kwa umakini    mwenendo wa bei za mazao makuu ya biashara nchini ambao imekuwa ikibadilika mara kwa mara kwa kutegemea bei za Soko la Dunia.

Katika kudhibit hili katika mwaka 2013/2014 tayari Serikali kwa kushirikiana na Wataalam kutoka Bodi Sita za mazao inayafanyia kazi maoni ya wadau kuhusu kuanzisha Mfuko Maalum wa Kufidia Bei za mazao ya Pamba, Kahawa, Chai, Tumbaku, Korosho, Katani na Pareto.

Miundombinu ya Masoko ya Mazao; Serikali inatambua umuhimu wa kuendeleza miundombinu ya masoko ya mazao Kama moja ya mkakati madhubuti wa kumrahisishia mkulima kufikisha mazao yake sokoni na kuongeza bei ya mazao hayo.

Chini ya Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini, Serikali, imekamilisha usanifu na kutangaza  zabuni  za  ujenzi  wa  barabara  zenye  jumla ya Kilometa 210.8 katika Halmashauri za Mbulu, Njombe, Iringa Vijijini, Kahama, Lushoto, Rufiji, Songea Vijijini na Singida Vijijini.

Zabuni Kwa ajili ya ujenzi wa maghala mawili katika Halmashauri za Wilaya ya Iringa Vijijini na Njombe zimetangazwa na taratibu za ujenzi wa ghala katika Halmashauri ya Mbulu zinakamilishwa. Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa barabara na miundombinu mingine ya masoko Tanzania Bara na Zanzibar.

Maendeleo ya Sekta ya Mifugo; Watanznia ni wakulima na wafugaji, Katika mwaka 2013/2014 Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo (2011/2012 – 2015/2016). Programu hiyo inalenga kuwa na Sekta ya Mifugo ya kisasa itakayoongeza ukuaji wa Sekta kutoka Asilimia 2.3 hadi 4.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2016.

Sekta ya mifugo ili kuwa ya kisasa zaidi tayari Ujenzi wa Mfumo wa Utambuzi na Ufuatiliaji Mifugo unatarajiwa kuanza kazi mwezi Agosti mwaka huu.

Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi; Sekta ya Uvuvi itaimarishwa katika mwaka 2012/2013, kwa kundelea kupitia Sera ya Taifa ya Uvuvi ya mwaka 1997 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji, iendane na mabadiliko ya Kiuchumi na Kijamii yaliyojitokeza pamoja na kuzingatia maendeleo ya Sayansi na Teknolojia katika Sekta ya Uvuvi.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali pia itaendelea kusimamia shughuli za ukuzaji wa viumbe kwenye maji ikiwa ni pamoja na kuanzisha vituo vipya vya kuzalisha vifaranga vya samaki.

Ufugaji Nyuki; Uzalishaji wa Asali na Nta kwa miaka ya hivi karibuni unatupa moyo kwamba, Ufugaji wa Nyuki unaweza kuwa ni shughuli ya kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini.

Wafugaji Nyuki wa Tanzania wamepata soko la kuuza zaidi ya Tani 100 za Asali Nchini Ujerumani. Wajasiriamali wengi wamepata Alama ya Utambulisho wa Biashara (Barcode) kwa ajili ya kutambulisha Asali yao.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itafanya mapitio ya Sera ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 ili iendane na mabadiliko yanayotokea.

Maendeleo ya Viwanda ; mchango wa Sekta ya Viwanda kwenye Pato la Taifa unaedelea kuongezeka  kwa kufikia Asilimia 9.7 mwaka 2012.

Viwanda vinavyoendelea vizuri katika uzalishaji na kutoa mchango  mkubwa  ni  pamoja na viwanda vya saruji, bia, unga wa ngano,  vinywaji baridi, sukari, rangi, nyaya za umeme na usindikaji  wa  ngozi.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kubuni mikakati mipya yenye lengo la kuendeleza na kuviwezesha viwanda vidogo na vya kati vya wajasiriamali wa ndani pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya ukuaji wa viwanda Nchini.

Serikali imedhihirisha hili kwa  kuhamasisha Usindikaji wa Ngozi hapa Nchini na kuongeza thamani ya zao la ngozi, kwa kuongeza Ushuru wa Ngozi Ghafi zinazouzwa nje ya Nchi kutoka Asilimia 40 hadi 90 kwa kilo kuanzia  Julai 2012.

Ongezeko hilo linathibitisha kwamba hatua zilizochukuliwa na Serikali zimeongeza usindikaji wa ngozi na kupanua wigo wa uzalishaji wa mazao ya ngozi Nchini. Serikali itaendelea kusimamia mafanikio hayo na kuchukua hatua zaidi zitakazoongeza usindikaji wa ngozi hapa Nchini.

Sekta ya Utalii ; Serikali imeandaa Mpango Mkakati wa kuifanya Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Mtwara na Tanga kuwa vituo vya utalii wa fukwe. Mikoa hiyo ina fukwe za kipekee zinazovutia watalii na pia zinafaa kwa uwekezaji wa kitalii.

Sekta ya Madini;  wachimbaji wadogo wa madini wana mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi yetu. Ili kuwaendeleza wachimbaji hao, Serikali imekamilisha Mkakati, Mpango Kazi na Programu ya Mafunzo pamoja na kuwatengea maeneo  wachimbaji  wadogo  kwa  mujibu  wa Sheria.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaimarisha ukaguzi kwenye uzalishaji na biashara ya madini pamoja na kuimarisha STAMICO ili itekeleze majukumu yake kikamilifu.

Hali ya ajira nchini; Serikali inatambua umuhimu wa kuongeza fursa za ajira kwa vijana wengi wanaoingia kwenye soko la ajira  kila  mwaka.

Ili kuongeza kasi ya ukuaji wa ajira, Katika mwaka 2013/2014 Serikali inakamilisha Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ajira kwa Vijana.  Programu hiyo ya miaka mitatu itaongeza fursa za Vijana 301,100 kuweza kujiajiri au kuajiriwa.

Msukumo zaidi utawekwa katika Miradi ya Kilimo, Viwanda Vidogo, Maeneo Maalum ya Kiuchumi (EPZ na SEZ), Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Sambamba na hatua hiyo, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa Vyuo vya Ufundi na vya Elimu ya Juu ili kuwawezesha kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.

Ardhi; pamoja na Nchi yetu kuwa na ardhi ya kutosha na inayofaa kwa Kilimo na uwekezaji mwingine, bado zoezi la uwekaji mipaka, kupima na kutoa Hati kwa matumizi mbalimbali halijakamilika.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za ardhi (Geodetic Control Network) na kurahisisha upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Mfumo huo utakaounganisha Ofisi za Ardhi Nchini unategemewa kukamilika mwaka 2014 na utaiwezesha Tanzania kuwa na kumbukumbu sahihi za ardhi.

Nishati; Serikali imeendelea kusogeza huduma ya nishati ya umeme karibu na Wananchi ili kuharakisha   maendeleo yao.

Katika  kutekeleza  azma  hiyo, gharama  za  kuunganisha  umeme  wa  njia  moja  kwa  wateja  wadogo Vijijini na  Mijini  zimepunguzwa kwa wastani wa kati ya  Shilingi Milioni 1,311,000 na Shilingi 114,000.

Hatua hiyo imewezesha wananchi wengi kumudu gharama ya kuunganisha umeme na kuongeza kasi ya usambazaji umeme Nchini.

Sekta ndogo ya Gesi Asilia inakua kwa kasi ambapo hadi kufikia Januari 2013, kiasi cha futi za ujazo Trilioni 35 zimegundulika Nchini. Ili kusimamia rasilimali hiyo muhimu, Serikali imeandaa rasimu ya Sera ya Gesi Asilia na kupata maoni kutoka kwa wadau

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mradi wa bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na ujenzi wa Mitambo ya kuzalisha umeme wa Kinyerezi (MW 200).

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ;  Serikali  inaendelea kutekeleza  Mradi  wa ujenzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wenye Awamu Tano. Awamu  ya  Kwanza  na ya Pili ya Ujenzi wa Mkongo huo wenye urefu wa Kilomita 7,560 imekamilika na kuunganisha Makao  Makuu  ya  Mikoa  24  ya  Tanzania  Bara.

Kazi ya   kuunganisha Kisiwa cha Unguja na Mkongo huo kupitia Dar es Salaam itakamilika mwaka huu.

Tunaelewa kuwa Tanzania sio kisiwa, hivyo Tanzania pamoja na Nchi zote Duniani kupitia Umoja wa Mawasiliano Duniani (ITU) zimekubaliana kusitisha matumizi ya teknolojia ya utangazaji kutoka Mfumo wa Analojia na kuanza Matumizi ya Teknolojia ya Dijitali ifikapo Juni 2015.

Hapa  Nchini, usitishaji wa matumizi ya mfumo wa mitambo ya analojia umeanza kutekelezwa tarehe 31 Desemba 2012 kwa awamu kwa kuanzia  na  Jiji  la  Dar es Salaam.

Katika mazingira ya sasa, sisi kama Taifa siyo  vyema kubaki kama kisiwa wakati  tumeunganishwa  na  mifumo  ya  teknolojia ya kidunia. 

Pamoja na changamoto zake, ni busara tuendelee na mabadiliko hayo sasa kuliko kusubiri na hatimaye tukajikuta tuko nyuma na nje ya mstari.

Sayansi na Teknolojia; katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kueneza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kupanua matumizi yake katika maeneo mbalimbali Nchini na Nchi jirani.

Vilevile, Serikali itaendelea na zoezi la kuhama kutoka katika mfumo wa analojia kwenda dijitali na kupanua na kuboresha Mtandao wa Huduma za Mawasiliano ya simu na intaneti Nchini.

Barabara na Madaraja ; Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa  katika  kujenga, kukarabati na kuboresha mtandao wa Barabara Kuu, za Mikoa, Wilaya pamoja na za Vijijini ili kuwa na mtandao bora wa barabara utakaowezesha Wananchi, hasa Wakulima kusafirisha  mazao  yao  hadi  kwenye  Masoko ya ndani na nje ya Nchi.

Serikali ya Awamu ya Nne imedhamiria kujenga na kukamilisha ujenzi wa Madaraja makubwa na ya kisasa mawili ambayo ni Daraja la Mto Malagarasi  na  Daraja  la  Kigamboni.

Ujenzi wa Daraja la Mto Malagarasi unaojumuisha ujenzi wa Daraja kubwa lenye urefu wa Meta 200 na Madaraja mengine madogo katika Bonde la Mto Malagarasi  unaendelea vizuri. Hadi mwezi Machi mwaka huu, Mkandarasi amekamilisha ujenzi kwa  Asilimia 85.

katika mwaka 2013/2014 Serikali itajenga Barabara Kuu kwa kiwango cha lami zenye urefu wa Kilometa 495 na kukarabati Barabara zenye urefu wa Kilometa 190 na Madaraja 11.

Serikali pia, itajenga barabara za Mikoa za lami zenye urefu wa Kilometa 54.3 na kukarabati Kilometa 855 kwa kiwango cha changarawe na Madaraja 36. Aidha, matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum ya Barabara Kuu na za Mikoa yataendelea kufanyika katika kipindi kijacho.

Usafiri wa Jiji la Dar es Salaam; msongamano wa magari katika barabara za Jiji la Dar es Salaam ni moja ya changamoto ambayo Serikali inaendelea kuifanyia kazi.

Katika mwaka 2013/2014 Serikali itaendeleza Jitihada za kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa   kuendelea kujenga miundombinu zaidi ya barabara mpya za kuingia na kutoka katikati ya Jiji; kuboresha  usafiri wa Treni ya Abiria; kuharakisha utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART); na kuimarisha usimamizi wa Sheria za Usalama Barabarani.

Serikali tayari  imeunda Kamati maalum ya wadau wa usafiri Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuchambua, kuanisha na kushauri mipango na mikakati ya baadaye ya kuboresha huduma hiyo ili iwe endelevu na salama.

Usafiri  wa Reli ya Kati na TAZARA; Serikali itaendelea  kuboresha miundombinu ya reli ya kati Kwa kujenga na kukarabati maeneo mbalimbali ili kuiwezesha kupitika wakati wote.

Katika mwaka 2013/2014 Upembuzi yakinifu wa reli ya kutoka Dar es Salaam hadi Rwanda na Burundi na kutoka Arusha hadi Musoma unatarajiwa kuanza.

Tayari tangu mwezi Machi 2012, Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China  zilitia  saini  Itifaki ya 15 ya kuboresha Reli ya TAZARA.

Hatua hizi zikikamilika zitaboresha kwa kiwango kikubwa usafiri wa Reli ya TAZARA.

Bandari; Serikali inachukua hatua za kuongeza uwezo na ufanisi wa bandari zake kwa kutekeleza Mpango Kabambe wa Mamlaka ya Bandari.

kutokana na nafasi ya Nchi yetu kijiografia na ongezeko kubwa la biashara na uingizaji wa mizigo ya hapa Nchini na Nchi jirani ambazo hazina bandari, uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam kuhimili ongezeko hilo unapungua.

Pamoja na jitihada zinazoendelea za kupanua miundombinu ya bandari hiyo, Serikali imeona umuhimu wa kuwa na Bandari mpya ya Bagamoyo ili isaidiane na Bandari zilizopo kukabiliana na ongezeko hilo.

Kwa mantiki hiyo mnao mwezi  Machi mwaka huu , Serikali ya Tanzania na China zimetia saini makubaliano ya kujenga Bandari mpya ya Bagamoyo ambayo itakuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Makubaliano hayo yanajumuisha pia ujenzi wa eneo huru la biashara na miundombinu mingine muhimu ikiwemo reli itakayounganisha Bandari ya Bagamoyo na Reli ya Kati na ya TAZARA pamoja na barabara ya lami kutoka Bagamoyo hadi Mlandizi.

Usafiri wa Anga;  katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Upanuzi na Uboreshaji wa Viwanja vya Ndege. Kazi zitakazofanyika ni pamoja na Upembuzi Yakinifu na usanifu wa kina wa ukarabati kwa kiwango cha lami wa njia za kuruka na kutua ndege kwa viwanja vya Iringa, Kilwa Masoko, Ziwa Manyara, Musoma, Mtwara, Njombe, Songea, Singida na Tanga.

Ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege kwa kiwango cha lami katika kiwanja cha Ndege cha Tabora umekamilika na kazi za ujenzi zinazoendelea katika kiwanja cha Kigoma zinatarajiwa kumalizika mwaka huu.

Elimu ya Msingi; Serikali ilianza kutekeleza Programu kubwa za kuendeleza elimu Nchini mwaka 2001 kwa lengo la kuongeza idadi ya Wanafunzi wa rika lengwa wanaojiunga na shule na kuboresha elimu.

Utekelezaji wa Awamu ya Kwanza na ya Pili ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM I & II) umeleta mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu, kuandikisha Wanafunzi wa rika lengwa na kupunguza pengo la uandikishaji kati ya Wanafunzi wa Kike na wa Kiume.

Katika mwaka 2013/2014 serikali itaendelea kutekeleza atekeleza Awamu ya Tatu ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM III) unaolenga kuboresha elimu kwa kuongeza idadi ya Walimu, vitabu vya ziada na kiada na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Elimu Maalum;  Serikali inaendelea kuweka msukumo  wa  kipekee katika  kutoa  Elimu Maalum  kwa watu wenye  Ulemavu  wakiwemo  wenye  Ulemavu  wa  Ngozi, Uoni Hafifu na Usikivu.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa Elimu Maalum hususan baada ya kupata takwimu sahihi za walemavu kutokana na Sensa ya Watu  na Makazi ya mwaka 2012.

Elimu ya Juu; Serikali inatekeleza Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Juu kwa kupanua na kuongeza Taasisi za Elimu ya Juu za Serikali na Binafsi.

katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kuongeza kiasi cha fedha kwa ajili ya Mikopo ya Elimu ya Juu na kuimarisha usimamizi wa  urejeshaji wa mikopo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kunufaika.

Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya Nchini; Serikali imeweka jitihada kubwa za kuhakikisha kwamba Vituo vya Utoaji wa Huduma za Afya katika ngazi zote Nchini vinapatiwa dawa muhimu na vifaa vya Teknolojia ya kisasa vya kuchunguza na kutibu magonjwa.

Udhibiti wa Maambukizi ya Malaria na UKIMWI; katika mwaka 2012, Serikali ilifanya Utafiti kuhusu Viashiria vya UKIMWI na Malaria. Taarifa ya matokeo ya utafiti huo inaonesha kuwa kiwango cha Malaria Nchini kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano kimepungua kutoka Asilimia 18 mwaka 2007 hadi Asilimia Tisa mwaka 2012.

Ni dhahiri kupungua kwa kiwango cha Malaria Nchini ni jitihada za kipekee zinazo endelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Nne kwa kushirikiana na Wananchi na Washirika wa Maendeleo kupitia Kampeni mbalimbali za Kudhibiti Malaria.

Kuhusu UKIMWI, Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaanza kutekeleza Mkakati Mpya wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013 hadi 2017 unaolenga kuwa na Sifuri tatu, yaani Kutokuwa na Maambukizi Mapya; Kukomesha Vifo Vitokanavyo na UKIMWI na Kuondoa Kabisa Unyanyapaa na Ubaguzi.

Lengo hilo litatimia iwapo sote tutabadili tabia zinazosababisha maambukizi mapya.

Lishe; tayari Serikali imesha chukua hatua thabiti za kupambana na utapiamlo hususan udumavu unaoathiri watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Serikali imezindua Mkakati wa Kitaifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011 hadi 2014/2015. Mkakati huo umeanza kutekelezwa kwa kuandaliwa Mpango wa Utekelezaji ulioainisha gharama na majukumu ya kila mdau katika kupunguza Utapiamlo Nchini.

Vilevile, Serikali inaendelea na zoezi la kuhuisha Sera ya Usalama wa Chakula na Lishe ya mwaka 1992 ili iendane na Mkakati wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2010/2011  hadi 2014/2015.

Huduma ya Maji Vijijini; Serikali inatambua kuwa upatikanaji wa maji ya uhakika na ya kutosha kwa wananchi Vijijini bado ni changamoto inayohitaji nguvu zaidi na mbinu mpya kwa kuzingatia ongezeko kubwa la watu pamoja na mabadiliko ya Tabianchi.

Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imetenga na kupima maeneo ya vyanzo vya maji na kuyawekea mipaka ili kuzuia uchafuzi na uharibifu wa vyanzo hivyo.  Aidha, Vituo mbalimbali vya kuchotea maji vimeainishwa katika Halmashauri 122 na kuwekwa kwenye ramani ili vifahamike.

Katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miradi ya maji Mijini na Vijijini pamoja na kujenga mabwawa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na mifugo hususan katika maeneo kame.

Vita Dhidi ya Rushwa;  Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la rushwa kwa kuelimisha Umma  kuhusu athari za Rushwa, kuziba mianya ya  rushwa  na  kuwasihi  Wananchi  kujiepusha  na vitendo vya rushwa.

Katika mwaka 2013/2014, TAKUKURU itaendelea na uchunguzi wa tuhuma zilizopo na mpya zitakazojitokeza, kuendesha Kesi nyingine zilizopo Mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa kutokana na kukamilika kwa chunguzi mbalimbali.

Dawa za Kulevya; Biashara na matumizi ya Dawa haramu za Kulevya bado ni tatizo Nchini. Hali hii inadhihirishwa na idadi kubwa ya watumiaji walio mitaani na wale wanaojitokeza kupata tiba.

katika mwaka 2013/2014, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini na kuandaa Mkakati wake wa Utekelezaji.

Ustawishaji Makao Makuu Dodoma; katika mwaka 2013/2014, itaendelea kuustawisha Mji wa Dodoma kwa kukamilisha ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo ya Kisasa, Chang'ombe, Kikuyu na Area A.

Vilevile, itaendelea na ujenzi wa Barabara kwa kiwango cha lami, usambazaji wa umeme wa msongo mkubwa pamoja na usambazaji wa mabomba ya maji safi katika eneo la Uwekezaji la Njedengwa.

Pia, itapima Viwanja vipya 4,476 katika maeneo ya Nzuguni, Mkonze, Ndachi na maeneo ya Viwanda. Pamoja na kazi hizo, kazi iliyoanza ya kuimarisha utendaji wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma itaendelea.

Bajeti ya mwaka 2013/2014; kama nilivyoeleza hapo awali, bajeti ya mwaka 2013/14 imelenga kutekeleza Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa miaka mitano; Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010; Awamu ya Pili ya Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA II); Malengo ya Maendeleo ya Milenia 2015; na kuanza kutekeleza maeneo ya vipaumbele yaliyoainishwa katika Labs. Madhumuni ya mipango na mikakati hii ni kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Mwezi Juni mwaka huu, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha makadirio ya bajeti ya mwaka 2013/2014 ambapo utekelezaji wake umeanza tayari tangu tarehe 1 Julai mwaka huu, hivyo ni jukumu la kila mtanzania kutimiza wajibu wake ili kuhakikisha mwelekeo wa kazi za Serikali katika kipindi cha 2013/2014 zinatekelezwa kikamilifu.

MWISHO

FilenameMAKALA-MWELEKEO.doc
FilesizeEmpty
Filetypedoc (Mime Type: application/msword)
Creatorfrancisca.swai
Created On: 06/30/2013 11:00
ViewersEverybody
Maintained byEditor
Hits1911 Hits
Last updated on 10/30/2014 11:17
Homepage
CRC Checksum
MD5 Checksum
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved