Logo
Details for “Hakuna Kuomba Kura kwa Kufunika Kiganja” – Sheria Mpya ya Gharama za Uchaguzi
PropertyValue
Name“Hakuna Kuomba Kura kwa Kufunika Kiganja” – Sheria Mpya ya Gharama za Uchaguzi
Description


“Hakuna Kuomba Kura kwa Kufunika Kiganja” – Sheria Mpya ya Gharama za Uchaguzi

Katika Mkutano wake wa 18, uliofanyika mwezi Januari 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya kuweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu Mapato, Matumizi  na Gharama za Kampeni na Uchaguzi wa Vyama vya  Siasa na Wagombea (Election Expenses Act 2009).  Sheria hiyo ilisainiwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 17 Machi, 2010 ili iweze kutumika.

Kutungwa kwa sheria hii ni kutokana na nia ya dhati  ya kukuza demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini, aliyoionesha Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete wakati akizindua Bunge  tarehe 30 Desemba 2005 huko Dodoma , kwa  kusema;

“Taifa tumeanza kuwa na fikra kuwa vyama vya siasa vimeweza kununuliwa kwa fedha. Kama hii ni kweli , lazima tuwe waangalifu sana na kuhakikisha kuwa Taifa letu haliwezi hata siku moja kuwekwa rehani kwa fedha  ili mradi tu mtu  fulani anataka kuingia Ikulu. Lakini siyo sahihi hata kidogo kununua  ushindi . Lazima tulipige vita jambo hili, kwa hali hii tunapashwa  kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi. Hali  hii itatufanya tuwe na muafaka wa wazi wa kisheria kwa chama  au mgombea kupata fedha kwa matumizi ya kampeni, na kwa matumizi ya wazi na halali na udhibiti wake.”

Mheshimiwa Rais alibainisha kuwa wenye fedha huwa na maslahi yao na hutaka kuchagua mtu atakayelinda maslahi yao.  Alisema kuwa udhibiti wa matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi ni muhimu lakini pia udhibiti huo lazima ufanyike kwa umakini mkubwa kwani ukidhibiti sana watu wanapitia mlango wa nyuma.

Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa  ambayo ni nyumba ya demokrasia, chini ya Msajili wa Vyama vya Siasa Bw. John Tendwa, iliandaa muswada wa sheria ya kuweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu Mapato , Matumizi  na Gharama za Kampeni na Uchaguzi wa Vyama vya  Siasa na Wagombea (Election Expenses Act 2009).

Ili kuhakikisha kuwa Sheria hii inapata ushiriki wa kutosha kutoka kwa wadau wote, Serikali kwa kupitia gazeti la serikali ilitoa Tangazo No. 50 la tarehe 11 Desemba 2009 na kutangaza muswada No. 17 wa Serikali kuhusu kuweka utaratibu wa kusimamia na kuratibu mapato na matumizi na gharama za kampeni na uchanguzi wa Vyama vya Siasa na mgombea(Election Expenses Act 2009).

Baada ya kukusanya maoni kutoka kwa mtu mmoja mmoja, Taasisi zisizo za Serikali  na vyama vya siasa  na hatimaye kuwasilishwa kwa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba. Muswada uliweza kujadiliwa tarehe 11 Februari 2010 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano na kupitishwa rasmi kama Sheria itakayoanza kutumika katika Uchaguzi Mkuu  Oktoba 2010.

Katika kuboresha maoni ya wadau mbalimbali, kabla  ya Wabunge kupitisha Sheria hiyo lakini pia walishiriki katika kuiandika sheria hiyo kwa wabunge wa Upinzani na Chama tawala kwa kushirikiana  bila kujali itikadi za vyama vyao bali kwa kuweka maslahi ya Taifa mbele, lengo likiwa ni kuzuia kabisa matumizi ya fedha chafu katika kujipatia uongozi  wa kisiasa katika ngazi zote.

Ni vyema Watanzania wakaelewa Sababu kuu na Madhumuni ya  kutungwa kwa Sheria ya Gharama za uchaguzi.

Sababu kuu za kutunga Sheria ya Gharama za uchaguzi ni kuweka utaratibu wa kisheria wa kusimamia mapato na matumizi ya gharama za Kampeni za Vyama  vya siasa na wagombea.

Sababu nyingine ni kuweka utaratibu utakaowezesha serikali kuchangia gharama za uchaguzi na kampeni kwa vyama vya siasa.

Vilevile utaratibu wa kisheria wa kuratibu zawadi, misaada na michango itakayotolewa na wagombea wakati wa Kampeni za uchaguzi.

Lakini pia Sheria hii inalenga katika kuweka utaratibu wa kudhibiti matumizi ya fedha wakati wa Kampeni za Uchaguzi na kuweka mfumo wa uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma .

Pamoja na mambo mengine, Sheria hii inabainisha utaratibu wa adhabu kwa watakaokiuka  masharti yaliyomo  kwenye Sheria yenyewe.

Madhumuni ya Sheria hii ya Gharama za Uchaguzi ni kuweka mazingira yatakayowezesha kuwepo kwa uwazi zaidi katika matumizi ya fedha zitakazotengwa kwa ajili ya Kampeni.

Sheria itasaidia kudhibiti matumizi ya fedha na vitendo vya rushwa kwenye Kampeni za Uchaguzi kwa kuwepo kwa utaratibu wa fedha zitakazotumika katika Kampeni na Uchaguzi ndani ya vyama vya siasa katika uteuzi wa mgombea.

Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa katika nchi nyingi kama vile: Ujerumani, Msumbiji, Zambia, Kenya , Uingereza , Ufaransa na Malawi imedhihirika kuwa kukosekana kwa sheria ya udhibiti wa matumizi ya fedha wakati wa kampeni na uchaguzi, hakuleti usawa katika mfumo mzima wa vyama vya siasa.

Ndani ya vyama vya siasa vyenyewe, wale wenye mifuko ya fedha wana sauti kubwa  ndani ya vyama, hivyo hii ni pamoja na uongozi ndani ya vyama na uteuzi wa wagombea kwa nafasi za juu za kiserikali.

Akichangia mswada wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi Bungeni, Mbunge wa Ukerewe, Mhe. Getrude Mongela alionyesha kusikitishwa kwake kwa hali ilivyo sasa katika kampeni na chaguzi za hapa nchini, akisema kwa kawaida  kiganja cha mtu anayeomba huwa chini  na anayetoa huwa juu kwa kumpa mwombaji, lakini sasa anayeomba anafunika kiganja cha anayemwomba.

“Wakati nagombea ubunge kwa mara ya kwanza nilikuwa ni mwanafunzi tu wa kutoka Chuo Kikuu na nilikuwa nagombea ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki, sikuanzia katika Bunge la Tanzania, lakini niliomba kura  kwa wabunge  kwa mikono yangu miwili wakati ule ilikuwa pale katika ukumbi wa Karimjee Hall, na bila hiyana wabunge walinichagua kuwa mbunge, kama wangetaka niwafunike viganja nisingeweza kwa maana ya kuwapa chochote lakini walichoangalia ni uwezo wangu wa kujieleza na kujiamini kwangu kwa jinsi ninavyoweza kuwatumikia wananchi’’ alisema Mhe. Mongela.

Kwa upande mwingine Chama chenye fedha nyingi au vyanzo vingi vya fedha kina nafasi  kubwa na uwezo mkubwa dhidi ya vyama vingine  ambavyo havina fedha na uwezo kidogo wa kupata fedha. Hali hii huleta tofauti kubwa baina ya vyama hivyo wakati wa ushindani  wa kisiasa ndani ya Kampeni na Uchaguzi.

Ni vyema ikaeleweka kuwa Sheria hii ya  Kudhibiti Matumizi ya Fedha wakati wa Kampeni na Uchaguzi  inazingatia vigezo vya  mazingira ya nchi yetu ya kisiasa, kama  ilivyo katika nchi nyingine zote duniani lakini vigezo vikuu vya mazingira ya kisiasa  ambavyo sheria  hiyo imejikita  ni katika mambo kadhaa.

Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na ukomo wa michango, michango inayozuiliwa, ukomo wa matumizi, muda mwafaka wa kampeni, kutangaza kwa mali au fedha za kampeni na uchaguzi (public disclosure), mchango wa Serikali.

Sheria ya Gharama za Uchaguzi imegawanyika katika sehemu nane. Sehemu ya Kwanza inaweka masharti kuhusu mambo ya utangulizi ambayo  ni jina, tarehe ya kuanza kutumika  kwa sheria hii katika Tanzania Bara na Zanzibar  na vilevile inaweka tafsiri ya misamiati itakayotumika.

Sehemu ya pili inaorodhesha kazi za Msajili wa Vyama vya Siasa ikiwemo mamlaka ya kusimamia na kukagua gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa  na mwenendo wa wasimamizi wa uchaguzi.

Sehemu  ya Tatu inahusu masharti kuhusu fedha zitakazotumika kwa ajili ya uchaguzi, maana ya gharama za uchaguzi , uchaguzi ndani ya Vyama vya Siasa, gharama  ambazo Vyama vya Siasa vinapaswa kutumia wakati wa uchaguzi, masharti  kwa Vyama vya Siasa na wagombea kutoa taarifa kuhusu gharama zitakazotumika wakati wa uchaguzi.

Aidha, sehemu hii inatoa taarifa kuhusu michango au misaada inayotolewa na kupokelewa na vyama vya siasa, kuzuia fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya Kampeni za Uchaguzi, Matumizi ya gharama kwa vyama na Taasisi za kiserikali  wakati wa kutoa elimu ya Kampeni na chaguzi za kisiasa.

Sehemu ya Tano inahusu masharti  yanayokataza baadhi ya matumizi ya fedha kama gharama za kampeni na uchaguzi. Matumizi  hayo ni yale yanayohusu  gharama kwa vitendo vinavyozuiwa  au kuwa haramu wakati wa kampeni na uchaguzi.

Sehemu ya sita ya Sheria ya Gharma za Uchaguzi  inapendekeza makosa ya  ujumla  pamoja na adhabu zinazoweza kutolewa kwa kukiuka masharti ya Sheria hii.

Sehemu ya saba inaweka masharti  kuhusu haki ya mgombea wa Ofisi ya Rais na Makamu wa Rais kutumia vyombo vya habari, wajibu wa Serikali na vyombo vya habari kumuwezesha kutumia  haki  hiyo.

Aidha, sehemu hii inaipa Serikali wajibu wa kutumia  vyombo vya ulinzi  na usalama ili kuhakikisha kwamba Vyama vya Siasa, wagombea wao na  wapiga kampeni wanafikia wapiga kura bila ubaguzi wala  kupewa vitisho.

Sehemu ya Nane ya Sheria inafanya marekebisho katika Sheria ya Vyama  vya Siasa ili kuoanisha masharti  ya Sheria hiyo. Marekebisho ya msingi ni kuongeza  kifungu cha 13A katika Sheria ya Vyama vya Siasa kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha Msajili wa Vyama vya Siasa kupata taarifa juu ya mgombea au chama cha siasa kinachojihusisha na vitendo vya ukiukaji wa masharti ya Sheria hii wakati wa kampeni za uchaguzi. Aidha, kifungu hicho kinaweka utaratibu utakaowezesha kuhifadhi utambulisho wa watoa taarifa (whistle blowers).

Ifahamike kuwa dhana ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi  imetokana na maamuzi ya Umoja wa Nchi za Kiafrika (African Union – AU) ya kupiga vita  rushwa na kuzuia rushwa wakati wa kampeni na uchaguzi. yaliyofanyika Jiini Maputo Msumbiji mwaka 2003.

Maamuzi hayo yalitaka nchi wanachama kutunga sheria zitakazosimamia udhibiti  wa matumizi ya  fedha wakati wa kampeni na uchaguzi na kuzitaka nchi hizo  kutunga sheria yenye kujikita katika vifungu vikuu viwili ambavyo ni : Vifungu  vinavyokataza matumizi na upatikanaji wa fedha haramu kwa vyama vya siasa pamoja na kuweka kifungu chenye kuonyesha uwazi (transparency) na uwajibikaji kwa vyama vya siasa wakati wa uchaguzi na kampeni.

Hakuna anayeweza kupinga kuwa rushwa katika demokrasia changa huondoa uwajibikaji katika Serikali, hali ambayo pia hukomaza rushwa ndani ya vyama vya siasa ambapo katika hali hii uwajibikaji katika serikali hupungua hasa kwa nchi isiyokuwa na  sheria ya kudhibiti  gharama za uchaguzi na kampeni.

Tanzania imefanya uamuzi wa kijasiri kwani  nchi nyingi za  Bara la Afrika hazina sheria ya uwazi na udhibiti  wa matumizi ya   fedha wakati wa  kampeni na uchaguzi .  Hivyo, kwa nchi zilizo kusini kwa Afrika (SADC) Tanzania imeamua kukuza demokrasia nchini kwa kuwa na sheria hiyo tofauti na nchi nyingine.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mheshimiwa Philpo Marmo wakati akiwasilisha hoja ya Sheria mpya ya Gharama za Uchaguzi  aliwabainishia Wabunge kuwa pamoja na kutungwa sheria hii ili iweze kusimamiwa  na kutekelezwa  kwa umakini inahitaji kuungwa mkono na wadau wote kwa vitendo lakini pie Serikali ipo tayari kuiboresha kwa kadri itakavyoona kuna umuhimu.

“Sheria hii mpya ya Gharama za Uchaguzi ili ifanikiwe  inahitaji  utashi wa kisiasa, elimu kwa umma  kutolewa juu ya Sheria hii ambapo Serikali itaiandika katika lugha ya Kiswahili ili kila mwananchi aielewe lakini  pia  Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wa Vyama vya Siasa vya Upinzani na Chama Tawala kuunga mkono Sheria hii ili kuzuia matumizi ya fedha chafu katika Kampeni na Uchaguzi.” Alisisitiza Marmo.

MwishoFilenameHakuna Kuomba Kura kwa Kufunika Kiganja.docx
FilesizeEmpty
Filetypedocx (Mime Type: application/octet-stream)
Creatorfrancisca.swai
Created On: 08/27/2013 11:49
ViewersEverybody
Maintained byEditor
Hits1279 Hits
Last updated on 10/30/2014 12:11
Homepage
CRC Checksum
MD5 Checksum
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved