Logo
Details for Upungufu wa chakula nchini unaepukika Elimu ya Usalama wa Chakula kwa wananchi ikitolewa.
PropertyValue
NameUpungufu wa chakula nchini unaepukika Elimu ya Usalama wa Chakula kwa wananchi ikitolewa.
Description

Upungufu wa chakula nchini unaepukika Elimu ya Usalama wa Chakula kwa wananchi ikitolewa.

kilimo ni moja ya Sekta muhimu katika uchumi na maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 74 ya Watanzania na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwa miaka yenye mvua za kutosha. Mara nyingi uwepo wa mvua za kutosha ni dalili ya uwepo wa mavuno mazuri hivyo mavuno mazuri hupelekea utoshelevu wa chakula.

Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake ya mwaka 2014/2015 Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza alisema, katika mwaka 2013/2014 unaonesha kuwepo kwa ziada ya tani milioni 2.2 za chakula. Ongezeko hilo, ambalo limetokana na kuwepo kwa mvua za kutosha na juhudi za Serikali za kuboresha uzalishaji kwa kutoa ruzuku ya pembejeo kwa wakulima, lilileta utoshelevu wa chakula nchini kwa asilimia 118.

Pamoja na kuwepo kwa ziada ya chakula kwa msimu wa mwaka 2013 laikini, katika kipindi cha kuanzia Julai, 2013 hadi Aprili 2014 Hifadhi ya Taifa ya Chakula NFRA ilitoa jumla ya tani 32,711 ili kukabiliana na upungufu wa chakula. Hadi kufikia tarehe 02 Aprili 2014 akiba katika maghala yote ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula -NFRA ni tani 194,747 za nafaka.

Akihojiwa  hivi karibuni na kituo kimoja cha Radio cha hapa nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Chakula, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika Bw. Karim Mtambo alibainisha kuwa kwa sasa nchi yetu  mikoa yote ina kiwango cha chakula kwa asilimia 93.

“Katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu hatujawahi kuwa na utoshelevu wa chakula kama ilivyo sasa kwani katika miaka yote kiwango cha utoshelevu wa chakula kimekuwa ni kati ya asilimia 102 na 105 lakini hivi sasa nchi yetu ina utoshelevu wa chakula wa asilimia 125 huku viwango vya kimataifa ni utoshelevu wa chakula wa asilimia 120” alisisitiza Mtambo.

Mtambo alifafanua kuwa Serikali imewaruhusu wakulima kuuza chakula sehemu yoyote ile ndani na nje ya nchi kwa kuwa chakula kipo cha kutosha ambacho kimevuka kiwango vya utoshelevu wa chakula cha kimataifa ambacho ni asilimia 120.

Pamoja na utoshelevu wa chakula hicho ni dhahiri kuwa uhifadhi wa chakula hicho umekuwa ni changamoto hali inayopelekea usalama wa chakula kuwa mdogo kwa kuwa wakulima wengi wanamwaga mazao ya chakula kama mahindi chini hawana elimu ya kutosha juu ya matumizi ya vihenge bora/vya kisasa na madawa ili kuweza kuzuia chakula kisibunguliwe na wadudu. Hali hii inachangia sana upungufu wa chakula kutoepukika nchini kwa kuwa tunavuna kiwango cha kutosha cha chakula lakini elimu duni ya usalama wa chakula hicho ni duni.

Mtambo anajaribu kufafanua juhudi za serikali za kunusuru chakula hicho kuwa tayari serikali imeanza kukarabati maghala ya chakula yaliyopo mikoani na Wilayani. Aidha Mnunuzi Mkuu wa chakula hicho ambaye ni Hifadhi ya Taifa ya Chakula –NFRA anaendelea kununua chakula hicho kilichopo hapa nchini.

Suala la msingi la kujiuliza ni, je wananchi wanayo elimu ya kutosha juu ya usalama wa chakula kwa kaya zao kwa mantiki ya kujua ni kiwango gani cha chakula kaya inapaswa kutumia katika msimu mzima wa chakula? Elimu ikitolewa usalama wa chakula upungufu wa chakula unaepukika kwani wananchi watajua ni kiasi gani wanaweza kuuza lakini pia wanapaswa kuhifadhi kwa ajili ya chakula kwa kaya zao lakini bila elimu hii jamii nyingi zinaishia kuuza chakula chote ili kutatua matatizo ya familia zao.

Kila mwaka Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imekuwa ikifanya tathmini ya Hali ya chakula nchini lakini pia imekuwa ikitoa chakula cha msaada katika maeneo yenye upungufu wa chakula hii imekuwa ada kwa serikali kufanya hivyo kwa baadhi ya maeneo hapa nchini, hata kama maeneo hayo yamepata uzalishaji wa kutosha wa mazao ya chakula bado Ofisi ya Waziri Mkuu huyapelekea chakula cha msaada baada ya tathmini kuonesha wanaoupungufu wa chakula.

Hali hii inaonesha Tanzania tunacho chakula cha kutosha lakini mantiki ya makala hii inalenga kuuonesha umuhimu wa wananchi kutambua usalama wa chakula ili kuweza kuepuka upungufu wa chakula kwa kuwa chakula kipo chakutosha lakini elimu ya kwa wananchi ya jinsi ya kuweka hifadhi ya chakula hicho ndio muhimu katika nchi yetu ili kaya ziweze kuwa na chakula hicho katika msimu mmoja hadi mwingine.

Kwa takriban watu bilioni moja duniani kote, jitihada za kila siku za kuzalisha, kuuza au kununua chakula ni harakati muhimu sana ambayo sio tu inatambulisha bali pia inakimu maisha yao. Hili ni jambo muhimu kwao, na kwetu sote.

Kukabiliana na tatizo la njaa duniani ni kitovu au msingi wa kile tunachokiita “usalama wa chakula” — kuwajengea uwezo wakulima kuzalisha na kuvuna mazao mengi, kuihudumia vyema mifugo yao au kuvua samaki wa kutosha— na hatimaye kuhakikisha kuwa chakula wanachokizalisha kinawafikia wale wanaokihitaji na hatimaye kukabili upungufu wa chakula.

Waziri wa 67 wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Rodham Clinton aliwahi kusema “ Usalama wa chakula ni suala la kiusalama. Njaa huhatarisha utulivu na usalama wa serikali, jamii na hata mahusiano kati ya nchi na nchi. Watu wanaokufa au waliodhoofika kwa njaa na ambao hawana kipato na hivyo kushindwa kuzihudumia familia zao huji kuta katika hali ya kukata tamaa. Kukata tamaa huko huongeza misuguano, migogoro na hata machafuko. Mwaka 2007, tulishuhudia machafuko yaliyosababishwa na ukosefu wa chakula katika zaidi ya nchi 60.”

Kwa hapa nchini Tanzania kwa kutambua kuwa Usalama wa chakula ni suala la kiusalama serikali kupitia mikoa kwa kushirikaiana na Wizara ya kilimo, chakula na Ushirika imekuwa na mipango endelevu ya kuhakikisha usalama wa chakula nchini ili kupunguza upungufu wa chakula ambao huyakumba baadhi ya maeneo.

Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) mkoani Simiyu, Bw. Joseph Nandira anabainisha kuwa Katika kipindi cha msimu wa 2013/2014, Mkoa ulijiwekea malengo ya kuzalisha jumla ya tani 1,003,578 za mazao ya chakula aina ya nafaka/wanga na tani 150,257 aina ya mikunde. Mavuno halisi yaliyopatikana ni tani 476,024 za chakula aina ya nafaka/wanga na tani 74,944  za chakula aina ya mikunde.

Nandira anaeleza kuwa kutokana na tabia ya wananchi kuuza sehemu kubwa ya chakula ili kukidhi mahitaji ya familia zao, mkoa ulifanya tathmini ya hali ya chakula mwezi Julai 2014, tathimini hiyo ilibaini kuwa Mkoa Unaupungufu wa chakula wa tani 48,975 za nafaka ambao umeanza kuanzia mwezi Oktoba na upungufu huo wa chakula unatarjiwa kuwepo mwezi Novemba/Desemba hadi Februari, 2015 kama wilaya hazitapata msaada wa chakula.

“Tathmini hiyo ilibaini Halmashauri za Wilaya za Busega na Meatu zina upungufu wa chakula kuanzia mwezi Agosti, 2014 hadi Februari, 2015. Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa na Bariadi Mji zina upungufu wa chakula kuanzia mwezi Oktoba, 2014 hadi mwezi Februari, 2015. Ili kukidhi haja ya upungufu wa chakula ndio maana tuliomba  jumla ya tani 48,975 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu.” Alisema Nandira

Nandira anafafanua kuwa ili kuhakikisha tatizo la upungufu wa chakula linakwisha tayari mkoa unayomikakati juu ya Usalama wa chakula ambayo inajikita katika Kuwahimiza wananchi kutumia vizuri chakula kilichopatikana na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima.

Nandira anabainisha kuwa elimu ya usalama wa chakula inajikita katika kuwaelimisha wannachi kuhusu makadirio ya mahitaji ya chakula ngazi ya kaya kwa mwaka pamoja na  Kuwashauri wananchi kuuza sehemu ya mifugo yao na kujinunulia chakula wakati huu ambapo chakula bado kina bei ndogo na kinapatikana ndani ya Wilaya na Mkoa.

“Sisi kama mkoa tunaendelea kuwashauri wananchi kujinunulia chakula kutokana na fedha za mauzo ya pamba. Kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hifadhi bora ya chakula, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vihenge bora/vya kisasa na madawa ili chakula kisibunguliwe na wadudu. Kuwashauri wananchi kuuza ziada ya chakula walichovuna na si vinginevyo” alisisitiza Nandira.

Aidha,  Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa maafa ikiwa na dhamana ya kuratibu shughuli za maafa, imekuwa ikiratibu kwa umakini masuala ya upungufu wa chakula nchini kwa  kufanya Tathmini ya Hali ya Chakula . Hivi karibuni Ofisi hiyo imefanya Tathmini ya Hali ya Chakula na Lishe Mkoani Simiyu katika Wilaya zake zote ambazo ni; Halmashauri za Wilaya za Bariadi, Itilima, Maswa ,Bariadi Mji, Meatu na Busega.

Akiongea mkoani Simiyu kiongozi wa Wataalam wa tathmini mkoani humo ambaye pia ni mratibu wa shughuli za maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Edgar Senga alibainisha kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilifikia maamuzi hayo ya kufanya tathmini mkoani Simiyu baada ya mkoa huo kutuma maombi katika Ofisi hiyo kuwa wana upungufu wa chakula.

“Ofisi ya mkoa ya Simiyu imeleta maombi kwa ofisi ya Waziri Mkuu kuwa wanaoupungufu wa chakula takribani tani 48,975, kwa kuwa Ofisi yetu ndio yenye dhamana ya kuratibu misaada ya chakula hivyo haikuwanabudi kufanya tathmini ya haraka ili kubaini hali ya chakula ya mkoa huu ili kuweza kuamua namna ya kushughulikia maombi yao ya msaada wa chakula”  alisema Senga

Senga alibainisha kuwa Wataalam wa tathimini hiyo wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika katika Idara ya Usalama wa Chakula ambao kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu walitawanyika katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ambapo katika kila Wilaya vilichaguliwa vijiji vitatu vya kufanyiwa tathmini.

“Katika kila kijiji wataalamu hawa watakuwa wanamadodoso ya Wilaya na  kijiji ambayo yatasaidia kutoa taarifa mahsusi za hali ya chakula na Lishe katika ngazi ya Wilaya na Kijiji, lakini pia wataalamu wanayo madodoso ya kaya ambayo yanalenga kupata taarifa za hali ya chakula na Lishe kwa kaya husika kwa vijiji vitakavyoteuliwa  na Serikali za vijiji hivyo. Hii ni kuhakikisha kuwa Serikali inapata taarifa sahihi na hatimaye kuweza kutoa chakula cha kutosha kwa maeneo yenye upungufu wa chakula” alisisitiza Senga.

Mnamo mwaka 2009 katika hotuba yake ya Mwisho wa mwezi Machi, kama ilivyo ada ya kuongea na wanachi kila mwisho wa mwezi Rais wa Jamhuri ya Muungano  wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho kikwete alilithibitishia Taifa kuwa hakuna mwananchi atakaye kufa kwa njaa.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kwamba tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha hakuna mtu atakaye kufa kwa njaa.” Alisisitiza  Kikwete

Kimsingi hii inadhihirisha nia thabiti ya serikali ya kuhakikishia wananchi ambao wengi ni wakulima wanapata usalama wa chakula kwani upungufu wa chakula huathiri jamii kupata nguvu kazi ya kusukuma gurudumu la maendeleo ambalo kimsingi vijana ndio wanaopaswa kushika usukani wake.

Afisa kilimo wa kata ya mwamanyili Bw Mashima  Eliasi anaeleza kuwa yeye kama kijana ambaye ni mtaalam wa kilimo anadhihirisha kuwa vijana katika kata yake wanalima kwa bidii lakini elimu ya usalama wa chakula inakuwa kikwazo kikubwa hivyo huathiri juhudi zote wanazokuwa wamezifanya za kulima mazao ya na kuvuna chakula cha kutosha.

“Hebu fikiria kijana wa hapa kijijini ametumia miezi kadhaa kulima pamba au mpunga kavuna mazao ya kutosha jambo la kwanza anafikiria kutatua matatizo ya familia yake kwa kutumia mazao hayo lakini bila elimu ya  hifadhi bora ya chakula, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vihenge bora/vya kisasa na madawa ili chakula kisibunguliwe na wadudu. Kushauriwa kuuza ziada ya chakula walichovuna hatima yake yeye anauza tu chote alichovuna hatimaye jamii ya Mwamanyili inapata upungufu wa chakula” alisema Mashima

Kukabiliana na tatizo la njaa duniani ni kitovu au msingi wa kile tunachokiita “usalama wa chakula” — kuwajengea uwezo wakulima kuzalisha na kuvuna mazao mengi, hifadhi bora ya chakula— na hatimaye kuhakikisha kuwa chakula wanachokizalisha kinawafikish katika msimu mwingine wa kilimo.

Elimu ya Usalama wa chakula ikitolewa kwa wananchi nchini Upungufu wa chakula nchini unaepukika hii ni kutokana na kuwa kwa hata wananchi wakipata mavuno makubwa au madogo watakuwa wanajua matumizai sahihi ya kaya zao hivyo mavuno yakiwa makubwa wanweza jua kiasi cha kuuza na cha kutunza katika hifadhi bora ya chakula, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vihenge bora/vya kisasa na madawa ili chakula kisibunguliwe na wadudu.

Aidha, Elimu ya Usalama wa chakula itawawezesha wanachi kujua jinsi ya kuukabili upungufu wa chakula wakati mavuno yakiwa kidogo kwa kuuza sehemu ya mifugo yao na kujinunulia chakula wakati huu ambapo chakula bado kina bei ndogo na kinapatikana ndani ya Wilaya na Mkoa pamoja na kujinunulia chakula kutokana na fedha za mauzo ya mazao ya biashara wanayolima hatimaye Ofisi ya Waziri Mkuu inaweza kuwa haipeleki chakula cha msaada katika maeneo mengi ya hapa nchini.

Mwisho.

FilenameMAKALA -SIMIYU.doc
FilesizeEmpty
Filetypedoc (Mime Type: application/msword)
Creatorfrancisca.swai
Created On: 09/25/2014 07:11
ViewersEverybody
Maintained byEditor
Hits1887 Hits
Last updated on 11/03/2014 07:15
Homepage
CRC Checksum
MD5 Checksum
Our website is...
 
mod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_countermod_vvisit_counter
mod_vvisit_counterToday105
mod_vvisit_counterYesterday117
mod_vvisit_counterThis week284
mod_vvisit_counterLast week825
mod_vvisit_counterThis month2169
mod_vvisit_counterLast month3455
mod_vvisit_counterAll days513804
Copyrights ©2013, The United Republic of Tanzania, Prime Minister's office All Rights Reserved